2014-08-02 09:53:24

Mchoko wa imani nchini Benin unapaswa kutafutiwa dawa makini!


Kanisa Katoliki nchini Benin hata katika udogo wake wa eneo, limebarikiwa kuwa na idadi kubwa ya watangazaji wa Injili, wanaochakarika usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba, Injili ya Furaha inawafikia watu wengi zaidi, kwa njia ya huduma makini katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu.

Kanisa nchini Benin linaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu kama sehemu ya mkakati wake wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Huduma hii inafanywa kwa kiasi kikubwa na Mapadre, Watawa na Makatekista. Kanisa Katoliki nchini Benin lina jumla ya Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yapatayo 73 na kati yake Mashirika ya Kitawa kwa wanaume ni 27. Kuna Mapadre wa Majimbo 1, 011 na Mapadre watawa ni 363 na kuna watawa 1, 247 kutoka katika Mashirika 8 yenye hadhi ya kijimbo.

Benin inaendelea kuhimiza mshikamano wa kimissionari kwa kushirikishana rasilimali watu kwa kutuma Mapadre wake ndani na nje ya Benin, tayari kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Takwimu zinaonesha kwamba, Benin imetuma Mapadre wake 206 nje ya nchi kama Wamissionari na kuna idadi kubwa ya Watawa wanaoshiriki pia utume huu kadiri ya Mashirika yao.

Pamoja na mafanikio yote haya, kuna haja wanasema wataalam wa maisha ya kiroho kwa Benin kufanya upembuzi yakinifu ili kuweza kukabiliana na matatizo na changamoto zinazojitokeza ndani ya Kanisa, ili kuwajengea uwezo waamini wa kuwa kweli ni Wakristo na Waafrika pasi na kuchanganya mambo.

Tamaa ya utajiri wa haraka haraka; uponywaji kwa njia ya miujiza na kuteteleka kwa maadili ni kati ya mambo yanayopaswa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu kwa njia ya Katekesi ya kina na makini; utamadunisho, ili kweli Injili iweze kugusa undani wa maisha ya watu, tayari kutolea ushuhuda wa imani katika matendo. Waamini wengi wanahudhuria Ibada mbali mbali zinazoadhimishwa na Mama Kanisa, lakini, wanapokumbwa na matatizo pamoja na changamoto za kiimani, waamini hao wanajikuta wamelegea kiasi hata cha kumezwa na malimwengu.

Hii inaonesha kwamba, kuna mchoko wa maisha ya kiimani na kimaadili, hali inayopaswa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu. Pengine, umefika wakati kwa Waamini kupatiwa Katekesi ya kina kuhusu: Imani, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa; Maisha adili yanayojikita katika Amri za Mungu sanjari na Maisha ya Sala. Kwa maneno mengine, Katekesi awali na endelevu ni muhimu sana kwa waamini Barani Afrika, ili waweze kuwa kweli ni mashahidi wa Kristo na Kanisa lake katika ulimwengu mamboleo.







All the contents on this site are copyrighted ©.