Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu,
mwingi wa rehema, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kwa mara nyingine tena kuzungumza
na taifa juu ya masuala muhimu yanayohusu nchi yetu. Mwezi wa Saba tunaoumaliza leo
ulikuwa na matukio mengi baadhi yakiwa makubwa na kushtusha na mengine yalikuwa matukio
ya kawaida.
Mashambulio ya Mabomu
Ndugu Wananchi;
Tarehe 3
Julai, 2014 na tarehe 07 Julai, 2014 kulitokea mashambulizi ya mabomu nyumbani kwa
Sheikh Sudi Ally Sudi na katika mgahawa wa Vama kwa mfuatano huo. Kabla ya hapo, kulikuwa
na matukio mengine matatu: Kanisa la Olasiti tarehe 5 Mei, 2012, Mkutano wa Kampeni
wa CHADEMA tarehe 15 Juni, 2013 na Baa ya Arusha Night Park tarehe 13 Aprili, 2014.
Hali kadhalika, tarehe 13 Juni, 2014 kulitokea shambulizi la mabomu katika eneo la
Darajani, Zanzibar.
Kila lilipotokea shambulizi uchunguzi ulifanyika na watuhumiwa
kukamatwa. Lakini, watuhumiwa waliokamatwa safari hii wanaelekea kutoa sura nzuri
zaidi ya mtandao wa watu wanaofanya vitendo hivi vya kikatili pale Arusha na kwingineko
nchini. Watu 38 wameishafikishwa Mahakamani, wengine 8 watafikishwa Mahakamani kesho
na uchunguzi na msako unaendelea kote nchini kuwapata watuhumiwa wengine.
Napenda
kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa
kazi kubwa na nzuri iliyotufikisha hapa tulipo sasa. Tunawaomba waongeze bidii, maarifa
na ushirikiano mpaka wote waliohusika wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Aidha,
natoa pongezi na shukrani maalum kwa wananchi wema waliotoa taarifa zilizowezesha
kukamatwa kwa watuhumiwa. Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi wananchi wenye taarifa
kuhusu wanaotafutwa au ye yote anayejihusisha na vitendo hivi viovu watoe taarifa
kwenye vyombo vya usalama ili hatua zipasazo zichukuliwe.
Kutupwa Viungo vya
Binadamu
Ndugu Wananchi;
Tarehe 22 Julai, 2014, katika Bonde la Mto
Mpiji lililopo eneo la Bunju Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, viligunduliwa viungo
vya binadamu na baadhi ya vitendea kazi vya madaktari vikiwemo aprons na gloves. Viungo
hivyo vilivyokutwa vimekakamaa na kuhifadhiwa katika mifuko myeusi 85, vilikuwa vimetupwa
jana yake tarehe 21 Julai, 2014. Tukio hilo lilileta taharuki na hofu kubwa katika
Jiji la Dar es Salaam na nchini kwa ujumla.
Uchunguzi uliofanywa uligundua
kuwa viungo hivyo vilikuwa vinatumika kufundishia wanafunzi wa udaktari katika Chuo
Kikuu cha Tiba kilichoko Mbezi Beach maarufu kwa jina la IMTU. Ni utaratibu wa kawaida
kwa vyuo vikuu vya udaktari nchini na kote duniani kutumia miili ya wanadamu waliofariki
kufundishia. Hata hivyo, pale viungo hivyo vinapokuwa havihitajiki tena kwa shughuli
hiyo, zipo taratibu zake za kuvisitiri ambazo hazikufuatwa. Bahati nzuri mamlaka husika
zimeona kasoro hiyo na hatua zimeanza kuchukulikuwa.
Tuziachie mamlaka hizo
kuchukua hatua zipasazo kwa mujibu wa madaraka yao na kwa mujibu wa Sheria na Kanuni
zinazotawala shughuli za namna hiyo. Ni matumaini yangu kuwa yaliyofanywa na IMTU
hayatafanywa tena na Chuo hicho wala chuo kingine cho chote hapa nchini.
Ziara
Yangu Mikoani
Ndugu Wananchi;
Katika mwezi huu wa Julai, nimefanya ziara
katika ya mikoa ya Tanga na Ruvuma. Nimefurahishwa sana na hatua kubwa ya maendeleo
waliyopiga wananchi wa mikoa hiyo. Pamoja na mchango wa Serikali, ari na mwamko mkubwa
wa kujiletea maendeleo walionao viongozi na wananchi wa mikoa hiyo vimechangia sana
katika kuongeza kasi ya maendeleo na mafanikio yanayoendelea kupatikana. Katika ziara
hizo, nilizindua miradi iliyokamilika na kuweka mawe ya msingi ya ujenzi wa miradi
mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ile ya barabara, umeme,maji, afya, elimu, majengo
ya Serikali, nyumba na kadhalika.
