2014-08-05 10:59:03

"Nitabaki nchini Libya hadi kieleweke!"


Monsinyo Giovanni Innocenzo Martinelli, Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Tripoli, Libya anasema, kwa sasa hali ni mbaya sana nchini Libya kwani kuna mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yanayoendelea kila kukicha. Kuna uharibifu mkubwa wa miundo mbinu na mali za watu. Watu wamechanganyikiwa kutokana na mashambulizi yanayofanywa na vikundi mbali mbali vya kijeshi vilivyogawanyika nchini Libya, kila kikundi kinataka kutawala.

Monsinyo Martinelli anasema kwa sasa watawa wote waliokuwa wanatoa huduma hospitalini wamekwishaondoka na Jumuiya ya Wakristo kutoka Ufilippini ambao walikuwa nchini Libya wameanza hata wao kuondoka, ingawa bado kuna Wakristo waliobaki. Kanisa bado linaendelea kutekeleza utume wake kwa kushirikiana na waamini walei hasa hospitalini ili kuwahudumia watu wanaoteseka kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea nchini Libya.

Hadi sasa hatima ya Libya haijulikani, lakini ni matumaini ya Monsinyo Martinelli kwamba, bado kutakuwepo Wakristo watakaojisadaka kwa ajili ya kuendelea kulihudumia Kanisa na wananchi kwa ujumla. Yeye kwa upande wake, ataendelea kuishi Libya hadi kieleweke na kamwe hatawaacha waamini wake bila ya kuwa na mchungaji katika kipindi hiki kigumu cha maisha yao. Monsinyo Martinelli anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya amani ya kudumu nchini Libya!







All the contents on this site are copyrighted ©.