2014-08-04 09:12:44

Changamoto kwa vyama vya kisiasa Tanzania!


Chama cha Wanataaluma wa Kikristo Tanzania, CPT, hivi karibuni kiliviandikia vyama vya kisiasa nchini Tanzania ujumbe maalum kuhusiana na Bunge maalum la Katiba, kuhusu kuwaangusha watanzania katika mchakato wa Bunge hili, umuhimu wa kujikita katika misingi sahihi ya kisheria pamoja na kuhakikisha kwamba muafaka unafikiwa, ili watanzania waweze kupata Katiba mpya. Kwa undani zaidi endelea kujichotea changamoto hii.

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa Tanzania, kwa heshima na upendo, tunawatumia kwa njia ya Ujumbe huu salaam za Mshikamano, Maridhiano na Amani! Katika Ujumbe wetu huu kwenu, tumezingatia “Ujumbe wa Kichungaji wa Pasaka 2014 kwa Waamini na watu wote wenye mapenzi mema” uliotolewa mwezi Aprili na Maaskofu Katoliki 32.

Tunasukumwa na moyo wa Mshikamano, Maridhiano, na Umoja wa Taifa letu Tanzania na watu wake kwa misingi ya Uhuru, Ukweli, Uwazi na Haki, inayozaa Uvumilivu na Amani ya kweli. Tunaomba na kuasa kuwa Ujumbe wetu huu upokelewe, kama ulivyonuiwa, kama mwaliko wa kuwa na moyo wa kujenga imani, si wa kukatisha tamaa na kutapanya viongozi na watu wote wenye nia na mapenzi mema kwa Wananchi na Nchi yetu Tanzania.

UJUMBE
    Katika Bunge Maalumu la Katiba mmewaangusha Wananchi

Watu wamechoka na mambo mengi yanayoendelea nchini. Tunahisi wanasema: ‘Yatosha’! Wazo la Katiba Mpya linachukuliwa kama nyenzo; watu wameiona kama njia au nyenzo ya kufikia upatikanaji wa mabadiliko wanayoyatamani. Maoni ya Wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Tume ya Warioba) hadharani na kwa njia za wazi yaliwaamsha watu kuhusu dhima yao katika utawala wa Nchi na uundwaji wa Katiba yake.

Walitoa maoni yao wakiwa huru kwa namna na katika njia na majukwaa huru mbalimbali; na walitegemea yabainishwe katika Taarifa na Rasimu ya Katiba rasmi ya Tume ya Warioba. Taarifa na Rasimu rasmi ya Tume ya Warioba vimezingatia kwa kiwango kikubwa maoni yaliyotolewa na Wananchi na kukusanywa na Tume hiyo.

Hata hivyo, hadi sasa, ahadi, iliyo katika Taarifa na Rasimu ya Tume ya Warioba, iko njia panda na imekwama.. Imekwamishwa na wanasiasa katika Bunge Maalumu la Katiba na mtuhumiwa mkuu ni Chama Tawala ambacho, kwa makusudi, kimekataa kuipa Rasimu rasmi ya Katiba hadhi yake stahiki kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka wa 2011 kama ilivyofanyiwa mabadiliko hadi 2013, kifungu cha 25. Masharti ya Kifungu hicho, katika kifungu kidogo cha (2) yanasema kama ifuatavyo:
(2) Mamlaka ya Bunge Maalum ya kupitisha masharti ya Katiba inayopendekezwa yatatekelezwa baada ya Rasimu ya Katiba kuwasilishwa na Mwenyekiti wa Tume na kupitishwa na Bunge Maalum.
Hii inamaanisha na kunuia kwamba (isipokuwa kwa tafsiri tofauti ya mahakama yenye mamlaka), ili “Bunge Maalum kupitisha masharti ya Katiba inayopendekezwa” itazingatia Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na si Rasimu nyingineyo yoyote.

Pasipo shaka, Rasimu ya Tume ya Warioba inaweza kuboreshwa na Bunge Maalum kwa masharti yake kufafanuliwa, kupanuliwa upeo au wigo wake, kuyaimarisha na kuyatengamaza lakini bila kutoka nje ya misingi yake, tunu na nguzo zake za kimsingi zinazotokana na kuaswa kwa kiwango kikubwa na ”’maoni ya wananchi” kwa madhumuni ya kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano.” (Kifungu cha 3 cha Sheria hiyo.)

