2014-08-02 11:47:40

Kumbu kumbu ya vita kuu ya kwanza ya dunia, ni changamoto ya kujikita katika msingi wa haki na amani!


Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linasema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka mia moja tangu Vita kuu ya kwanza ya dunia ilipotokea, iwe ni fursa kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuchuchumilia misingi ya haki, amani na utulivu. Canada iliingia rasmi katika vita kuu ya kwanza ya dunia hapo tarehe 4 Agosti 1914 kwa kushirikiana na Uingereza dhidi ya Ujerumani iliyokuwa imevamia Ubelgiji.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linasema kuna haja ya watu kutofautisha kati ya vita na madhara yake, kwani kimsingi haipaswi kabisa kusherehekea majanga yaliyosababishwa na vita na badala yake kuwaheshimu Askari waliojitoa mhanga, ili kupambana na udhalimu, wakakubali kupoteza maisha yao, kupata vilema na majeraha makubwa. Kwa maneno mengine, Askari wamekuwa ni wahanga wa kwanza wa vita kuu ya kwanza ya dunia.

Waamini wanaomboleza kutokana na vifo vyao na kuwaombea pumziko la amani, huko mbinguni, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu. Katika vita kuu ya kwanza dunia wahudumu wa maisha ya kiroho walifanya kazi kubwa ya kuwasindikiza Askari pamoja na familia zao; kiasi kwamba, wakawa kweli ni mwanga wa matumaini katika maeneo ambamo mtutu wa bunduki ulikuwa unatawala.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linasema, amani ni jina jipya la maendeleo kama anavyokazia Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI. Vita itaendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu: Ukosefu wa fursa za ajira, njaa, dhuluma na hali ya kukata tamaa. Kutokana na changamoto hizi, kuna haja ya kujenga dunia ambamo haki na amani vinatawala.

Ni wajibu wa Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashahidi wa haki na amani; wafuasi na wamissionari wa Mfalme wa amani, tayari kutangaza Injili ya Furaha kwa watu wa mataifa!







All the contents on this site are copyrighted ©.