Roho Mtakatifu ni kielelezo cha umoja na utofauti wa karama ndani ya Kanisa!
Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha Wakristo kufanya hija ya pamoja wakiwa wameambatana
na Yesu ambaye daima amejidhihirisha kuwa ni mvumilivu, hata pale wanapotenda dhambi,
hakuna sababu ya kusimama wala kukata tamaa, bali wawe ni watu wenye matumaini. Yesu
ni mwanga unaowaangazia waja wake katika hija ya maisha yao hapa duniani pamoja na
kuwajalia nguvu ya kutembea salama.
Baba Mtakatifu ameyasema hayo, Jumatatu
tarehe 28 Julai 2014 alipomtembelea rafiki yake Mchungaji Giovanni Traettino wa Kanisa
la Kipentekoste kwenye Kanisa la Upatanisho ambalo bado linaendelea kujengwa huko
Caserta, Tukio hili limehudhuriwa pia na umati wa waamini wa Kanisa la Kipentekoste
kutoka ndani na nje ya Italia. Baba Mtakatifu anasema, katika mahangaiko ya kuganga
njaa, watoto wa Yakobo walibahatika kukutana na ndugu yao Yosefu waliyekuwa wamemsaliti
kwa kumuuza utumwani Misri.
Wakristo wanapaswa kutembea huku wakiwa wameshikamana
ili kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa, kwa kuvuka kikwazo cha chuki na uhasama
mambo ambayo kwa sasa hayana tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya Kanisa la
Kristo. Kazi kubwa inayotekelezwa na Shetani ni kupandikiza mbegu ya utengano kati
ya Wakristo, lakini ikumbukwe kwamba, Yesu katika sala yake ya Kikuhani ameombea umoja
wa Kanisa, hata katika utofauti wake, kazi ambayo inatekelezwa na Roho Mtakatifu.
Baba
Mtakatifu anasema hapa kuna haja ya kujenga umoja uliopatanishwa na Roho Mtakatifu,
kwa kuwawezesha Wakristo kushirikishana karama katika maelewano. Utandawazi ulichangamotishe
Kanisa kushikamana kwa kuendelea kujikita katika taalimungu ya kiekumene mintarafu
kazi ya Roho Mtakatifu sanjari na kutembea mbele ya Mwenyezi Mungu, ili kukutana na
ndugu katika Kristo.
Baba Mtakatifu Francisko amegusia kuhusu Fumbo la Umwilisho,
Neno wa Mungu alipofanyika mwili na kukaa kati ya watu wake. Yesu ni Mtu kweli na
Mungu kweli, aliyezaliwa bila kuumbwa, Mwenye Umungu mmoja sawa na Baba, kielelezo
cha upendo wa Mungu kwa binadamu na changamoto kwa binadamu kupendana wao kwa wao,
lakini zaidi kwa kuonesha upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa
Jamii.
Wakristo wanahimizwa kwenda pembezoni mwa Jamii ili kuwatangazia watu
Injili ya Furaha, kwani watu wana kiu na njaa ya kukutana na Mungu pamoja na kusikia
ukweli kuhusu Yesu Kristo. Ikumbukwe kwamba, Injili ni kielelezo cha upendo, ukweli,
uzuri na furaha. Wivu na chuki ni vikwazo katika kutangaza Injili ya Furaha na matokeo
yake ni Wakristo kugawanyika na hata kudhulumiana kama ilivyojitokeza kwa baadhi ya
Wakatoliki kuwanyanyasa Wakristo wa Makanisa ya Kipentekoste, kwani walionekana kuwa
kama "kiwingu".
Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuomba msamaha
kwa dhuluma na nyanyaso zilizofanywa na Wakatoliki dhidi ya Wakristo wa Kanisa la
Kipentekoste. Anamwomba, Mwenyezi Mungu awakirimie ujasiri wa kutambua udhaifu huu
na kuthubutu kuomba msamaha. Ukweli unawawezesha watu kukutana katika hija ya maisha
kwa kumtafuta ili hatimaye kuweza kumkumbatia Yesu ambaye daima anawatangulia katika
hija na mahangaiko yao ya ndani.
Baba Mtakatifu amewashukuru wenyeji wake kwa
kumwezesha kukutana na Wakristo wa Kanisa la Kipentekoste na kushirikishana nao utajiri
wa maisha na utume wa Kanisa, daima wakijitahidi kumwendea Yesu ambaye ndiye yule
Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za dunia. Wafuasi wa kwanza waliokutana na
Yesu, walibadilika na kuwa watu wapya zaidi, kiasi cha kuwa ni watakatifu wanaojikita
katika umoja wa Kanisa. Wakristo waendelee kushirikiana katika umoja na mapendo kama
ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika uhalisia wa maisha!