2014-07-31 08:57:46

Papa ni mjumbe wa upendo na huruma, ameguswa na mahangaiko ya watu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini katika barua yake ya kichungaji iliyochapishwa hivi karibuni baada ya kuhitimisha mkutano wake wa 109 wa mwaka linasema kwamba, hija ya kitume inayotarajiwa kufanywa na Baba Mtakatifu Francisko nchini humo mwanzoni mwa mwezi, yaani kuanzia tarehe 15 hadi tarehe 19 Januari 2015 ni kutaka kuwashirikisha wananchi wa Ufilippini ujumbe wa kichungaji unaojikita katika misingi ya upendo, huruma na kuguswa na mahangaiko ya watu. RealAudioMP3

Baba Mtakatifu Francisko atakuwa ni Papa wa tatu kutembelea Ufilippini baada ya watangulizi wake Paulo V Ina Mtakatifu Yohane Paulo II. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko inalenga kuwaimarisha ndugu zake katika imani kwa Kristo na Kanisa lake, ili waweze kuwa tayari kutolea ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo sanjari na kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha, pasi na kukata wala kujikatia tamaa. Ni mwaliko wa kutoka kifua mbele kwa ajili ya kuwatangazia wengine Injili ya Furaha.

Maaskofu wanasema, Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wananchi wote wa Ufilippini kusonga mbele kwa imani na matumaini baada ya kukumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha majanga makubwa kwa maisha ya watu na mali zao. Waamini na wananchi wa Ufilippini katika ujumla wao wanaalikwa kuanzia sasa kujiandaa kwa makini kukutana na Baba Mtakatifu Francisko, kwa kujivika mioyoni mwao fadhila ya unyenyekevu na huruma zinazopaswa kumwilishwa kila siku ya maisha yao.

Maaskofu wanasema, fadhila hizi zinaweza kutekelezwa kwa kuwafundisha watoto Biblia, kuwasaidia jirani zao wanaohitaji msaada wa hali na mali; kwa kuwatembelea na kuwasaidia wagonjwa na wafungwa. Lakini jambo la msingi katika maisha ya kiroho ni kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kuziishi Sakramenti za Kanisa kwa kujiandaa vyema. Kwa namna ya pekee, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu iwasaidie waamini kupata nguvu ya maisha ya kiroho inayobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe, ili waweze kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na Jamii kwa ujumla.

Waamini waonje huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho pamoja na kuzisaidia Familia zao kuwa kweli ni shule ya sala na utakatifu wa maisha; Familia Kanisa dogo la nyumbani, linalosali, linalotafakari Neno la Mungu na kulimwilisha katika imani tendaji. Yote hii ni mikakati inayoweza kuwasaidia waamini pamoja na wananchi wa Ufilippini kujiandaa kwa ajili ya ujio wa Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao.

Katika maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Ufilippini, wamekazia umuhimu wa wananchi kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, kama kielelezo cha furaha yao kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Changamoto hii wanasema Maaskofu Katoliki wa Ufilippini inapaswa kujionesha katika ngazi mbali mbali ya maisha, kwa kushuhudia ule wito wa kuwa kweli ni watoto wa Mungu. Wasimame kidete kulinda na kutetea Injili ya maisha pamoja na kuendelea kuchangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo ya nchi yao, huku utu na heshima ya mwanadamu ikipewa kipaumbele cha kwanza.

Maaskofu wanasema changamoto hii iguse dhamiri za wanasiasa, ili waweze kubadili na kuanza mchakato utakaosaidia kutibu na kung’oa kabisa Saratani ya rushwa, ufisadi na wizi wa mali ya umma, janga ambalo kwa sasa ni la kitaifa. Wanasiasa wanapaswa kujipambanua kwa kuonesha kwamba, uongozi ni huduma inayopania kusimamia na kutekeleza mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu.

Maaskofu wanawataka Makleri kuonesha ile sura ya Kristo mchungaji mwema anayejisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Wanakondoo wake. Katika historia ya maisha ya Kanisa nchini Ufilippini, kuna baadhi ya Makleri wameelemewa mno na ubinadamu kiasi cha kusababisha kashfa na makwazo kwa Familia ya Mungu. Lakini bado kuna kundi kubwa la Makleri na Watawa wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii bila upendeleo.

Ni wajibu wa wananchi wote wa Ufilippini kulinda na kutunza mazingira kama sehemu ya urithi wa kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemdhaminisha mwanadamu kwa ajili yake na kwa ajili ya kizazi kijacho. Uchafuzi wa mazingira na ukataji ovyo wa misitu ni mambo ambayo ni hatari kwa ustawi na maendeleo ya watu. Ni wajibu wa kila mtu kulinda na kutunza mazingira; kujenga na kuendeleza moyo wa mshikamano, kwa kusaidiana na kuwajibikiana kama ndugu wamoja wanaopania kukuza fadhila ya uaminifu inayojikita katika ushuhuda wa maisha.
Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.