Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI mara tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki
tarehe 21 Juni 1963, kunako tarehe 10 Agosti 1964, Papa Paulo VI akachapisha Waraka
wake wa kwanza wa kichungaji, unaojulikana kama "Ecclesiam Suam" "Kanisa la Bwana",
Waraka unaonesha dira na mwelekeo wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu
ya Ukristo, kwa kuzingatia changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili
wa Vatican.
Ni katika mwelekeo huu, Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI akafanya
hija ya kitume Nchi Takatifu ili kukutana na kusali na Patriaki Anathegoras, mwanzo
wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa. Papa Paulo VI katika Waraka
huu analitaka Kanisa kutambua dhamana na wajibu wake; kuanza mchakato wa kujipyaisha
kwa kujielekeza katika majadiliano ya kidini na kiekumene, ili dunia iweze kuwa ni
mahali pazuri zaidi pa kuishi.
Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI anapenda kuwaambia
watu wa mataifa kwamba, Kanisa limebarikiwa kuwa na amana ambayo watu wanaitafuta
katika historia ya maisha yao. Ni Waraka unaojikita katika fadhila ya mapendo kwa
Mungu na jirani. Ni kutokana na mwelekeo huu, Kanisa halina budi kuwashirikisha watu
upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Watu watambue kwamba, Kristo
ndiye ile hazina iliyofichika machoni pa wengi, lakini ni muhimu sana katika maisha
ya watu.
Tafakari ya kina iliyofanywa na Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI, ilihitimishwa
tarehe 11 Julai 1964. Kuanzia tarehe 6 Agosti 1964 alianza utume wake mjini Vatican,
wakati Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Siku kuu ya Kung'ara kwa Bwana, kielelezo
cha ufunuo wa Mungu na utukufu wa Kristo, ili kuwaimarisha Mitume wake waweze kukabiliana
barabara na Kashfa ya Msalaba. Miaka kumi na minne baadaye, Papa Paulo VI tarehe 6
Agosti 1978, akiwa Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, akafariki dunia, huku akiwa anasali,
ile sala kuu, yaani Sala ya Baba Yetu.