Injili ya Kristo, Familia na Uhuru ni mambo yanayopaswa kushibana pasi na ukinzani!
Hati ya kutendea kazi kwa ajili ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia
itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014 inaonesha
utajiri mkubwa na uchambuzi wa kina uliofanywa kwa kuangalia matatizo, changamoto
na fursa zilizopo katika maisha na utume wa Familia.
Mababa wa
Sinodi watakuwa na fursa kwa kipindi cha miaka miwili kuweza kusali, kutafakari na
hatimaye kutoa suluhu kwa changamoto ambazo zinaikumba familia katika ulimwengu wa
utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Matatizo na changamoto za
kifamilia ni mwaliko kwa Mama Kanisa kuwatangazia tena watu Injili ya Familia, itakayogusa
undani na vipaumbele vya maisha yao; uhuru na dhamana yao kwa kushiriki kikamilifu
katika kazi ya uumbaji na malezi ya Kikristo kwa watoto wao sanjari na kudumisha misingi
ya maadili na utu wema.
Watu watambue kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano
wa Mungu jambo linalojenga mahusiano ya pekee na Mwenyezi Mungu anayeheshimu na kuthamini
uhuru wa mwanadamu. Mwenyezi Mungu amempatia mwanadamu Amri na Maagizo yake ambayo
yanapaswa kutekelezwa kwa dhati kama kielelezo cha upendo kwa Mungu. Uhuru ni dhana
pevu ambayo ni sehemu ya utamaduni, Mapokeo na Mafundisho ya Kikristo.
Kila
mtu anao uwezo wa kujichagulia mfumo wa maisha yake. Dhana ya uhuru wanasema wachunguzi
wa mambo ya maisha ya kiroho na kimaadili “imechakachuliwa” na wajanja wachache kiasi
kwamba inaanza kupoteza dira na mwelekeo wake. Uhuru unawapatia watu kuamua kuoa au
kutokuoa; kuwa na watoto au kuendelea kula kuku kwa mrija pasi na bughuza na kero
za watoto. Yote haya yanajikita katika dhana ya uhuru binafsi.
Utume wa familia
unahitaji mwelekeo tofauti kabisa wa kutambua dhana ya uhuru, kwani hapa kunahitajika
ukomavu wa kimaadili, utu na maisha ya kiroho mintarafu dhana ya uhuru wa mtu. Waamini
watambue na kuthamini uhuru wao wa kuwa kweli ni Watoto wa Mungu, kwa kuepuka kishawishi
cha ubinafsi kinachokwamisha hata wakati mwingine mahusiano ya kijamii. Uhuru wa waamini
unapaswa pia kuzingatia Mafundisho ya Kanisa, Maadili na Utu wema.
Hapa kuna
haja ya kuheshimu kanuni na sheria maadili, kwa kufuata dhamiri nyofu, ili kukuza
na kudumisha mahusiano mema ndani ya jamii. Ndiyo maana Kanisa katika mapambazuko
ya Millenia ya tatu ya Ukristo linataka kujikita zaidi katika Uinjilishaji Mpya unaozingatia
ushuhuda wa maisha adili na matakatifu kwa kuwataka waamini kuwa kweli ni chachu ya
kuyatakatifuza malimwengu.
Mchakato huu uwasaidie waamini kutambua umuhimu
wa Mafundisho ya Kanisa na kujitahidi kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha yao,
kwa kutambua thamani kubwa ya uhuru ambao wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu; uhuru unaowawajibisha
katika maisha yao ya kiroho na kimaadili; uhuru pasi na mipaka ni utumwa na majanga
katika maisha ya watu!