Nimepata faraja kubwa kupata taarifa kuwa
ahadi zangu nyingi na zile zilizomo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi zimekamilika
na zingine ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Ndoto ya miaka mingi, kabla
na baada ya Uhuru, ya wananchi wa Mikoa ya Kusini ya kutaka Mikoa yao ifunguke na
kuunganishwa na mikoa mingine kwa barabara za lami sasa kuna uhakika wa kukamilika.
Barabara ya kutoka Mbinga, Songea hadi Namtumbo iliyojengwa kwa msaada wa Serikali
ya Marekani imekamilika na tuliizindua. Tuliweka mawe ya msingi ya kujenga barabara
ya lami kutoka Namtumbo, Tunduru, Mangaka hadi Mtambaswala kwenye Daraja la Umoja
linalounganisha Tanzania na Msumbiji kwa msaada wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na
Serikali ya Japan. Barabara ya kutoka Mangaka hadi Masasi iliyojengwa kwa msaada wa
Serikali ya Japan imekamilika na tuliizindua. Katika barabara ya kutoka Mtwara hadi
Mbamba Bay kimebaki kipande cha kilometa 66 kutoka Mbinga kwenda Mbamba Bay ambacho
hakikuwa na mpango wo wote wa kuwekewa lami kwa sasa. Bahati nzuri, Mwakilishi Mkazi
wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Bibi Tonia Kandiero alitangaza pale Namtumbo
kuwa Benki yake itafadhili ujenzi wa barabara hiyo. Mambo sasa yamekamilika.
Kule
Masasi mkoani Mtwara na Nachingwea mkoani Lindi tulizindua kukamilika kwa mradi mkubwa
wa maji wa Mbwinji unaomaliza tatizo kubwa la maji kwa miji hiyo kwa miaka mingi ijayo.
Nyumba
za Bei Nafuu
Ndugu Wananchi;
Nikiwa wilayani Mkinga na katika Manispaa
ya Songea nilizindua nyumba za gharama nafuu zilizojengwa na Shirila la Nyumba la
Taifa (NHC). Nyumba hizo za vyumba viwili na vitatu zinauzwa kwa bei ya shilingi milioni
31 hadi 42. Wenzetu wa NHC walinieleza utayari wa kujenga nyumba zaidi endapo watapatiwa
maeneo na Halmashauri za Wilaya na Miji. Walinilalamikia kuwa hawapati ushirikiano
wa kutosha kutoka mamlaka husika. Nilipokuwa Mkinga na Songea niliagiza Halmashauri
hizo na nyinginezo nchini kutenga maeneo kwa ajili ya NHC na Mifuko ya Hifadhi za
Jamii yote ili waweze kujenga nyumba za bei nafuu kwa ajili ya wafanyakazi na wananchi
kwa ujumla.
Hii ni fursa ya aina yake kwa wananchi wa kipato cha chini na
cha kati kuweza kujipatia nyumba kwa urahisi. Halmashauri zisiwe kikwazo wakati ardhi
imejaa tele na kila wakati wanapima viwanja vipya. Jambo lingine zuri waliloniambia
viongozi wa NHC ni kwamba zipo Benki ambazo wanashirikiana nazo kutoa mikopo kwa watu
wanaonunua nyumba zao. Ni matarajio yangu kwamba uongozi wa Halmashauri zote nchini
utaitikia maelekezo yangu na kwamba utatenga maeneo kwa ajili ya mashirika yetu hayo.
Matibabu
kwa Wazee
Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa wilaya ya Kilindi nilifurahishwa
sana na utaratibu wa kuwapatia wazee huduma ya matibabu. Kama mjuavyo Sera ya Afya
inataka wazee na watoto wa chini ya miaka mitano watibiwe bure katika hospitali za
Serikali. Bahati mbaya vitambulisho wanavyopata wazee vimekuwa havithaminiwi ya kutosha.
Kwa sababu hiyo, nafuu wanayostahili kupata imekuwa haipatikani kwa urahisi na wengine
huikosa kabisa.
Katika Wilaya ya Kilindi, Halmashauri ya wilaya imeamua kuwakatia
wazee hao Bima ya Afya inayotolewa na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na hivyo kuondoa
kabisa migogoro inayohusiana na vitambulisho vya wazee vilivyokuwepo kabla. Kwa kuzingatia
malalamiko ya mara kwa mara ninayoyapata kutoka kwa wazee kuhusu matibabu, nashauri
Halmashauri zote nchini ziige mfano wa Wilaya ya Kilindi. Kama Kilindi wameweza kwa
nini wengine washindwe.
