Kongamano la kwanza la Familia kwa ajili ya Nchi za Amerika ya Kusini linaloongozwa
na kauli mbiu "Mimi na Familia yangu tutamtumikia Bwana", lililofunguliwa mapema siku
ya Jumatatu linatarajiwa kufungwa Jumamosi tarehe 9 Agosti 2014 mjini Panama.
Kongamano
hili ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili
ya Familia itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014.
Kongamano hili limeandaliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribiani. Wajumbe wanaendelea kupembua umuhimu wa
familia katika maendeleo ya kijamii sanjari na mshikamano wa kimissionari.
Hapa
wajumbe wanaangalia fursa, changamoto na matatizo yanayozikabili familia Amerika ya
Kusini katika mchakato wa maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho
na kimwili. Wajumbe wanapenda kutumia fursa hii kwa ajili ya kubainisha sera na mikakati
makini inayoweza kusaidia familia kutekeleza nyajibu zake, kwa kusaidiwa na Serikali
husika.
Mada nyingine zinazofanyiwa kazi kwa wakati huu ni elimu, mawasiliano,
Injili ya uhai, uchumi na mchakato wa Uinjilishaji Mpya unaojikita katika ushuhuda
wa maisha adili na matakatifu. Hapa wajumbe wanashirikishana maisha ya kiroho, ili
kuibua mkakati wa kichungaji utakaofanyiwa kazi kwa ajili ya kuzijengea uwezo Familia
ili ziweze kutekeleza dhamana yake. Kuna sala maalum kwa ajili ya familia na utume
wake, ili kuziwezesha familia kutambua na kuendeleza tunu msingi za maisha ya ndoa
na familia kadiri ya mpango wa Mungu.
Hapa mambo yanayokaziwa ni tunu msingi
za maisha ya kiroho, kijamii na kanuni maadili, ili kujenga ulimwengu unaojikita katika
ubinadamu, upendo na mshikamano wa kweli. Ikumbukwe kwamba, Familia ni chemchemi ya
uhai, udugu, upendo na amani ya kweli!