Papa asema kuweni watu wa huruma, ushirikiano na shukurani..
Jumapili wakati wa sala ya Malaika wa Bwana, Papa Francisco akiuhutubia makusanyiko
ya watu katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, alielekeza mawazo katika
somo la Injili, juu ya mikate na samaki kama ilivyoandikwa katika Injili ya Mathayo
(14:13-21), muujiza wa Bwana Yesu, kulisha watu ya elfu tano kwa mikate mitano na
samaki wawili.
Papa Francisko, alisema somo hili lina mambo matatu muhimu
katika maisha ya kila Mkristo nayo ni: huruma; kushirikiana; shukrani, ambavyo ni
kiini cha Sakramenti ya Ekaristi. "Kristo" alisema Papa Francisko, hakughadhabishwa
na umati wa watu, waliokuwa wakimfuata, kila mahali kwa bidii, bali aliwahurumia
kwa sababu Alijua kwamba, hawamfuati tu kwa sababu za udadisi, lakini walikuwa na
haja. Papa Francisko aliendelea kusema kwamba, uponyaji mwingi wa Kristo, ulifanywa
kwa ishara ya huruma yake. Kwa mifano hiyo Yesu anatufundisha kujali mahitaji ya
watu wahitaji na hasa maskini wetu wenyewe. Mahitaji yetu, hata kama ni halali, kamwe
si ya dharura, kama ya wenzetu maskini, ambao wanakosa mahitaji muhimu katika maisha.
Akiligeukia
kugawana mkate , Papa Francisko, alilinganisha majibu ya wanafunzi wakati wanakabiliwa
na watu wengi wahitaji, na jibu la Yesu. Wanafunzi wanaona ni halali kuwaambia watu
waondoke waende kujitafutia kwingine chakula, lakini Yesu anawaambia, waliulishe umati
wa watu huo kwa chakula walichokuwa nacho. Katika hili Papa alieleza, tunaona mambo
mawili , wanafunzi wanafikiri na kutoa jibu kwa mtazamo wa kidunia, ambamo kila mmoja
na ajitunze mwenyewe, Na Yesu anatoa jibu katika mantiki ya Kimungu, ambayo ni ile
ya kugawana kilichopo. Na hivyo kwa Mantiki ya Kimungu watu walikula hadi kutosheka
na kusaza. Hii ilikuwa ni ishara inayotualika tujenge imani kwa Mungu. Na kwamba Mungu
wa huruma, hatulazimishi sisi kwenda nje kutafuta mkate wetu wa kila siku, iwapo tunajua
jinsi ya kugawana na ndugu zetu wake kwa waume wahitaji, kile tulicho nacho.
Na
tatu katika ujumbe wake, Papa alizungumzia juu ya ekaristi, ujumbe unaosikika wakati
Yesu akiubariki Mkate kuugawa katika umati wa watu . Inasemekana ni tendo hilohilo
alilolifanya katika karamu yake ya mwisho, wakati alipoweka kumbukumbu ya kudumu ya
sadaka yake ya ukombozi, kumbukumbu kwamba, si mkate wa hapa duniani, lakini mkate
wa uzima wa milele, zawadi ya Kristo ya Nafsi yake, anaitoa Yeye mwenyewe kwa Baba
kwa upendo kwa ajili yetu.
Papa Francisko alihitimisha kwa sala ya Mama
yetu, Mama wa Maongozi ya Mungu, ili aweze kuongozana na sisi katika hija yetu ya
kidunia na atusaidie sisi katika jitihada za kukidhi mahitaji ya wale tunao kutana
nao njiani katika roho ya udugu.