2014-08-01 15:31:52

Hatoki mtu hapa hadi kimeeleweka!


Kwenye riwaya ya Kusadikika ya Shaaban Robert kuna Mfalme Jeta. Mfalme huyu alikutwa na mjumbe wa Kusadikika akiwa amekaa eneo moja ambapo, bahari, maziwa, mito mikubwa iliyokuwa inakokozoa kila kitu – mawe, magogo, majengo, udongo, n.k. – vyote vinatiririkia kinywani mwake na kuishia tumboni.

Lakini Jeta alisikika akilia: “Njaa! Njaa! Kiu! Kiu!”. Kinachonishangaza mimi ni kwamba endapo mfalme na kiongozi huyu, licha ya kuchepusha mito na kila raslimali itumike kwa faida yake bado hatosheki, anazidi kulalamika na kulia “mwenzenu mkisikia nimekufa, basi mjue kilichoniua ni njaa na kiu.” Je! kwa mlalahoi aliyekaushiwa maji na chakula atabaki na hali gani? Hii ndiyo hali halisi ya ulimwengu wa leo.

Katika Injili ya leo Yesu anakumbana na aina hiyo ya watu kama akina Jeta. Tumsikilize Yesu anavyotufundisha jinsi ya kufanya muujiza wa kupata lishe ya kushibisha na kuridhisha wote bila kulalamika kwa wongo mtupu kama wa mfalme Jeta.

Katika kitendo chake cha kugawa chakula (mikate na samaki), Yesu, anataka kulitatua tatizo la njaa ulimwenguni. Tunapozungumza juu ya njaa, siyo tu chakula kinachoshibisha matumbo tu, bali hata ile njaa ya mahitaji yote ya binadamu katika maisha. Mpango wa Mungu kwa binadamu anataka wasiteseke katika kuupata uhondo wa ulimwengu wa sasa na ujao. Kwa hiyo ameweka kila kitu hapa duniani ili watoto wake waweze kujitosheleza katika mahitaji yao na ulimwenguni ameweka tayari maji, ameweka chakula, madini tele, mafuta, mimea nk.

Kichwa cha Injili ya leo kinasema kuwa “Yesu anawalisha watu zaidi ya elfu tano” aidha, “Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili..., akawapa wanafunzi, na wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba wakaokota masazo ya vipande vya mikate…”

Ujumbe huu ni wa kiteolojia. Muujiza huu ni mwaliko kwetu kutoa jibu juu ya njaa ya maisha ambayo watoto wa Mungu wanayo katika ulimwengu huu. Muujiza unatufundisha sisi tuweze kufanya muujiza aina hiyo wa kuhakikisha kunakuwa chakula cha kutosha hata kubaki cha kushibisha njaa ya watu wa ulimwengu. Nja hiyo yaweza kuwa ya kawaida, ya kibaolojia, ya kibinadamu (utu) yaani njaa ya haki, njaa ya upendo, ya amani, njaa ya mahaba, njaa ya afya nzuri nk.

Ili kulielewa vyema lengo la muujiza huu wa Yesu, tuifuatilie lugha ya kibiblia inayotumika katika mfano huu yaani picha mbalimbali na maelezo mengine yanayoonekana kujipinga. Mathalani imeandikwa, “Naye Yesu aliposikia hayo aliondoka huko katika chombo, akaenda mahali pasipo watu, faraghani.” Maana yake alisafiri baharini katika mashua. Halafu “makutano waliposikia walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao” Hapa haieleweki watu walisikia toka wapi kwamba Yesu amewasili huko. Halafu haiwezekani wao wasafiri ufuoni na wafaulu kuwasili hapo mapema zaidi ya Yesu aliyesafiri kwa mashua waweze kumlaki.

Yasemwa pia kwamba pahala hapo palikuwa nyika au jangwa: “Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pia;” maana yake pahala pale hapakuwa na uoto wowote ule wa majani. Kumbe tunasikia kuwa baada ya kugeuza mikate Yesu “akawaagiza makutano waketi katika majani:”.

Hayo majani yalitoka wapi endapo tumeambiwa kuwa pahala hapo ni nyika au jangwa. Kisha tena idadi ya watu waliokula ni tata “wanaume elfu tano bila kuhesabu wanawake na watoto.” Utata mwingine ni jinsi ya kuongezeka kwa mikate kulivyofanyika, haieleweki kama mikate ilitoka mikono ya Yesu mwenyewe au toka mikono ya wanafunzi wake. “Wakamwambia, “Hatuna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili. Yesu akasema: Nileteeni hapa.”