Ndugu Wananchi;
Katika mikoa hii miwili nilipokea
taarifa za kutia moyo kuhusu juhudi za wananchi na Serikali katika kupanua fursa za
elimu. Vijana wengi wenye umri wa kujiunga na shule za msingi wanafanya hivyo na wale
wote wanaofaulu mtihani wa darasa la saba wanapata fursa ya kwenda sekondari. Hatuna
tena tatizo la fursa. Pamoja na mafanikio hayo mazuri, taarifa za wanafunzi wengi
kushindwa kumaliza elimu ya msingi na sekondari, zimenishtua na kunisikitisha sana.
Katika Mkoa wa Tanga kwa mfano, kati ya wanafunzi 50,921 walioanza darasa la kwanza
mwaka 2007 , ni wanafunzi 41,017 tu ndiyo waliofanya mtihani mwaka 2013. Hivyo basi,
wanafunzi 9,904 ambao ni sawa na asilimia 19.4 hawakumaliza elimu ya msingi. Kwa upande
wa sekondari, katika mkoa wa Ruvuma, kwa mfano, kati ya wanafunzi 18,892 walioanza
kidato cha kwanza mwaka 2010 ni wanafunzi 9,968 sawa na asilimia 52.76 ndiyo waliofanya
mtihani wa kidato cha nne.
Hivyo basi, wanafunzi 8,924 sawa na asilimia 47.2
hawakumaliza elimu ya sekondari. Taarifa za namna hii nilizipata pia katika ziara
zangu ya Mikoa ya Kagera, Geita na Simiyu. Nina kila sababu ya kuamini kuwa hali ni
hiyo hiyo kwa Mikoa mingine mingi nchini. Kwa kweli kiwango hiki cha wanafunzi wanaoshindwa
kumaliza elimu ya msingi na sekondari ni kikubwa mno. Kinanisikitisha sana, hakikubaliki
na hakiwezi kuachwa kiendelee.
Ndugu Wananchi;
Kwa maoni yangu wazazi,
walimu na viongozi wanao wajibu maalumu wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanahudhuria
masomo shuleni tangu wanapoanza mpaka wanapomaliza masomo yao. Huu ni wajibu wa lazima
na siyo hiari. Ni wajibu wa kisheria. Kwa hiyo, nimeagiza kwamba, wazazi, walimu,
Maafisa Elimu wa Wilaya wa Msingi na Sekondari na Kamati husika katika Halmashauri
zote nchini ziwajibike ipasavyo kuhakikisha kuwa utoro mashuleni unakomeshwa.
Ajenda
ya mahudhurio shuleni iwe ni ya kudumu katika vikao vyote vya Halmashauri. Kuanzia
sasa Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule ni lazima watoe taarifa za mahudhurio ya wanafunzi
kwa Maafisa Elimu wa Wilaya kila miezi mitatu. Maafisa Elimu wa Wilaya nao watalazimika
kutoa taarifa kwenye vikao vya Halmashauri mwezi mmoja baada ya kupokea taarifa hizo.
Halmashauri hazina budi kuchukua hatua stahiki za kijamii na kisheria kuhakikisha
kuwa watoro wanarudi shuleni. Wazazi wa watoto hao au mtu ye yote atakayebainika kuhusika
na utoro huo abanwe ipasavyo.
Sheria ya Elimu ya 1978 ipo, itumieni kwa ukamilifu
kulitatua tatizo hili. Haipendezi kusubiri mpaka miaka saba kwa wanafunzi wa shule
ya msingi au miaka minne kwa wanafunzi wa sekondari ipite ndipo taarifa za utoro kwa
wanafunzi zitolewe au zijulikane. Lazima ufuatiliaji wa mahudhurio uwe wa mara kwa
mara ili hatua za kuzuia ziweze kuchukuliwa mapema. Ninawataka viongozi wa TAMISEMI,
Mikoa na Wilaya kuchukua hatua stahiki kudhibiti tatizo hili la utoro na watoto wengi
kutokumaliza masomo. Litarudisha nyuma maendeleo ya taifa.
Umeme Vijijini
Ndugu
Wananchi;
Nilipokuwa mkoani Ruvuma nimezindua ujenzi wa miradi mingi ya umeme
vijijini. Kwa mujibu wa miradi hiyo vijiji 309 vitapatiwa umeme kati ya vijiji 509
vya Mkoa huo vinavyohitaji umeme. Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati
kwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospiter Muhongo na viongozi wenzake, viongozi
na wafanyakazi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) pamoja na TANESCO kwa kazi kubwa
na nzuri waifanyayo ya kufikisha umeme vijijini. Kwa kweli ni mara ya kwanza katika
historia ya nchi yetu suala la umeme vijijini kupewa msukumo mkubwa kiasi hiki, kwani
kinachofanyika Ruvuma kipo nchi nzima. Nawaomba wananchi wanaofikishiwa umeme wautumie.
