Papa aendelea na Katekesi yake kwa mahujaji na wageni.
Jumatano hii, Baba Mtakatifu Francisko, alianza tena kutoa katekesi kwa mahujaji na
wageni, hapa Vatican licha ya kuwa kipindi cha mapumziko katika kipindi cha joto kali.Papa
akiwa tofauti na watangulizi wake , ameamua kubaki katika makazi yake ya Vatican badala
ya kwenda nje ya Vatican.
Katekesi yake ya Jumatano hii, iliendelea kutoa
tafakari juu Kanisa, Taifa la Mungu. Alisema, Kanisa likiwa limeandaliwa tangu katika
Agano la Kale na kujengwa na Kristo katika utimilifu wa wakati, Kanisa linakuwa ni
watu wapya, waliojengwa katika Agano Jipya.
Papa Francisco amefafanua kwamba,
upya unaoletwa na Kristo, hauweki kando kile kilichoandaliwa kabla, , lakini hukamilisha
yaliyoandaliwa. Katika maandiko, Matakatifu Yohana Mbatizaji, ni kiungo kati ya
ahadi na unabii wa Agano la Kale na utimilifu wao katika Agano Jipya. Yohana anasema,
aliendelea kueleza Papa, kwamba, anamtaja Yesu na kututaka sisi tumfuate, kwa kufanya
toba na kubadilika. Na sheria mpya ambayo Yesu anatoa katika Hotuba ya Mlimani ,
ilikamilisha sheria aliyopewa Musa juu ya Mlima Sinai.
Yesu katika hotuba
yake ya Heri aliyoitoa milimani , anatuonyesha njia ambayo, pamoja na neema yake,
tunaweza kufikia furaha halisi. Anatuambia, katika Injili ya Mathayo, kwamba maisha
yetu ya Kikristo yatahukumiwa kwa jinsi gani tulimtendea yeye kupitia watu wadogo
na hasa watu waliotupwa pembezoni na jamii na watu maskini wahitaji.
Na kwamba
katika moyo wa agano jipya, tunapata kutambua kwamba, ndani ya Kristo , tunakumbatiwa
na neema na huruma ya Mungu, na kwamba maisha yetu lazima yaonyeshe ushuhuda wa upendo
wake alioutoa kwa watu wote wake kwa waume.
Kama kawaida Papa baada ya kukamilisha
Katekesi yake alisalimia makundi mbalimbali ya watu waliofika kumsikiliza . Katika
katekesi hii kulikuwa na makundi makubwa ya watu Uingereza, Norway, Zimbabwe, Japan
na Marekani. Na kwao wote aliwapa baraka zake kwao na familia zao akiwaombea furaha
na amani katika Bwana Yesu.