2014-08-01 11:10:38

Papa atembelea makao makuu ya Wayesuit na kupata nao chakula cha mchana


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, mwanzilishi wa Shirika la Wayesuit, iliyoadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 31 Julai 2014, ametembelea Makao makuu ya Wayesuit yaliyoko mjini Roma pamoja na kupata chakula cha mchana na Wayesuit wanaoishi hapo.

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha nia hii kwa mkuu wa Shirika ili kuweza kuwa pamoja na ndugu zake katika imani, katika hali ya faragha pasi na makuu.

Taarifa inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya chakula cha mchana, ameendelea kuzungumza na Wayesuit kwenye chumba cha mapumziko, huku wakijipatia kahawa. Wakati wa chakula cha mchana wameshiriki pia ndugu zake Padre Paolo Dall'Oglio, Myesuit, aliyetekwa nyara mwaka mmoja uliopita huko Syria hadi sasa hajulikani mahali alipo.

Baba Mtakatifu amebadilishana maneno ya faraja na ndugu hawa kwa kuthamini na kutambua mchango uliotolewa na Padre Paolo Dall'Oglio katika maisha na utume wake. Katika chakula hiki, walikuwepo pia Wajesuit kutoka Ulaya wanaoendelea na majiundo yao kwa kushiriki katika semina maalum.







All the contents on this site are copyrighted ©.