Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, CCEE linaendelea kufuatilia
kwa umakini mkubwa myumbo wa miito ya maisha ya kipadre na kitawa Barani Ulaya sanjari
na kushuka kwa idadi ya waamini wanaoshiriki katika maisha na utume wa Kanisa; yaani
waamini wanaohudhuria Ibada na Liturujia mbali mbali kama sehemu ya mchakato wa maisha
yao ya Kikristo.
Maaskofu wanatambua
changamoto hii na ndiyo maana wameamua kuifanyia kazi katika mkutano wa wakurugenzi
wa miito kutoka Barani Ulaya uliofanyika hivi karibuni Jimboni Varsavia, Poland. Ili
kuzungumzia wito na maisha ya Kipadre na Kitawa, waamini wanapaswa kwanza kabisa
kumtambua Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Hapa ni mwanzo
wa hija ya maisha na utume wa Kipadre.
Kumbe, kuna haja kwa Kanisa kukazia
majiundo yatakayowasaidia vijana kumfahamu Yesu Kristo, ili waweze kuwa tayari kujisadaka
kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Majiundo ya awali na endelevu ni muhimu sana katika
hatua mbali mbali za maisha ya vijana wanaonesha ari na wito wa kutaka kuwa Mapadre
na Watawa.
Hata leo hii, Mwenyezi Mungu anaendelea kuwaita vijana kutoka sehemu
mbali mbali za dunia, ili waweze kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, licha
ya changamoto na vizingiti ambavyo vijana wanakabiliana navyo katika hija ya majiundo
yao. Watu wengi wanaendelea kumezwa na malimwengu kiasi cha kushindwa kutoa kipaumbele
cha pekee kwa uwepo wa Mungu katika maisha yao.
Majiundo ya Kipadre yatoe
kipaumbele cha pekee kwa Majandokasisi kumfahamu, kumpenda na hatimaye waweze kujitoa
kumtumikia Yesu, Kanisa na jirani zao kwa kutambua kwamba, wito wao ni zawadi kubwa
kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowawajibisha.
Yesu anaendelea kuwaita vijana
na wasichana kumfuasa katika maisha ya Kipadre na Kitawa, ingawa takwimu zinaonesha
kwamba, hali ya miito ya maisha ya Kipadre na Kitawa Barani Ulaya inachechemea kwa
kasi ya ajabu, changamoto ya kuibua mbinu na mikakati ya shughuli za kichungaji, ili
kuwasaidia vijana kutambua na kuimarisha miito yao kwa kufanya maamuzi magumu kama
anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.
Miito inaweza kuzaliwa, kukuzwa na kuendelezwa,
ikiwa kama waamini watatambua dhamana yao katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini
wajenge na kukuza moyo wa Sala, Ibada na ushiriki wa Sakramenti za Kanisa hasa Ekaristi
Takatifu na Kitubio; Sakramenti zinazowaonjesha waamini huruma na upendo wa Mungu
pamoja na kuwapatia nguvu ya kusonga mbele katika kumshuhudia Kristo kwa kujisadaka
kwa ajili ya jirani zao.
Kuna haja kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko
kwa waamini kujenga na kuimarisha urafiki na Yesu pamoja na Mapadre na Watawa wenyewe
kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Vinginevyo ni kuendelea kumpigia Mbuzi gitaa
pasi na mafanikio yanayokusudiwa!