2014-07-31 15:36:27

Wapeni ninyi chakula!


Yesu anatamka mwenyewe maneno haya “wapeni ninyi chakula”. Tunayasikia haya leo katika Injili ya domenika ya kumi na nane ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa


Somo la kwanza lazungumzia juu ya karamu ya Bwana. Somo hili lituongoze kuelewa somo la Injili siku hii ya leo na maana nzima ya liturjia ya leo. Nabii anaandika neno hili taifa la Israeli wakiwa utumwani lakini baada ya mfalme kusaini mkataba wa kuwaweka huru kurudi kwao. Maneno ya Nabii ni ya uzima – wanaalikwa wale na wanywe. Bwana Mungu atafanya upya agano walilolivunja baada ya mji na hekalu kuharibiwa/kunajisiwa.

Nabii anaongozwa na imani yake kwa Mungu na uwezo wake juu ya historia ya ulimwengu. Nabii ana matumaini kwa historia inayoongozwa na Mungu. Anakumbuka karamu ya kutoka utumwani Misri – Kut. 12 – wanatoka utumwani na mlo unakuwa alama ya kukombolewa kwao. Utamaduni huu wa karamu unaonekana wazi katika Agano Jipya. Katika karamu ya chakula – uzima mpya unapatikana. Karamu ya chakula inahitimishwa na karamu kuu ya upendo – KARAMU YA MWISHO – KARAMU YA BWANA – ambao ni uzima wa kweli na wa milele.

Mhubiri maarufu Padre Munachi anatumia mfano huu ambao binafsi unanipa changamoto kubwa. Jamieson – mkulima maarufu na mcha Mungu akiwa anasali pamoja na mwanae jioni moja anasali hivi. Tuombe kwa ajili ya maskini yule pale barabarani ili Bwana amjalie mahitaji yake. Mara moja mwanae anaingilia kati na kumwambia baba yake – baba tusimsumbue Mungu bure. Tunaweza sisi kumpatia mahitaji yake maskini yule. Sisi tuchukue nafasi ya Mungu kwani ametujalia haya tuliyo nayo.


Pengine sala na matashi mema hayatoshi. Hata katika injili ya leo, mitume wanaonesha mapenzi kwa wale watu wenye njaa. Wanamwambia Bwana awaruhusu warudi kwao. Ni hapa Yesu anawaambia WAPENI NINYI CHAKULA. Kardinali Manning anasema – utakatifu haupatikani kwa kutenda jambo la pekee sana bali katika kutenda jambo la kawaida katika jicho la kimungu.

Katika Injili – Yesu alipowaambia wapeni ninyi chakula wanajiangalia kwa makini na kutambua kuwa kati yao kuna kijana mwenye mikate mitano na samaki wawili - Yoh. 6:9. Ajabu kweli, tena toka kwa kijana tu. Pengine twamfananisha na machinga kwa wakati wetu huu. Mtu ambaye tungeweza kumfukuza, anakuja kati yetu kutusumbua, sisi tunamsikiliza Yesu n.k.

Mara nyingi tunapokuwa na mahitaji tunamkimbilia Mungu – ni sawa kabisa. Leo anatualika pia kuona au kutambua kwanza karama au wezo wa jirani yetu. Mungu ametupatia wenzetu ili kwa njia yao tumtukuze Mungu na kuwapatia wenzetu mahitaji yao. Laiti kama tungetambua na kuheshimu uwezo, karama na nguvu ya Mungu katika wenzetu maisha yetu yangekuwa tofauti kabisa.

Pengine leo baada ya kusikia Injili hii tubaki na tafakari hii iwe ni tafakari ya kufanyia kazi leo na kuendelea kwa kila aliyesikia injili hii ya leo ukirudi nyumbani, katika familia, jumuiya, sehemu ya kazi, jaribu kuangalia karama, uwezo au cho chote chema alicho nacho mwenzako na kukitambua na ikibidi kumwomba kiwekwe hadharani. Kama wasemavyo wa leo – kuibua vipaji vya wenzetu.

Mtume Andrea alifaulu kuona kati ya watu wengi – kijana mwenye vipande vitano vya mkate na samaki wawili. Mara nyingi kama wale mitume tunaweza kuwatakia wenzetu mema lakini hatuko tayari kufanya kitu cha pekee. Katika injili twaona kuwa nia ya kutenda hata jambo dogo kwa upendo linaleta uhai na uzima. Wanaume elfu tano wakala, wakashiba bila kuhesabu wanawake na watoto.


Serikali ya Uingereza ilitaka kumtunuku Jenerali Gordon kwa utumishi wake uliotukuka huko China. Jenerali Gordon alikataa kupewa fedha na heshima yo yote ile, ila alipokea medali ya dhahabu ikionesha rekodi yake nzuri ya utendaji kwa miaka 33. Aliheshimu medali hii kama zawadi yake kubwa na ya pekee. Mara tu baada ya kifo chake medali ile haikuonekana mahali po pote. Katika harakati za kuitafuta ikafahamika kuwa aliitoa katika mji wa Manchester wakati wa njaa kali na aliagiza iuzwe ili kinunuliwe chakula kwa watu wenye njaa. Na siku hiyo alipoitoa iliandikwa kitu cha mwisho kabisa nilichokuwa nacho hapa duniani na nilichokithamini sana nimekitoa kwa Bwana Yesu Kristo.


Katika Injili twaona kuwa kama tukiweka nia yetu na mapenzi yetu katika matendo, hata kile kidogo tulicho nacho hubadilisha maisha. Hutupatia changamoto kubwa sana ya matumizi mazuri hata ya kile kidogo tulicho nacho. Injili inakuwajibishaje leo? Wewe una kitu gani – mikate mingapi na samaki wangapi? Unatoaje au kushirikisha wengine ulicho nacho? Pamoja na mengi mazuri yaliyopo au tuyafanyayo, bado ulimwengu wetu una njaa ya chakula, ya upendo, ya amani n.k.


Katika semina iliyofanyika kwa watoto na vijana – katika maswali 10 ya mwanzo yaliyoulizwa – mzazi/mlezi anakupa nini – ilitoka orodha ndefu ya vitu – ambavyo vingi vyao hata wanaopewa hawavihitaji. Watoto wetu na vijana wetu wanalalamika kuwa wanapewa vitu badala ya utu. Tena hawavihitaji kabisa. Ni changamoto kubwa.


Ndugu wapendwa, tutambue kuwa Mungu hakumuumba mtu pasipo kitu hivyo usiseme kuwa sina kitu cha kutoa. Ni kufuru kwa Mungu na watu wake.Hakuna maskini ambaye hana cha kutoa na hakuna tajiri ambaye hana cha kupokea. Hazina yako ni ipi? Au hazina yako ni nini/ipi? Lulu yako ni ipi? Je, unatambua karama ulizo nazo au alizo nazo jirani yako? Wewe una nini cha kutoa au unatoa nini au umeshatoa nini katika maisha yako?


Baba Mtakatifu Yohane Paulo II anatutaka sisi sote tuzidi kuwa wakarimu (Mane Nobiscum Domine - KAA NASI BWANA NO 28). Anatuambia kwamba ukarimu kwa wahitaji ndicho kipimo kitakachopima uhalisia wa uadhimishaji wetu wa Ekaristi. Tuone furaha katika kutoa kuliko kupokea.


Tumsifu Yesu Kristo. Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.