2014-07-29 08:47:05

Serikali ya Chad inaridhishwa na mahusiano kati yake na Vatican


Askofu mkuu Franco Coppola, Balozi wa Vatican nchini Chad, hivi karibuni aliwasili nchini Chad na kupokelewa na viongozi wa Kanisa mahalia, tayari kuanza utume wake nchini humo kwa kuwasilisha hati za utambulisho kwanza kabisa kwa Waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikishano wa kimataifa Bwana Moussa Mahamat Dabo.

Serikali ya Chad inaridhika na uhusiano mwema uliopo kati yake na Vatican na kwamba, inatambua mchango mkubwa unaotekelezwa na Kanisa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu.

Askofu mkuu Coppola akiwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais Idriss Dèby Itno wa Chad aliyekuwa ameambatana na viongozi mbali mbali wa Serikali, Rais amemshukuru kwa namna ya pekee baba Mtakatifu Francisko kwa maisha na utume wake kwa ajili ya Kanisa, lakini zaidi kama mtetezi wa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Serikali ya Chad itaendelea kuunga mkono juhudi za Kanisa mahalia katika kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kanisa Katoliki linapenda kukuza na kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, watu wakiheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, licha ya tofauti zao za kidini, kikabila na mahali anapotoka mtu! Kanisa litaendeleza mchakato wa kudumisha amani kwa kuwashirikisha vijana ambao kimsingi ndio wadau wakuu wanaoweza kujenga au kubomoa amani, ikiwa kama hawatafundwa kikamilifu.

Chad imeendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa Barani Afrika kwa wananchi wake licha ya tofauti zao za kidini kuendelea kuheshiminiana na kuishi pamoja kama watoto wa Baba mmoja.

Askofu mkuu kama sehemu ya utambulisho wake, ameadhimisha pia Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na Familia ya Mungu nchini Chad. Ametumia fursa hii kuwasilisha hati zake za utambulisho kutoka kwa Katibu mkuu wa Vatican Kardinali Pietro Parolin na kumkabidhi Askofu Jean Claude Bouchard, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Chad.







All the contents on this site are copyrighted ©.