Hata gharama za kuunganisha umeme zimepunguzwa makusudi, ili watu wengi waweze kumudu
kuingiza umeme majumbani na kwenye shughuli za kichumi na huduma. Mchakato wa Katiba
Mpya
Ndugu Wananchi;
Kama tujuavyo, Bunge Maalum la Katiba lililoahirishwa
tarehe 25 Aprili, 2014 kupisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza
la Wawakilishi kushughulikia bajeti za Serikali husika, litakutana tena tarehe 5 Agosti,
2014 kuendelea na kazi yake ya kutunga Katiba Mpya. Kwa vile Bunge Maalumu la Katiba
halikuweza kumaliza kazi yake ndani ya siku 70 zilizotengwa kwa mujibu wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, nimeliongezea Bunge hilo siku 60 kwa ajili ya kukamilisha kazi
yake. Nimefanya hivyo kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na Sheria hiyo hiyo.
Hatua
Iliyofikiwa Kabla ya Kuahirishwa kwa Bunge
Ndugu Wananchi;
Itakumbukwa
pia kuwa, tarehe 16 Aprili, 2014, baadhi ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba hasa
kutoka vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi walisusia mjadala uliokuwa unaendelea
Bungeni na kutoka nje. Wakati wanatoka Bungeni, kazi kubwa ilikuwa imefanyika. Tayari
Kamati zote 12 za Bunge hilo zilikuwa zimekamilisha kujadili Sura ya Kwanza na ya
Sita za Rasimu ya Tume. Sura hizo zinazungumzia utambulisho wa nchi na muundo wa muungano.
Kamati zote zilipiga kura ya kupitisha uamuzi wao kuhusu sura hizo mbili. Kamati kadhaa
ziliweza kupata theluthi mbili ya kura kwa Wajumbe wa pande zote mbili za Muungano,
jambo lililoonyesha dalili njema kwamba Katiba mpya inaweza kupatikana.
Baada
ya hapo, taarifa ya kila Kamati iliwasilishwa kwenye Bunge zima. Kwa mujibu wa Kanuni
za Bunge Maalumu la Katiba, maoni ya wachache nayo yaliwasilishwa. Kazi iliyokuwa
inafuatia, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge ni kwa Kamati ya Uandishi kukamilisha taarifa
yake na kuiwasilisha kwenye Bunge zima kwa ajili ya kujadiliwa. Baada ya Wajumbe kujadili
taarifa hiyo itafuatia kupiga kura ili kuamua kuhusu Sura hizo mbili. Kama yalivyo
masharti ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, uamuzi utafanywa kwa theluthi mbili ya
kura za kila upande wa Muungano wetu.
Sababu za Baadhi ya Wajumbe Kususia
Bunge Maalumu la Katiba
Ndugu Wananchi;
Sote tumewasikia Wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba waliosusia vikao vya Bunge hilo wakielezea sababu zilizowafanya
watoke Bungeni. Walitoa matamko kwenye vyombo vya habari na pia katika mikutano ya
hadhara waliyoiitisha na kuhutubia sehemu mbalimbali nchini. Sababu walizotoa zimekuwa
zikiongezeka na kubadilika kadri siku zinavyosonga mbele na upepo wa kisiasa unavyokwenda. Hivi
sasa wanazungumzia mambo mawili. Kwanza, kwamba Bunge Maalumu halina mamlaka ya kuifanyia
mabadiliko yo yote Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kwa maoni yao, kazi ya Bunge Maalumu la Katiba ni kujadili na kupitisha tu Rasimu
ya Katiba ya Tume na siyo kubadili cho chote. Pili, wametoa sharti la wao kurudi Bungeni
ni kuhakikishiwa kwamba, kitakachojadiliwa Bungeni ni Rasimu ya Tume. Bila ya sharti
hilo kukubaliwa, wamesisitiza kutorudi Bungeni.
Mamlaka ya Bunge Maalum la
Katiba
Ndugu Wananchi;
Mimi nimehusika katika kubuni wazo la kuwa na
mchakato wa kuandika Katiba Mpya, na katika maandalizi ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, ya kuongoza na kuendesha mchakato huo. Kwa kweli sikumbuki wakati wo wote
katika vikao vya Baraza la Mawaziri kujadili Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba tulipozungumzia Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa haiwezi kufanyiwa
marekebisho na Bunge Maalumu la Katiba.
Mimi siyo Mwanasheria na hivyo nakiri
kwamba naweza kuwa na upungufu katika kuelewa maana ya baadhi ya maneno ya kisheria.