Hatimaye, unaona ingawa muujiza huu unaelezwa karibu mara sita katika injili, lakini maelezo ya kila mmoja hayafanani. Tofauti hizi zote ndizo zinazotupatia mwanya wa kuelewa vizuri zaidi maana ya fasuli hii. Mwinjili anataka kutuganjulia, ujumbe wenye thamani kubwa katika maisha yetu, nayo ni kutufundisha jinsi ya kufanya muujiza wa raslimali tulizo nazo katika maisha.

“Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia … akawaponya wagonjwa wao.” Mungu mwenye mapendo, mwenye huruma hapendi viumbe vyake viteseke. Hivi mkutano huu mkuu unawakilisha taifa zima, ulimwengu wote, watu wanaosubiri kutoshelezwa mahitaji yao kutoka kwa Bwana anayeanza ulimwengu mpya jinsi Mungu aliyotaka.

Nyikani (pembeni mwa ziwa Galilaya hakuna jangwa), bali kibilia jangwa hapa lamaanisha mang’amuzi waliyokuwa nayo Wayahudi jangwani kwa miaka arobaini. Ndiyo ulimwengu na maisha yetu hapa duniani.

Fikra na mawazo ya watu wa kale juu ya upatikanaji wa chakula na mali huwakilishwa na hoja wanazozitoa hapa wanafunzi wa Yesu. Hivi ndivyo tunavyofanya binadamu tukiwa na njaa au tunapokuwa na hitaji. Wanafunzi wake walimwendea, wakasema, “Mahali hapa ni nyika tupu na saa imekwisha pita; uwaage makutano waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula”. Wakimaanisha kwamba, kila mmoja ajitegemee mwenyewe, akajitafutie ridhiki yake. Asiye na hela “kazi kwake!”

Tatizo hapa ni kwamba, inabidi wote waende viijini kununua. Bila kujali kwamba hapo kuna mchanganyiko wa watu: kuna vijana wanaoweza kuwahi haraka, kuna wazee, kuna watoto, kuna waja wazito, kuna wagonjwa wanaoenda polepole au wanaoshindwa kabisa kutembea. Wale watakaowahi wanaweza kujilundikia mikate mingi zaidi.

Mapato ya mantiki hii ni kwamba, ulimwengu hautaweza kamwe kutatua tatizo la njaa katika maisha haya, kwa vile ni ufalme wa mashindano, ufalme wa ubinafsi, ufalme wa kujikusanyia mali huo ndiyo ulimwengu unaotumia mali yake siyo kadiri ya mpango wa upendo wa Mungu bali kadiri ya matakwa na uwezo wa mtu binafsi. Kitendo hicho ndicho kinaamsha njaa kwa mwenye mali na kwa asiye nayo.

Ni dhahiri kwa anayefikiri kwa mtindo huu anakuwa na uhakika kwamba kugawana raslimali hivyo hakuwezi kuwatosheleza wote mali ya ulimwengu huu. Mtu huyo anakuwa kama mfalme Jeta. Hata kama atapata raslimali zote, lakini daima utamsikia analia: “Njaa, njaa, Kiu, kiu”.

Yesu anatoa pendekezo jipya wanafunzi wake anapowaambia: “Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi kula.” Kwa jibu hili unaona jinsi Ufalme wa Mungu ulivyo na mchango juu ya mali ya ulimwengu huu. Kumbe wanafunzi hawa hawatofautiani na watu wa leo wanaotenganisha dini ya kweli na maisha ya kawaida. Wanadiriki hata kuwapumbazisha wengine wakiwaaminisha kuwa hakuna mahusiano kati ya Mungu na mali ya dunia hii.

Hayo ni mawazo finyu ya kutenga Mungu na maisha ya kawaida ya duniani hapa. Angalieni jibu finyu la wanafunzi wa Yesu: “Hatuna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili”. Wanaongea uwongo kwa uhakika, bila kujua kwamba wakijumlisha idadi ya mikate mitano na ya samaki wawili wanapata jumla namba saba, inayomaanisha ukamilifu. Idadi hiyo inataka kututhibitishia kuwa hapa ulimwenguni binadamu anayo raslimali (hazina) iliyokamilika tena ni ya aina tofauti. Aidha raslimali hiyo inatutosheleza sote. Endapo mali hiyo haitutoshelezi sote basi ni kwa sababu imemilikiwa na wachache.

Kwa hiyo maajabu kuonja jinsi mali yanawezesha kumtosheleza kila mmoja, na kuridhisha hitaji la binadam, huo ndiyo muujiza ambao Yesu anataka kutufundisha sisi leo. Muujiza wenyewe unaanza pale Yesu anaposema: “Nileteeni hapa!” kama vile angetuambia sisi “Kama mtanikabidhi mimi raslimali hii iliyo kamili, ambayo ninyi mnasema haitoshi mimi ninaweza kuwaonesha jinsi ya kugawana hadi inawatosheleza wote.”

