Afrika ya Kusini yashikamana na wananchi wanaoteseka Mashariki ya Kati!
Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, limemwandikia barua ya mshikamano na
upendo Patriaki Fuad Tawal wa Yerusalemu pamoja na Familia ya Mungu huko Mashariki
ya Kati kutokana na vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati, hali ambayo imesababisha
mateso na mahangaiko makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia. Maaskofu wanakumbuka kwa
uchungu mkubwa madhulumu na nyanyaso wanazokabiliana nazo, jambo ambalo kamwe haliwezi
kuvumika.
Maaskofu wanasema, mateso na mahangaiko ya wananchi wa Palestina
yamefikia kiwango cha hali ya juu. Wanapenda kuungana nao kwa njia ya sala na mshikamano
wa dhati, kwa kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuongeza shinikizo litakalosaidia upatikanaji
wa amani ya kudumu huko Mashariki ya Kati. Ikiwa kama Afrika ya Kusini, ilifanikiwa
kukomesha utawala wa ubaguzi wa rangi, wanatumaini kwamba, mshikamano wa kimataifa
unaoweza kusaidia pia kukomesha vitendo vyote vya ukosefu wa haki msingi za binadamu.
Maaskofu wanawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni
mashahidi wa Injili na vyombo vya amani, ili kuweza kusitisha chuki na uhasama kati
ya watu. Maaskofu wanawahakikishia sala zao katika kipindi hiki kigumu! Ujumbe huu
umetiwa sahihi na Askofu mkuu Stephen Brislin, Rais wa Baraza la Maaskofu KatolikiAfrika
ya Kusini.