Dini lisiwe ni jukwaa la kuwagawa wananchi kwa mafao ya kisiasa!
Askofu Emmanuel Badejo wa Jimbo Katoliki la Oyo, nchini Nigeria, amewataka wanasiasa
nchini Nigeria kuacha mtindo wa kutumia dini kama jukwaa la kutekeleza matakwa yao
ya kisiasa na matokeo yake wanasababisha kinzani za kidini na migawanyiko ya kijamii!
Uchu wa mali na madaraka na ubinafsi ni kati ya mambo ambayo yameendelea kusababisha
majanga makubwa kwa nchi nyingi Barani Afrika.
Pale ambapo wanasiasa wametumia
dini kama jukwaa la utekelezaji wa utashi wao wa kisiasa, hapo kumekuwepo na kinzani
pamoja na machafuko ya kidini. Hali kama hii ndiyo inayoendelea kujitokeza nchini
Nigeria. Tofauti za kidini na kiimani ni utajiri mkubwa unaoweza kutumiwa kwa ajili
ya ustawi na maendeleo ya nchi husika na kamwe, kisiwe ni chanzo cha kinzani, migongano
na hatimaye vita ya kidini, jambo ambalo kwa sasa limepitwa na wakati.
Askofu
Badejo anasema, wanasiasa wengi nchini Nigeria wameanza kujipanga kwa ajili ya kuanza
mchakato wa uchaguzi mkuu nchini humo, unaotarajiwa kufanyika kunako mwaka 2015. Mashambulizi
ya kigaidi yanayoendelea kufanywa na Kikundi cha Boko Haram sehemu mbali mbali za
Nigeria na kushindwa kwa Serikali kuweza kukidhibiti ni kielelezo wazi kwamba, hapa
si bure, kuna mkono wa baadhi ya wanasiasa ambao wanaunga mkono vitendo vinavyofanywa
na Boko Haram kwa ajili ya mafao yao binafsi.
Inasikitisha kuona kwamba, Nigeria,
iliunda mazingira na hatimaye kuibuka kwa Kikundi cha Boko Haram na sasa Nigeria si
mahali pa amani na utulivu tena, kwani watu wanaishi kwa wasi wasi mkubwa kuhusu maisha
na mali yao!