Yesu Kristo awe ni kiini cha maisha na utume wa Wakristo!
Mchungaji Giovanni Traettino wa Kanisa la Kipentekoste mjini Caserta, Italia, Siku
ya Jumatatu, tarehe 28 Julai 2014, amemshukuru kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu Francisko
kwa kuwapatia heshima ya kuwatembelea na kukaa kwa pamoja mbele ya Mwenyezi Mungu.
Wakristo hawa wamemhakikishia Baba Mtakatifu Francisko kwamba wanampenda na wanamwombea
katika maisha na utume wake na kwamba, kuteuliwa kwake ni zawadi kubwa kutoka kwa
Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa na Ulimwengu kwa ujumla.
Katika maisha yake,
anasema Mchungaji Traettino kwamba, Baba Mtakatifu anaweza kuwaendea watu na kugusa
undani wa mioyo yao sanjari na kujenga mahusiano thabiti ya kijamii, kwa kutambua
kwamba, wote ni ndugu katika Kristo Yesu, kielelezo cha uhuru na ujasiri katika kutambua
mapungufu ya kibinadamu, tofauti zilizopo kati ya Makanisa na matumaini ya kujenga
umoja miongoni mwa Wakristo, changamoto endelevu kutoka kwa Yesu mwenyewe.
Ni
vigumu sana kujenga umoja pasi na unyenyekevu na kwamba, Mitume walitambua Ukuu wa
Mungu uliokuwa umejificha katika maisha ya mwanadamu na kwamba, ukweli ni mchakato
unaowawezesha watu kukutana na hiki ni kiini cha ujumbe wa Kikristo. Ni mwaliko wa
kutubu na kumwongokea Yesu Kristo, ambaye ni hazina kuu, inayomshirikisha mwanadamu
furaha ya kweli na kwamba, Yesu Kristo anapaswa kuwa ni kiini cha maisha na utume
wa Wakristo, kwa kutendeana mema.
Mchungaji Traettino anasema, kukutana na
Yesu ni kukutana na ukweli ambao ni sehemu ya vinasaba vya Injili vinavyowawezesha
Wakristo kuendeleza majadiliano ya kiekumene, ili wote waweze kuwa wamoja, kwa kujielekeza
zaidi katika majadiliano ya kiekumene yanayobubujika kutoka katika maisha ya kiroho,
ili kujenga umoja wa kweli kati ya watu wa mataifa sanjari na ujenzi wa Umoja wa Fumbo
la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Hapa kuna haja kwa wakristo kutubu na kumwongokea
Mwenyezi Mungu.
Fumbo la Umwilisho ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha
upendo wa Mungu kwa binadamu; Mungu ambaye anajitambulisha kwa njia ya maskini na
wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Wakristo wanaalikwa kuifia dhambi na ubinafsi
wao, tayari kufufuka na kuvikwa taji ya utukufu na Roho Mtakatifu. Wakristo wanatumwa
kutangaza Habari Njema ya Wokovu na kuwafunda watu kadiri ya Mafundisho ya Yesu.
Lengo
ni kujenga na kuimarisha umoja katika imani, kwa kuonea aibu utengano, vita, madhulumu
na kinzani hata nchini Italia. Pamoja na yote haya kuna haja kwa Wakristo kujielekeza
zaidi na zaidi katika upatanisho, kanuni maadili, upendo, uwajibikaji kama ambavyo
inajionesha kwa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko.
Wakristo hawana
budi kuwa ni kielelezo cha upatanisho unaobubujika kutoka katika undani wa maisha
yao na kujidhihirisha kwa wao kujipatanisha na Yesu, ili kukumbatia Msalaba, kielelezo
cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu; upendo unaompatanisha binadamu
na Muumba pamoja na jirani yake. Wakristo wa Kanisa la Kipentekoste wanamheshimu sana
Mtakatifu Francisko wa Assis anayewachangamotisha kutafuta kwanza mambo msingi.