Hata hivyo, sikumbuki kuwepo kwa kifungu cho chote katika Sheria kinachosema kuwa
Bunge Maalumu la Katiba halina mamlaka hayo. Tangu tulipoyasikia maneno hayo yakisemwa
nimeuliza nithibitishiwe ukweli wa madai hayo bado sijaambiwa vinginevyo. Kama ukweli
huo upo naomba anisaidie. Badala yake naambiwa kuwa maneno yaliyotumika katika Sheria
haiakisi dhana inayotolewa kuwa kazi ya Bunge Maalum la Katiba ni kubariki Rasimu
na siyo kufanya vinginevyo. Nimeambiwa kuwa sheria inasemaTume itaanda Rasimu ya Katiba
na Bunge Maalum la Katiba litatunga Katiba iliyopendekezwa.
Ndugu Wananchi;
Tarehe
30 Desemba, 2010, nilipozungumzia dhamira yangu ya kuanzisha mchakato wa kuandika
Katiba Mpya nilieleza wazi nia ya kuwepo kwa uwakilishi mpana wa Watanzania katika
mchakato huo. Ndiyo maana katika Sheria tukaweka ngazi nne katika mchakato wa kutunga
Katiba. Ngazi ya kwanza ikiwa ya wananchi kutoa maoni yao juu ya kila wanachotaka
kijumuishwe katika Katiba ya nchi yao. Ngazi ya pili, ni ya wananchi kupitia wawakilishi
wao katika Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na Mabaraza ya Kitaasisi kutoa maoni yao kuhusu
Rasimu ya kwanza ya Katiba iliyotayarishwa na Tume.
Ngazi ya tatu inajumuisha
wawakilishi wa wananchi waliopo kwenye Mabaraza ya Kutunga Sheria ya Sehemu zetu mbili
za Muungano, yaani Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi, wakichanganyika
na Wawakilishi wa makundi mbalimbali ya jamii ya Watanzania kutoka pande zote mbili
za Muungano. Hawa ndio wanaounda Bunge Maalumu la Katiba, lenye jukumu la kutunga
Katiba inayopendekezwa.
Mamlaka ya kutunga Katiba kwa mila na desturi za Mabaraza
ya Kutunga Sheria ni uwezo wa kurekebisha, kubadili, kufuta na hata kuongeza kilichopendekezwa.
Ingekuwa kilichokusudiwa ni kubariki tu lisingetumiwa neno la kutunga Katiba. Hali
kadhalika, lisingewepo sharti la kupiga kura na msisitizo wa kupata theluthi mbili
kwa kila upande wa Muungano. Aidha, kama ingekuwa jukumu la Bunge Maalumu ni kubariki
tu Rasimu lisingepewa siku 70 za kazi na Rais kupewa mamlaka ya kuongeza siku zaidi
kadri aonavyo yeye inafaa.
Ngazi ya nne na ya mwisho, tuliweka kura ya maoni
ya wananchi kukubali au kukataa Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba.
Kama ingekuwa Rasimu ya Tume haiwezi kubadilishwa hata nukta kwa nini basi tuweke
kura ya maoni ya kuwahusisha wananchi wote?
Ndugu Wananchi;
Tulizibuni
ngazi hizi nne kwa dhana kwamba kile ambacho hakikuonekana au hakikuwekwa sawa katika
ngazi moja kitaonekana na kurekebishwa katika ngazi inayofuata katika ngazi zile tatu
za mwanzo. Na, iwapo Katiba iliyotungwa haitawaridhisha wananchi wanayo haki ya kuikataa.
Kwa kufanya hivyo, wananchi ndiyo waliopewa turufu ya mwisho.
Ndugu wananchi;
Kwa
kweli, napata shida kuelewa mkanganyiko unatoka wapi na hasa wale wanaoongoza kuhoji
mamlaka ya Bunge Maalumu kuwa ni wale wale waliotunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
tena hatua kwa hatua. Nashangazwa zaidi ninapoona wale wale waliotunga Kanuni za Bunge
Maalumu ndiyo wanaoongoza kuhoji uhalali wa kile walichokitunga.
Kanuni za
Bunge Maalumu la Katiba, Ibara ya 33 (8) inasema: Nanukuu: “Wakati wa mjadala, Mjumbe
yoyote anaweza kutoa mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko yaliyomo
katika Sura za Rasimu ya Katiba zinazojadiliwa kwa utaratibu ufuatao: (a) Ikiwa ni
marekebisho, maboresho au mabadiliko yanayobadilisha jambo la msingi, au yanayobadilisha
maudhui ya Ibara, mapendekezo ya marekebisho yatapelekwa kwa maandishi kwa Katibu
siku moja kabla ya mjadala wa Ibara husika. (b) Ikiwa ni marekebisho madogo, ambayo
hayabadili msingi au maana, mapendekezo ya marekebisho yatawasilishwa na mjumbe wakati
wa mjadala baada ya kupata ruhusa ya Mwenyekiti”. Mwisho wa kunukuu.
