Kardinali Andrew Yeom Soo-jung, Askofu mkuu wa Jimbo kuu Seoul, Korea ya Kusini anasema,
hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Korea ya Kusini kuanzia tarehe 13
hadi tarehe 18 Agosti 2014 kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya sita ya vijana wa
Bara la Asia ni tukio la aina yake kwa wananchi wote wa Korea.
Ni matumaini
ya Kanisa nchini Korea kwamba, Baba Mtakatifu Francisko atasaidia mchakato wa kuziunganisha
Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini; nchi pacha ambazo kwa zaidi ya miaka hamsini
zimekuwa zikiangaliana kwa “macho ya makengeza”.
Kardinali Andrew anasikitika
kusema kwamba, kukosekana kwa majadiliano ya kina kati ya Korea ya Kusini na Korea
ya Kaskazini ni mambo ambayo yanatishia amani, usalama na ustawi wa wananchi wa pande
hizi mbili, ambao kimsingi wanapaswa kuwa kweli ni wamoja. Hija ya kitume ya Baba
Mtakatifu Francisko nchini Korea, inaweza kuwa ni mwanzo mpya wa mchakato wa majadiliano
na upatanisho kati ya Nchi hizi mbili.
Hii inatokana na ukweli kwamba, Baba
Mtakatifu Francisko ni kiongozi anayependa kuona haki na amani vikitawala, sanjari
na utunzaji bora wa mazingira pamoja na kutetea utu na heshima ya binadamu. Haya ni
mambo msingi ambayo ameyaonesha tangu awali kabisa alipochagulia kuliongoza Kanisa
Katoliki. Haki na amani, utu na heshima ya binadamu ni dhana inayomwilishwa katika
uhalisia wa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama ilivyojionesha wakati
wa hija yake ya kitume katika Nchi Takatifu.
Wananchi wa Korea wanaweza hata
wao kuishi katika umoja na udugu. Licha ya kinzani zinazoendelea huko Mashariki ya
Kati, lakini Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Juni 2014 aliweza kuwakutanisha
Marais wa Palestina na Israeli mjini Vatican ili kusali kwa ajili ya kuombea amani
huko Mashariki ya Kati. Hii ni mbegu ya amani iliyopandwa katika mioyo ya watu, itazaa
matunda kwa wakati wake.
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko hapo
tarehe 18 Agosti 2014 kabla ya kukunja vilago na kurejea tena mjini Vatican ataadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea amani na upatanisho nchini Korea. Tarehe
10 Agosti 2014 mjini Geneva, Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeandaa Ibada maalum
ya kiekumene kwa ajili ya kuombea amani na upatanisho kati ya Korea ya Kusini na Kaskazini.