Mpendwa msilikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo!
Karibu katika kipindi chetu tuendelee kuitafakari familia kama shule ya fadhili na
maadili. Katika vipindi vilivyopita, tulijaribu kuitazama fadhila ya unyenyekevu na
umuhimu wake katika jamii ya watu. Tulihitimisha vipindi vyetu kwa kualikana kuwa
tuwe wanyenyekevu katika yote, na kwa njia hiyo tutainuliwa katika yote na tutajenga
amani na wenzetu.
Tunakamilisha
somo letu lile kwa kutafakari kilema ambacho kinapingana moja kwa moja na fadhila
ya unyenyekevu, nacho si kingine bali ni kiburi. Kiburi ni hali ya kujiona na kujidhani
kuwa umekamilika katika yote na juu ya yote, na hivyo huhitaji neno wala chochote
kutoka kwa yoyote.
Kilema cha kiburi huendana na tabia za majivuno, kujikweza,
kujisifu, ukaidi, kujiamini kupita kiasi, maringo na dharau. Pamoja nazo kinaambatana
pia na tabia za kutoambilika, kutoulizika, kutoshaurika na kutoonyeka. Kiburi ni
kilema kibaya sana kwa sababu ndiyo kinachotutenga na wanadamu wenzetu na mwisho kinatutenga
na Mungu. Mbaya zaidi, huweza pia kubadili hulka yetu kama asemavyo Mt. Augustino,
“kiburi kiliwafanya malaika wakawa mashetani”. Na sisi tuwapo na kiburi huwa tunakuwa
ni shetani na ndiyo maana katika kiburi twafanya mambo mengi ya kishetani-shetani.
Watu
wenye kiburi wanatazamwa na maandiko matakatifu kama ishara pia ya mwisho wa nyakati.
Mwisho wa nyakati uliyojaa uangamizi huashiriwa na jinsi watu walivyo na kiburi. Neno
linasema “...katika siku za mwisho...watatokea watu wasio na upendo mioyoni, wasio
na huruma, wachongezi, walafi na wakali..., wakaidi na waliojaa kiburi” (rej. 2Tim
3:1-9). Kiburi ni ishara ya uangamizi na maandiko yanaonesha wazi, mwisho wa mwenye
kiburi sio mwema; na hata historia zinatushuhudia pia, wenye kiburi wote waliangukia
pua. Mkumbuke Sauli mfalme, kwa kiburi chake aliifukuza neema ya Mungu na Bwana akamkataa.
Badala ya kumtegemea Mungu, kiburi chake kilimtuma awategemee wachawi. (1Nyakt.10:13-14a).
Kiburi
na mtu wa kiburi ni chukizo kwa Bwana. Maandiko yasema “kuna vitu sita anavyovichukia
Bwana, naam vipo saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi mdanganyifu, mikono
imwagayo damu, moyo uwazao mawazo mabaya, miguu myepesi kukimbilia maovu, shahidi
wa uwongo abubujikaye uwongo na mtu apandaye mbegu ya fitina kati ya ndugu” (Mith.
6:16-19). Hapo tunaona wazi msululu wote wa machukizo huo hutoka kwa mtu mwenye kiburi.
Mtu mwenye kiburi kwa kiburi chake yupo tayari kutenda kila aina ya dhambi ndiyo maana
mafundisho ya imani yetu, yanatuelekeza kwamba kiburi ni moja ya mizizi ya dhambi.
Rai tunayoitoa hapa kwa wazazi na wote wenye dhamana ya malezi katika familia
ya mwanadamu ni kwamba, tujitahidi kuwalea watoto wetu katika fadhila njema, na kuwasaidia
wasikomae katika kiburi, kwani kiburi huwapeleka kuishi katika utundu wenye kifo ndani
mwake. Watoto wetu wajengwe katika usikivu na utii kwa wazazi, walimu, walezi na wote
wenye mamlaka halali. Hizi fujo nyingi za vijana zinazosikika mashuleni hata maofisini,
zina msingi katika kiburi tunachokomaa nacho tangu udogoni.
Yoshua Bin Sira
anatuonya sana juu ya madhara ubaya wa kiburi na matokeo yake. Nasi katika tafakari
hii, tunataka tutumie kitabu cha Yoshua Bin Sira kama dira yetu. Mintarafu kiburi,
Yoshua Bin Sira anatuasa “mwenye kiburi ataishia vibaya mwishoni...atalemewa na taabu”
(rej. YbS. 3:26-27). Na haswa wengi huwa tunakuwa watu wema kwa nyakati fulani, lakini
pale tunapoingiliwa na kiburi, basi mwisho huwa unakuwa ni wa aibu. Ili kutuangusha
kwa kutuporomosha kwa aibu na fedheha, shetani hutuinua juu kwa kutujaza kiburi kikavu
kisichorekebishika isipokuwa kwa anguko kuu la aibu.
Kiburi huwafanya wenye
akili waonekane hawana maarifa tena. Historia zinatushuhudia kwamba, wapo watu wengi,
waliokuwa watawala na enzi na mamlaka, walianza kwa uungwana, lakini kwa sababu ya
kiburi chao wakaifukuza neema ya Mungu, mwishoni wakawa chukizo kwa wote.
Daima
na popote, kiburi hubeba mimba ya uharibifu na aibu. Hakuna mwenye kiburi anayeweza
kusimama siku zote. Mwenye kiburi lazima ataangushwa tu, na anguko lake huwa ni la
aibu kuu. Sote daima tunapoiambata fadhila ya unyenyekevu, tuombe neema ya kuepukana
na kiburi. Kilema cha kiburi hutufanya tuchukiwe na watu na tupoteze maana katika
jamii tunamoishi. Kiburi sio uungwana!
Kutoka katika studio za Radio Vatican,
ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.