Kanuni
hii ilipotungwa, Wajumbe wote wa Bunge Maalumu pamoja na wale ambao baadae walisusia
vikao vya Bunge walikuwepo Bungeni na walishiriki kuipitisha. Tena basi, baadhi yao
walikuwa Wajumbe wa Kamati ya Kanuni iliyopendekeza Kanuni hizo. Unapowaona watu wale
wale sasa wanakuwa vinara wa kuhoji mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba, unajiuliza
maswali mengi kuhusu watu hao bila ya kupata majibu yaliyo sahihi na kutosheleza akili
na ufahamu wetu. Ndugu Wananchi;
Unaposoma Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
na Kanuni za Bunge Maalumu, hii ni dhahiri kwamba wote walikuwa na uelewa wa pamoja
kuhusu mamlaka ya Bunge Maalumu ya kujadili Rasimu iliyoandaliwa na Tume na kutunga
Katiba inayopendekezwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura.
Kinachojadiliwa
Bungeni ni Rasimu ya Tume
Ndugu Wananchi;
Yapo madai yanayotolewa na
kuenezwa na Wajumbe waliosusia Bunge Maalumu la Katiba kwamba kinachojadiliwa Bungeni
siyo Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ndiyo maana basi wanaweka sharti la kujadiliwa
Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba ndipo warudi Bungeni. Madai haya nayo yananipa taabu
kuyaelewa. Ndugu zetu hawa walishiriki siku zote 19 za Kamati 12 zilipokutana kujadili
Sura ya Kwanza na ya Sita za Rasimu ya Tume.
Halikadhalika. walikuwepo na
kushiriki kwa ukamilifu wakati taarifa za Kamati, tangu ya Kwanza mpaka ya 12, zilipowasilishwa
kwenye Bunge zima. Aidha, na wao walishiriki kutoa maoni ya wachache kwa dakika 20
na kutoa ufafanuzi kwa muda wa dakika 30 kwa kila Kamati. Haya maneno ya sasa kwamba
kinachojadiliwa Bungeni siyo Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba bali nyingine kabisa ambayo
wanadai eti ni ya CCM yanatoka wapi.
Mimi nadhani kuwa huenda katika Kamati
kumefanyika marekebisho kwenye Rasimu ambayo hayakuwapendeza. Kama hivyo ndivyo, wawe
wakweli kuhusu jambo hilo kuliko kusema mambo yasiyowakilisha ukweli halisi wa Rasimu
inayojadiliwa. Matokeo yake ni kuwafanya wafuasi wao na wapenzi wao na hata watu wengine
waamini kuwa kinachojadiliwa siyo Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba bali nyingine tena
ni ya CCM. Jambo hilo si kweli na wenyewe wanajua kwamba si kweli ila sijui kwa nini
wameamua kupotosha ukweli.
Ndugu Wananchi;
Kinachonishangaza, zaidi
ni kwamba, kama hawakuridhishwa na yaliyofanyika, kwa nini wasingetumia mifumo waliyojitengenezea
wenyewe kwenye Kanuni kumaliza tofauti zao? Kanuni zinaelekeza kuwa mambo wasiyoridhika
nayo yajadiliwe kwenye Kamati ya Mashauriano na Maridhiano. Ukiacha mifumo ya maridhiano
ndani ya Bunge ukaenda nje kwa wananchi au vyombo vya habari na mitandao si jawabu
la tatizo.
Ndugu Wananchi;
Ndiyo maana nashawishika kuunga mkono wale
wote wanaowasihi Wajumbe wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na wengine warejee Bungeni.
Watumie mifumo maalum ya Bunge iliyowekwa na Kanuni kutafuta maridhiano. Hali kadhalika,
wasichoke kuwa na mawasiliano na vyama vingine vya siasa na hasa CCM kutafuta maelewano.
Mimi niko tayari kusaidia pale watakapoona inafaa kufanya hivyo kama ambavyo nimekuwa
nikifanya ziku za nyuma. Nililolisema mwanzoni kabisa mwa mchakato na nalirudia
tena leo kwamba, ili tuweze kufanikiwa kupata Katiba Mpya ambayo sote tunaitaka, maelewano
baina ya wadau wakuu wa kisiasa ni jambo lisilokuwa na badala yake. Vinginevyo kupata
theluthi mbili kwa pande zote mbili za Muungano haitawezekana. Ndiyo maana nampongeza
sana Msajili wa Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Jaji Francis Mutungi, kwa uamuzi wa kuvikutanisha
vyama vinne vikuu vya siasa kujadili namna ya kuondoa mtihani uliopo sasa katika mchakato
wa Katiba.
