Baba Mtakatifu Francisko kwa kusoma alama za nyakati na kutambua matatizo na changamoto
zinazoendelea kuzikabili familia nyingi za Kikristo katika maisha na utume wake, ameamua
kuitisha Sinodi Maalum ya Maaskofu ili kuweza kusali, kutafakari na hatimaye, kushirikishana
kuhusu: hali ilivyo, matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha na
utume wa Familia kwenye ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Kanisa linataka
kuwaonjesha tena wanandoa umuhimu na uzuri wa maisha ya ndoa na familia kadiri ya
mpango wa Mungu kwa maisha ya mwanadamu. Mama Kanisa anakumbusha kwamba, daima kuna
uhusiano wa dhati kati ya Sakramenti ya Ndoa na Sakramenti nyingine za Kanisa, hususan
Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Kitubio.
Pale ambapo wanandoa wanavunja
maagano yao ya ndoa na kuamua kuoa au kuolewa tena wanajikuta wakikikabiliana na vizuizi
vya sheria za Kanisa, changamoto kubwa kwa waamini wenyewe na viongozi wao wa Kanisa.
Ni jambo la muhimu sana kwa mwamini kutambua hali yake na kujizuia kwenda kinyume
na sheria pamoja na utaratibu uliowekwa na Mama Kanisa.
Utafiti wa kina uliofanywa
Jimbo kuu la Torino, Kaskazini mwa Italia unaonesha kwamba, kuna asilimia kubwa ya
Mapadre nchini Italia wasiowafahamu wanandoa walioachika na kuamua kuoana tena, ambao
hawashiriki Komunio Takatifu. Hii inaonesha kwamba, kuna baadhi ya wanandoa walioachika
na kuamua kuoana tena wanaoendelea kukomunika licha ya kuwa na kizuizi cha kupokea
Sakramenti hii.
Baadhi ya Mapadre wamekiri kwamba, katika Parokia zao, kuna
kundi la waamini wachache ambalo limeendelea kuwa aminifu kwa mafundisho, sheria na
kanuni za Kanisa. Halikomuniki, lakini linaendelea kushiriki vyema katika maisha na
utume wa Kanisa. Kwa wanandoa wenye vikwazo pengine wanashindwa kutambua umuhimu wa
Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu katika maisha yao na hivyo wanajikuta
wakishiriki Mafumbo Matakatifu kwa mazoea!
Utafiti huo unaonesha kwamba, wakati
mwingine, hata Mapadre wenyewe licha ya kufahamu vizuizi vya wanandoa hao, wameendelea
kuwakomunisha kwa kuogopa macho na maneno ya watu ambayo yangeweza kubadilika na kuwa
ni kikwazo hasa kwenye vyombo vya habari!
Wanandoa wengine, ili kuogopa makwazo
katika Parokia zao, wanaamua kuhamia Parokia nyingine, wasikofahamika na hivyo wanaendelea
kukomunika. Hizi ni kati ya changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi wakati wa Maadhimisho
ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia. Bado kuna kundi kubwa la waamini
linalopokea Ekaristi Takatifu bila ya kufanya maandalizi makini ya maisha ya kiroho
kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.
Katika
hali tete kama hii, Mababa wa Sinodi watakuwa na mchango mkubwa katika kuyapatia ufumbuzi,
masuala haya yanayoendelea kusababisha mkanganyiko wa mawazo kuhusu Sakramenti ya
Ndoa, Ekaristi Takatifu na Upatanisho.