    Tunahitaji kuanzia kwenye misingi sahihi

Je, watu wanataka nini? Wanataka kuwa wamoja, wenye heshima na wanaothaminiana, kila mmoja akiwa na thamani yake katika jamii.
Msingi wetu wa kina ni utu na tunu za maadili.
Rasimu ya II ya Tume ya Warioba inauwasilisha vyema msingi huu.

    Yabidi juhudi ya kuweka msingi huu ifanywe kidhati katika Bunge Maalum la Katiba

Majadiliano yawe huru, yasibanwe na misimamo ya vyama vya siasa. Vyama vya siasa, ambavyo ni makundi madogo kati ya jamii kubwa zaidi ya Wananchi, viwape wajumbe na wafuasi wao maagizo ya kufuata maoni binafsi ya moyoni na akili zao katika kujadili mawazo, maoni na mapendekezo ya Wananchi yaliyo katika Rasimu ya Tume ya Warioba iliyowasilishwa rasmi na Mwenyekiti wa Tume hiyo kwenye Bunge hilo. Muache kufanya siasa za kivyama kwenye Bunge Maalum la Katiba. Muikubali Rasimu rasmi ya Tume ya Warioba kama inavyotakiwa na sheria kama msingi halali wa kutafuta muafaka wa kitaifa katika Bunge Maalum hilo.

Rasimu hiyo imewasilishwa kwa wananchi na Rais mwenyewe kwa Taarifa yake (Rais) : Toleo hili la Rasimu ya Katiba linachapishwa kwenye Gazeti la Serikali kwa mujibu wa kifungu cha 20(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, na itawasilishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa. Dar es Salaam Jakaya Mrisho Kikwete22 Januari, 2014 Rais

Mh. Rais anawajibika kushauri Bunge Maalum na kuomba radhi
Mh. Rais anawajibika kulishauri Bunge Maalum hilo kufuata njia hii; pia anapaswa kuomba radhi kwa kuondoa mchakato kwenye misingi na njia yake rasmi iliyowekwa kisheria.

    Hatua za kisheria dhidi ya Bunge Maalum?

Kama haya tunayoasa na kushauri hayawezi kupatikana kihiari, itabidi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya Bunge Maalum la Katiba, au kuomba mahakama yenye mamlaka kutoa tafsiri sahihi ya vifungu husika vya sheria na ka kanuni kuhusu mwenendo wa Bunge hilo. Kuna sababu za kisheria za kuhoji utendaji wa Bunge Maalumu la Katiba na hasa ikiwa kutokuwa tayari kuijadili Rasimu rasmi ya Tume ya Warioba kama msingi wa Bunge Maalum mwezi wa Agosti, 2014 kutaendelea.

Hii ni njia isiyoridhisha tukiilinganisha na njia ya kubadilika kwa hiari na kuomba radhi, ambayo ingeacha mwanya wazi na chanya kuanzisha upya mjadala juu ya uundwaji wa Katiba Mpya na kufikia mwafaka na maridhiano ya kitaifa.

    Je, ni busara kuruhusu ukosefu wa muafaka katika Bunge Maalum kuendelea?

Kuruhusu hali ya ukosefu wa muafaka ulioliteka Bunge Maalum kuendelea, na kuwa na suluhu iliyolazimishwa na Chama Tawala kwa Watanzania, si busara na ina hatari ya kuchochea utumiaji wa nguvu katika jamii kwa ujumla, ambao unaweza kujitokeza katika namna mbalimbali tofauti, lakini yote yakileta madhara kwa jamii nzima. Baadhi ya madhara ni kama yafuatayo:





HITIMISHO
Kwa kuhitimisha, tunaviomba na kuviasa Vyama vya Siasa vyenye uwakilishi katika Bunge Maalum, hasa Chama Tawala, kuweka upandeni maslahi ya misimamo yake, wajipambanue kwa hoja madhubuti zenye kufikiria hasa Wananchi na Taifa. Ni kwa maslahi ya Vyama vyote vya Siasa, na hasa Chama Tawala, kubaki na imani ya wananchi. Vinginevyo, watu watahisi wamesalitiwa na watapoteza imani na maelewano na vyama ambavyo hadi sasa wamekuwa wakiviamini na kuvikubalii. Kwenye uchaguzi, wanaweza hata kuvinyima kura.








All the contents on this site are copyrighted ©.