2014-08-04 08:58:39

Imarisheni maboresho katika miundo mbinu!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa Jiji la Mbeya uongeze mapato yake ya ndani kwa kuweka mifumo ya kisasa ya ukusanyaji mapato. Ametoa agizo hilo Jumamosi, Agosti 2, 2014 wakati akizindua stendi ya kisasa ya mabasi katika eneo la Nane Nane nje kidogo ya Jiji la Mbeya.

“Nikuombe Meya Kapunga, wewe na watu wako ongezeni mapato ya ndani ya Jiji la Mbeya. Wekeni mifumo ya kisasa ya makusanyo inayotumia teknolojia ya habari na mawasiliano, acheni kutumia risiti za kuandika wa mikono,” alisema. Akizungumzia mradi wa stendi mpya ya mabasi, Waziri Mkuu alisema ujenzi wa stendi hiyo ni miongoni mwa kazi zilizo kwenye mradi mkubwa unaohusisha uboreshaji wa huduma na miundombinu kwenye miji na majiji saba hapa nchini (Tanzania Strategic Cities Programme).

Alisema mradi huo uliibuliwa na Serikali tangu mwaka 2006 kwa kushirikiana na Benki ya Dunia. Miji na majiji mengine yanayohusika na mradi huo ni Mwanza, Arusha, Tanga, Kigoma, Mtwara na Dodoma. “Utekelezaji wa miradi katika miji na majiji haya saba, umetuwezesha kupata ufadhili katika awamu ya pili ya mradi huu ambayo itajumuisha miji 17. Tusingekubaliwa kuingia awamu ya pili kama ninyi madiwani msingesimamia vizuri miradi hii,” alisema.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Bw. Mussa Zungiza alisema ujenzi wa stendi hiyo yenye ukubwa wa mita za mraba 30,000 utasaidia kupunguza msongamano wa magari kwenye barabara kuu ya TANZAM ambako mabasi ya mikoani yalikuwa yakisimama na kupakia ama kushusha abiria.

Alisema mradi huo wa stendi ya Nane Nane uliogharimu sh. Bilioni 2.9/- ni sehemu tu ya mradi mzima ambao thamani yake ni sh. Bilioni 31.4 ambazo zimetumika kujenga barabara za kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 23.1, daraja moja na dampo la kisasa la kutupia taka (sanitary land fill) katika kata ya Nsalaga. “Hata hivyo, mradi huo uko chini ya uangalizi wa mkandarasi hadi Desemba 4, 2014 utakapokabidhiwa rasmi kwa Halmashauri ya Jiji, “ alisema Bw. Zungiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Pinda ameutaka uongozi wa Jiji la Mbeya kuhakikisha unatengeneza kwanza miundombinu ya maji na vyoo katika eneo jipya lililopo jirani na stendi mpya ya Nane Nane ambalo limetengwa mahsusi kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama ‘wamachinga’. “Ni vema Jiji litenge kiasi cha fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za muhimu kama maji na vyoo badala kukimbilia kuwalundika mahali hapa. Wafanye biashara zao, na hata mtu akitoka stendi akaja kununua bidhaa zao, kama na shida apate mahali pa kujihifadhi,” alisema huku akishangiliwa na umati uliohudhuria uzinduzi huo.

Aliwataka wawapangie maeneo ya mabanda yao, na ikibidi watafute mwekezaji anayeweza kufanya kazi hiyo. “Tusifanye kosa la kuja kuwalundika tu. Ni heri kugharimika kidogo lakini pawe pazuri. Tengenezeni eneo hili ili kituo chenu kiwe cha mfano na wengine waje waige,” aliongeza.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi (OWM - Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Bw. George Owuor, Kaimu Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Bibi Nora Katabarwa, Wakuu wa Mikoa ya Rukwa, Iringa, Njombe na Katavi ambao walikuwa jijini Mbeya kuhudhuria kongamano la Uwekezaji na wanahudhuria maonyesho ya Nane Nane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.








All the contents on this site are copyrighted ©.