Ombi langu kwa viongozi wa vyama hivyo ni kuitumia vyema fursa ya
majadiliano kuukwamua mchakato kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake. Hali kadhalika
nampongeza sana Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Mheshimiwa Samwel Sitta, kwa
kuitisha kikao cha Kamati ya Mashauriano na Maridhiano. Bahati mbaya ni kwamba Wajumbe
wa vyama vilivyosusia Bunge Maalumu hawakushiriki. Ni matumaini yangu kuwa Mheshimiwa
Sitta hatokata tamaa kuendeleza juhudi za mashauriano na kwamba katika vikao vijavyo
na wenzetu hawa watashiriki.
Ndugu Wananchi;
Hivi karibuni kumekuwepo
pia madai yanayoelekeza lawama kwangu. Kwanza nalaumiwa eti kuwa mambo yalikuwa yanaenda
vizuri mpaka pale nilipotoa hotuba ya ufunguzi wa Bunge Maalumu ndipo yalipoharibika.
Pili nalaumiwa kwamba nawezaje kuikana Rasimu ya Katiba ambayo na mimi ni mmoja wa
watu waliotia sahihi katika Rasimu hiyo.
Niruhusuni nianze na hili la pili.
Nadhani ndugu zetu wanaotoa madai haya yameitafsiri isivyo sahihi yangu katika Gazeti
la Serikali lililotangaza rasmi Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume ya Mabadiliko
ya Katiba. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba baada ya Tume kumaliza kazi
yake ya kuandika Rasimu ya Katiba, Rais wa Jamhuri ya Muungano amepewa kazi tatu kufanya.
Kwanza, kupokea Rasimu hiyo na Taarifa ya Tume kutoka kwa Mwenyekiti jambo ambalo
lilifanywa tarehe 30 Desemba, 2013. Pili, amepewa kazi ya kuitangaza rasmi Rasimu
ya Katiba na Taarifa ya Tume kwa watu wote kuiona na kuisoma ndani ya siku 30. Alipewa
sharti la kuitangaza katika Gazeti la Serikali na vyombo vingine vya habari.Hili nalo
lilifanywa hivyo tarehe 22 Januari, 2014.
Ndugu Wananchi;
Katika kutangaza
katika Gazeti la Serikali sharti linamtaka anayetangaza ajitambulishe kuwa yeye ni
nani na atie sahihi yake. Kwa kufanya hivyo, hakumfanyi yeye kuwa naye ni mhusika
na maudhui ya kila kinachopendekezwa na Tume. Sahihi zilizomo ndani ya Rasimu na Taarifa
ya Tume ni za Wajumbe wa Tume, kamwe sahihi ya Rais haimo hivyo hawezi kulaumiwa kuwa
anaikana sahihi yake. Yeye ametimiza wajibu wake wa kutangaza, akaiweka hadharini
kwa umma wa Watanzania kuiona na kusoma Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume vilivyotayarishwa
na kutiwa sahihi na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kazi ya tatu ni kuitisha
Bunge Maalumu ambayo nayo imekamilika tangu tarehe 18 Februari, 2014.
Ndugu
Wananchi,
Jambo lingine linalofanana na hilo ni yale madai kwamba nilikuwa
napata taarifa ya maendeleo ya mchakato ndani ya Tume mara kwa mara, iweje leo nitoe
maoni tofauti kama niliyoyatoa katika hotuba yangu kwenye Bunge Maalumu. Ni kweli
kabisa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba,
Makamu wake, Mheshimiwa Jaji Agustino Ramadhani na Mheshimiwa Dkt. Salim Ahmed Salim
wamekutana na mimi kwa nyakati mbalimbali kuzungumzia mwenendo wa mchakato. Lakini,
hayakuwa mazungumzo ya kina kuhusu nini kiwe vipi katika maudhui na mapendekezo ya
Tume. Ukweli ni kwamba Rasimu zote mbili nilizipata mara ya kwanza nilipokabidhiwa
rasmi, tena kwa uwazi. Napenda watu wasijenge dhana kuwa nilipewa Rasimu na kuisoma
kabla ya kukamilika na hivyo nilitoa maoni yangu. Tume hii ilikuwa huru na niliiacha
iwe hivyo. Sikuiingilia kwa namna yo yote ile kupenyeza mambo ninayotaka yawemo. Kuthibitisha
dhamira yangu ya kutaka Tume iwe huru katika kufanya kazi zao hata pale waliponitaka
nitoe maoni niliwaomba tusifanye hivyo ili nisiwakwaze katika kufanya kazi zao, wakapata
taabu ya kuwianisha wanayofikiria na mawazo yangu.
Ndugu Wananchi;
Kuhusu
madai kwamba mambo yalikuwa yanakwenda vizuri na kwamba hotuba yangu iliyavuruga,
napenda kusema wazi kuwa lawama hizo hazina ukweli wo wote. Ni madai yasiyokuwa na
msingi. Kwani mimi hasa siku ile nilifanya lipi la ajabu. Ukweli ni kwamba nilisema
yale yale ambayo Tume yenyewe imeyasema katika Rasimu ya Katiba na Taarifa za Tume.
