2014-08-01 10:33:20

Simameni kidete kulinda, kutetea na kuendeleza tunu msingi za maisha ya ndoa na Familia ya Kikristo!


Familia inajengeka katika mahusiano thabiti kati ya mwanaume na mwanamke wanaopania kushiriki katika mpango wa Mungu, kujenga Jamii, kuwalinda na kuwatunza watoto katika misingi ya amani na utulivu. Haya ni kati ya mambo msingi yaliyoibuliwa katika maadhimisho ya Kongamano la Familia Kitaifa lililofanyika mjini Kinshasa, DRC kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 25 Januari 2014.

Kongamano hili lilikuwa limeandaliwa na Jumuiya ya Wakristo kwa kushirikiana na Kitivo cha Sheria na Sayansi Jamii cha Chuo Kikuu cha Kikatoliki nchini DRC. Nyaraka za kongamano hili ambao ni mchango kutoka kwa wadau mbali mbali wanaotaka kujenga na kudumisha misingi ya familia bora inayojikita katika imani ya Kikristo, kanuni maadili na utu wema zimezinduliwa hivi karibuni.

Professa Jules Dobo katika ufafanuzi wake amekazia uelewa makini wa Familia kadiri ya mafundisho ya Kanisa Katoliki na kwamba, wanasiasa na watunga sera wanapaswa kuunga mkono juhudu za kudumisha familia bora.

Kutokana na kisingizio cha utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, familia zinajikuta zikikabiliana na changamoto nyingi ambazo zinataka kuyumbisha kanuni maadili na utu wema, kwa kisingizio cha usawa wa kijinsia; ndoa za watu wa jinsia moja; mazingira ambayo yanawanyima watoto kulelewa na kukulia katika maisha ya kifamilia kadiri ya mafundisho ya Kanisa Katoliki.

Kuteleleka kwa misingi bora ya familia, upendo na mshikamano wa dhati, magonjwa, vita na kinzani za kijamii, zimepelekea watoto wengi kujikuta wakiishi katika mazingira hatarishi. Takwimu zinaonesha kwamba kuna watoto millioni mia moja wanaoishi katika umaskini mkubwa na kwamba, kati yao kuna watoto laki mbili na themanini wanaoishi katika mazingira hatarishi mjini Kinshasa.

DRC kuanzia mwaka 2009 hadi wakati huu imekuwa ni mlengwa mkubwa wa biashara haramu ya binadamu. Washiriki wa Kongamano la Familia Kitaifa huko DRC linawataka wadau mbali mbali kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi bora ya maisha ya ndoa na familia! Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema wawe ni vyombo vya kutangaza Injili ya Uhai kwa kupinga utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba na kifo laini.

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wawe makini na madhara yanayoweza kusababishwa na vyombo vya mawasiliano ya jamii katika maisha ya ndoa na familia.







All the contents on this site are copyrighted ©.