Kutolipa ada kutaharibu ubora wa elimu nchini Kenya
Askofu Maurice Muhatia Makumba, mwenyekiti wa Idara ya Elimu na dini na shuleni, Baraza
la Maaskofu Katoliki Kenya anasema kwamba, amri iliyotolewa na Serikali ya Kenya kuwataka
wamiliki wa shule kutoa vyeti vya wanafunzi waliohitimu shule ni jambo ambalo linaweza
kusababisha madhara makubwa katika ubora wa elimu inayotolewa nchini Kenya.
Askofu
Makumba anaishauri Serikali kutafuta njia muafaka itakayowawezesha wazazi kulipia
gharama ya elimu wanayodaiwa shuleni badala ya kutoa amri ambayo ina madhara makubwa
katika ustawi na maendeleo ya sekta ya elimu nchini Kenya. Mwelekeo huu unaweza kuwachochea
wazazi na walezi nchini Kenya kutolipa ada ya shule kwa watoto wao kwa makusudi kwani
Serikali inawakingia kifua.
Shule zitakabiliwa na hali ngumu ya uendeshaji
wa shughuli zake, ikiwa kama wazazi na walezi wanahamasishwa kutolipa ada ya shule
matokeo yake uborwa wa elimu utapungua kwa kiasi kikubwa! Bodi za shule zipewe dhamana
ya kuangalia wazazi wale ambao wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kiasi cha kushindwa
kulipa ada, ili waweze kupewa msamaha. Serikali ya Kenya hivi karibuni imetangaza
mkakati wa kutaka kupunguza gharama katika sekta ya elimu, ili kutoa fursa kwa wakenya
wote kufaidi matunda ya elimu, wazo ambalo limebezwa na Umoja wa Walimu wa Shule za
Msingi nchini Kenya, (KUPPET).