Kanisa laomba siku tatu za toba na mafungo kupambana na ebola
Katika kikao maalum kilichojumuisha viongozi wa Makanisa nchini Liberia, Maaskofu
Katoliki , Wachungaji na wakuu wa makanisa mengine mbalimbali, kwa lengo la kujadili
jinsi ya kupambana na virusi vya ebola vilivyotia hofu kubwa raia wa Liberia,viongozi
hao wanasema, jibu la kwanza kwanza kabisa ni kumlilia Mungu mwenye uweza wa kusitisha
uwepo wa virusi hivyo vinavyokatisha maisha ya watu bila huruma. Kwa ajili hiyo Kanisa
limetoa wito kwa watu wote, kuwa na siku tatu za mafungo na toba kama hatua ya kupambana
na ebola.
Kikao hicho kilifanyika chini ya uenyekiti wa Rais wa Baraza la
viongozi wa Kidini uliofanyika hapo tarehe 30 Julai 2014, katika Kanisa la Kiinjili
la Mtakatifu Stephano, kilihudhuriwa na viongozi wa Kanisa kutoka pande zote za Liberia.
Katika kikao hicho , Viongozi hao walipendekeza siku hizo tatu za mafungo na toba
zianze Jumatano hii tarehe 6 Agosti hadi Ijumaa ijayo , watu wabaki majumbani mwao
kusali na kufunga , kumlilia Mungu kwa bidii, aliepushe taifa lao na janga hili la
ebola. Uwe ni wakati pia wa kuwaombea baraka na usalama wafanyakazi wote wa afya wanaohudumia
wagonjwa wa ebola kwa wakati huu.