Hapa Yesu ametuona binadamu kama watoto wadogo waliorushiwa pipi au chokoleti. Watagongana na kuumizana, na watakaofaidi ni wachache wenye nguvu; hadi pale wanapozikabidhi kwa mkubwa anayeweza kuwagawia kwa utaratibu.

Baada ya kukabidhiwa mali hiyo Yesu: “Akawaagiza makutano waketi katika majani.” Hapa unarejeshwa kwenye zaburi ya 23 “Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza kando ya maji ya utulivu huniongoza.” (Zab 23:1-2) kadhalia “Waandaa meza mbele yangu, machoni pa watesi wangu.” (Zab 23: 4b). Hiyo ni picha ya ufalme wa Mungu. Bwana ameandaa dhifa kwa ajili ya watoto wake wote.

Tendo lifuatalo baada ya kuwaketisha watu linatuonesha kuwa sasa muujiza hauna budi kutokea. Kabla ya kuigawa ile mikate “Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili akatazama juu mbinguni”. Hapa anatufundisha tunachotakiwa kukifanya tunapokuwa mbele ya chakula, au tunapogundua raslimali yoyote ile yatubidi kwanza kuinua macho na kutazama mbinguni, yaani tumshukuru Mungu na tutambue kwamba kila kitu huja toka mbinguni.

Tutambue kwamba hakuna mtu yeyote mwenye mamlaka na mali, sisi sote ni waalikwa tu. Bosi na mmiliki mkuu ni Mungu peke yake. “Dunia na kila kilichomo ni mali ya Bwana.” Kumbe binadamu ni wapumbavu, wanapojidanganya kuwa wamegundua raslimali aliyoishatuwekea Mungu ardhini kama vile mafuta, gesi, dhahabu nk. hawatazami tena mbinguni kwa Mungu, badala yake wanaanza kuipangia bajeti.

Mapato yake, wanaumizana, wanatengana, wanaachana ukoo nk. Ukiliona taifa lolote lile linagombania raslimali za ulimwengu huu, ujue taifa hilo limeshapoteza mwelekeo na halina imani kwa Mungu hata kama lingejidai linakereketwa na imani yake. “Mwisho wa watu hao ni uharibifu, Mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao.” (Wafilipi 3:19).

Baada ya kutazama mbinguni ndipo Yesu “akaimega ile mikate” hiyo ni alama ya kugawa au kutoa. Kuonesha kuwa sisi sote ni watoto wake na wapokeaji tu. Kisha “akawapa wanafunzi.” Yaani mwenye uwezo wa kufanya muujiza ni yule tu aliye mwanafunzi halisi wa Yesu. Asiyeelewa na kupokea mantiki hii ya Yesu, hataweza kamwe kufanya muujiza huu. Kisha “wanafunzi wakawapa makutano”.

Kwa vile Mungu alishatayarisha vizuri kabisa chakula (mali, mahitaji) kwa watoto wake ili kiweze kutosheleza na kuridhisha wote. Kwa hiyo yabidi wanafunzi wanaoelewa mantiki ya Mungu wakigawe. Utajiri wa Mungu ni mkubwa sana, uwezo aliokuwa nao kila binadamu hapa duniani ni mkubwa sana, akili yake, mawezo yake, ugunduzi wake na mapaji yake ni makubwa.

Raslimali za dunia hii huweza kufanya maajabu na miujiza tu endapo zitatumika kadiri ya mpango wa Mungu na kadiri ya mapendekezo anayotupatia Bwana Yesu. Ujumbe mzuri namna hii utaupata tu ukiwa mfuasi wa Yesu Kristu. Hitimisho la Injili ya leo ni muhimu pale inaposema “Wakayaokota masazo ya vipande vya mikate,” bila kupoteza ovyo mabaki, kwa sababu kisitupwe hovyo au kusahauliwa kipaji chochote kile cha Mungu, yaani, kumthamini kila mtu na mapaji yake. Kuthamini kila kitu anachotupatia Mungu.

Ujumbe wa leo ni kwamba hata sisi tunao uwezo wa kufanya muujiza tukiwa na imani juu ya mapendekezo ya Yesu kuhusu Ulimwengu mpya. Tuzitolee kwanza kwa Mungu raslimali zetu, mali zetu, naye atatufundisha jinsi ya kuyagawana vyema. Vinginevyo licha ya kukalia raslimali kedekede tutabaki tunalia daima kama Jeta. “Njaa, njaa, Kiu, kiu!”.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.