Vyombo vya mawasiliano ya jamii ni nyenzo ya imani na amani!
Jukwaa la Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki Barani Afrika, UCAP, hivi karibuni limehitimisha
mkutano wake uliokuwa unafanyika mjini Bamako, Mali, kwa kuongozwa na kauli mbiu "Vyombo
vya mawasiliano ya jamii ni nyenzo msingi ya amani na majadiliano Barani Afrika".
Mkutano huu ulifunguliwa na Bwana Thierno Amadou Hass Dialo, Waziri wa masuala
ya dini na ibada nchini Mali, aliyewataka waandishi wa habari Wakatoliki kuwa ni vyombo
vya vya imani na wajumbe wa amani. Waandishi wa habari wanapaswa kueneza habari zitakazosaidia
kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa, maendeleo na mawasiliano yanayowajibisha.
Kwa
upande wake, Askofu mkuu Jean Zerbo wa Jimbo kuu la Mali anaona kwamba, ni rahisi
sana kuweza kudhibiti kinzani za kisiasa, lakini kinzani hizi zinapochukua sura ya
udini na ukabila, Jamii inajikuta kwamba, iko hatarini kutumbukia katika maafa makubwa.
Hivyo Askofu mkuu Zerbo amewataka waandishi wa habari kutekeleza dhamana yao nyeti
kwa kuwajibika barabara, kwa kuangalia matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo.
Wajumbe
wa mkutano huu wamekumbushwa kwamba, mawasiliano ya jamii ni nyenzo msingi katika
kushiriki mchakato wa Uinjilishaji Mpya, ili kuwatangazia watu wa nyakati hizi Injili
ya Furaha. Ni changamoto kubwa inayopania kuenzi Injili ya Uhai, uhuru wa kuabudu,
haki na amani, maendeleo, mshikamano pamoja na kuwarithisha vijana wa kizazi kipya
tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu.
Ili kurithisha mambo haya kuna haja
kwanza kwa waandishi wenyewe wa habari kuwa ni mashahidi wa imani ili kuweza kuwashirikisha
wengine ule utajiri unaobubujika kutoka katika undani wa mioyo yao! Waandishi wa habari
wawe kweli ni vyombo vya kutangaza imani na huduma ya amani. Mkutano huu umehudhuriwa
na wajumbe kutoka katika nchi kumi na nne za Kiafrika.