Mkutano mkuu wa wanafunzi vijana Wakatoliki kufanyika Libreville, Gabon
Mtandao wa Wanafunzi Wakatoliki Afrika, ulioanzishwa kunako mwaka 1987, kwa lengo
la kuwaunganisha wanafunzi waliosoma katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu
zinazomilikiwa na kuongozwa na Kanisa Katoliki Barani Afrika, kuanzia tarehe 3 hadi
tarehe 7 Agosti 2014, utaadhimisha mkutano wake mkuu wa saba unaofanyika kila baada
ya miaka miwili mjini Libreville, huko Gabon.
Mkutano huu unaongozwa na kauli
mbiu "Ujenzi wa mtandao wa wanafunzi vijana wakatoliki ili kulinda utambulisho wa
mwafrika Barani Afrika na Ulimwenguni". Lengo la mkutano huu ni kuwapatia fursa wanafunzi
vijana Wakatoliki kufanya tathmini kuhusu mchango wao ndani ya Kanisa na katika ulimwengu.
Vijana hawa pia watapata fursa ya kutafakari ujumbe wa siku ya kuombea amani
duniani uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2014. Ni ujumbe unaokazia
udugu kama njia ya amani. Vijana wanapenda kupambanua mbinu mkakati wa mawasiliano,
utakaowawezesha kutekeleza dhamana na wajibu katika maisha na utume wa Kanisa pamoja
na kuanzisha makao makuu yatakayosimamia na kuratibu kazi za mtandao huu.
Maadhimisho
ya mkutano huu yamegawanyika katika sehemu kuu mbili: sehemu ya kwanza itajadili kuhusu:
utawala bora, demokrasia, mikakati ya kujitegemea na udhibiti wa migogoro na kinzani
Barani Afrika. Sehemu ya pili itajikita zaidi katika masuala ya bajeti, uchaguzi wa
viongozi wapya pamoja na kuangalia Katiba ya Mtandao huu. Mkutano unatarajiwa kuhudhuriwa
na vijana kutoka katika nchi mbali mbali Barani Afrika.