Niliyoyasema kuhusu malalamiko ya watu wa pande zetu za Muungano na uzuri na changamoto
za miundo ya Serikali mbili na Serikali tatu ni yale yale yaliyomo kwenye taarifa
za Tume. Nimetumia takwimu zile zile za Tume. Pengine kilichoonekana kuwa kibaya ni
jinsi nilivyozifasiri taarifa hizo na mapendekezo ya Tume.
Jambo lingine ambalo
nimelifanya ni kutoa maoni yangu kuhusu baadhi ya vipengele vya Rasimu hususan uandishi
na dhana mbalimbali zilizokuwamo. Silioni kosa langu kwa kufanya hivyo, kwani Rasimu
imetolewa hadharani kwa watu kuijadili. Na mimi kama raia ninayo haki ya kufanya hivyo
kama wafanyavyo wengine. Kwa nini nilaumiwe kwa kutumia haki yangu hiyo.
Lakini,
pia mimi ndiye Rais wa nchi yetu, ninayo dhamana ya uongozi na ulezi wa taifa letu.
Itakuwaje kwa jambo kubwa la hatma ya nchi yetu nilinyamazie kimya. Watanzania wangeshangaa
na wangekuwa na haki ya kuhoji Rais wao ana maoni gani. Bahati nzuri nilitoa maoni
yangu mahali penyewe hasa, na kwa uwazi, kwenye Bunge Maalumu la Katiba. Hata hivyo,
ni muhimu kusisitiza kuwa namna nilvyotoa maoni yangu sikuwa natoa maagizo wala kushurutisha,
ndiyo maana kila wakati niliwakumbusha Wajumbe kuwa mamlaka ya uamuzi ni yao. Yangu
yalikuwa maoni tu wanahiyari ya kuyakubali au kuyakataa. Niliwataka Wajumbe wasome
na kuielewa vyema Rasimu. Nilisema wasome sura kwa sura, mstari kwa mstari na neno
kwa neno. Niliwaomba wajiridhishe kuhusu uandishi na dhana mbalimbali. Nilitoa mifano
ya mambo yahusuyo uandishi ambayo ni vyema wayatazame. Pia nilitoa mifano ya dhana
ambazo niliwasihi wajiridhishe juu ya kufaa kwake kuwepo. Kuhusu muundo wa Serikali
tatu, nilieleza wazi kuwa sina tatizo nao kama ndiyo matakwa ya Watanzania. Lakini,
nilieleza hofu yangu kuhusu mapendekezo ya Tume na kuwataka Wajumbe wafanye kazi ya
ziada kuondosha udhaifu iwapo wataukubali muundo unaopendekezwa.
Nilieleza
nia yangu ya kutaka tuwe na Serikali ya Muungano yenye ukuu unaoonekana, yenye nguvu
ya kuweza kusimama yenyewe, inayoweza kuwa tegemeo kwa nchi Washirika, Serikali isiyokuwa
tegemezi wala egemezi kwa nchi washirika na ambayo inavyo vyanzo vya uhakika vya mapato.
Hivi kwa kutoa ushauri huo kwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba inageuka kuwa nongwa.
Kwa kweli sielewi lawama ni ya nini?.
Naamini sistahili lawama bali pongezi
kwa kuwa muwazi na kutoa ushauri wa msingi ambao utasaidia nchi kupata Katiba nzuri
inayojali maslahi ya watu wa nchi yetu na ya nchi zetu mbili zilizoungana miaka 50
iliyopita.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Mwisho, ni maoni yangu
ya dhati kuwa mgogoro uliopo sasa katika mchakato wa Katiba hauna sababu ya kuendelea
kuwepo. Naamini hayo yote ambayo Wajumbe wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi wanayalalamikia
yanaweza kushughulikiwa kwa ukamilifu katika mifumo ya Bunge Maalumu la Katiba iliyotengenezwa
na Wajumbe wote na wao wakiwemo. Nawasihi waitumie. Hali kadhalika, kwa kupitia mazungumzo
wanayofanya na wenzao wa Chama cha Mapinduzi wanaweza kutengeneza nguvu ya pamoja
kutatua changamoto za sasa na zitakazojitokeza baadaye. Kilicho muhimu ni kwa pande
zote kuwa na dhamira ya dhati ya kutoka hapa tulipo sasa. Kama utashi wa kisiasa upo
kwa kila mmoja wetu, hilo ni jambo linalowezekana kabisa. Narudia kuahidi utayari
wangu wa kusaidia kadri inavyowezekana tusonge mbele.