Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kusaidia mchakato wa kusitisha vita huko Mashariki
ya Kati!
Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano
wa kimataifa mjini Vatican anasema kwamba, Sekretarieti ya Vatican imewatumia ujumbe
wa maandishi Mabalozi na wawakilishi wa nchi na mashirika mbali mbali ya kimataifa
mjini Vatican ili kuonesha wasi wasi na hofu ya Baba Mtakatifu Francisko kuhusu kuteteleka
kwa amani huko Mashariki ya Kati.
Wakristo wanaendelea kuteseka na kudhulimiwa;
Makanisa na nyumba za Ibada zinaendelea kuharibiwa na kwamba, wakristo hawana nafasi
tena ya kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu hata katika nchi yao wenyewe! Ikumbukwe
kwamba, Wakristo huko Iraq kama ilivyo kwa nchi nyingine huko Mashariki ya Kati, wamekuwepo
huko zaidi ya miaka elfu na kwamba, wamechangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na
maendeleo ya Mashariki ya Kati. Wakristo wanataka kuendelea kuishi katika nchi yao
ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa amani na upatanisho.
Askofu
mkuu Mamberti anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika matukio mbali mbali anaendelea
kuonesha mshikamano wake wa pekee kwa Wakristo na watu wote wanaoteseka huko Mashariki
ya Kati kutokana na vita. Anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kuendelea
kusali, ili amani ya kweli iweze kupatikana. Baba Mtakatifu kwa njia ya Baraza la
Kipapa linaloratibu Misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum amepeleka msaada wa kiuchumi
kwa ajili ya wananchi wanaoteseka huko Mashariki ya Kati.
Sekretarieti ya Vatican
inaendeleza mchakato wa mikakati ya kidiplomasia, ili kuwahamasisha viongozi wakuu
wa Jumuiya ya Kimataifa kuyaangalia mateso na mahangaiko ya Wakristo huko Mashariki
ya Kati. Ni matumaini ya Vatican kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaguswa na kuanza kushughulikia
mateso ya wananchi wa Iraq katika ujumla wao kwani vitendo vinavyofanyika huko Mashariki
ya Kati vinagusa utu na heshima ya binadamu na haki zake msingi. Haya ni mambo msingi
yanayowawezesha wananchi kuishi kwa amani na utulivu, hata katika tofauti zao msingi.
Askofu mkuu Dominique Mamberti anasema, inasikitisha kuona kwamba, vita inayoendelea
huko Mashariki ya Kati imeanza kuzoeleka, lakini watu wakaendelea kuteseka na kupoteza
maisha. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhamasisha waamini na watu wote wenye
mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki ya Kati. Kuna haja kwa
Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, vita inasitishwa, amani inatawala kwa ajili
ya ustawi na mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu.