Huu ni wakati wa kutenda kwa unyenyekevu, amani na utulivu wa ndani!
Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alifanya mahojiano na gazeti moja linalochapishwa
nchini Argentina, El Clarin, ili kuzungumzia mambo msingi yaliyojiri katika maisha
na utume wake katika kipindi hiki tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki.
Kwa bahati mbaya kuna watu wengi wanadhani kwamba, siri ya furaha inajikita
katika afya njema, upendo, mali, madaraka na mambo kama haya, lakini Baba Mtakatifu
anasema, watu wanapaswa kuishi kadiri wanavyokirimiwa na Mwenyezi Mungu pasi na kutafuta
makuu. Katika ujana wake, alikuwa bega kwa bega kumsaidia mama yake katika kazi za
nyumbani na kwamba, alimsindikiza mama yake mzazi hata katika dakika zake za mwisho
wa maisha yake, akiwa na furaha na utulivu wa ndani kutokana na kazi kubwa aliyoifanya
katika maisha yake.
Baba Mtakatifu anasema, changamoto kubwa kwa watu wa kizazi
hiki ni kuonesha upendo na mshikamano wa dhati kwa watu wanaotafuta nafuu katika maisha
yao; watu wanaokimbia vita, nyanyaso, dhuluma na majanga asilia. Bara la Ulaya kwa
sasa linawaogopa wahamiaji, lakini hata hivyo kuna nchi kama Uswiss ambayo hata katika
udogo wake, imekuwa ni kielelezo cha upendo na mshikamano kwa kutoa hifadhi kwa wahamiaji
laki nane.
Kuna tofauti kubwa kati ya watu wanaoishi Kaskazini na Kusini, kiasi
kwamba, hakuna uwiano mzuri wa matumizi ya rasilimali ambayo kimsingi ni zawadi kubwa
kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayopaswa kutumiwa kwa ajili ya mafao ya wengi. Kuna idadi
kubwa ya maskini wa hali na kipato katika nchi changa duniani, ingawa wana utajiri
na rasilimali nyingi. Uchimbaji wa madini umekuwa ni chanzo kikubwa cha uchafuzi wa
mazingira hali ambayo inasababisha majanga makubwa kwa watu!
Baba Mtakatifu
anasema, katika maisha yake hajawahi kutamani mambo makubwa yanayozidi uwezo wake.
Alipokuwa kijana alijiona kuwa ni mwamba thabiti na wakati wa ujana wake amekuwa kama
ni mto unaotembea na katika uzee anajiona kwamba, kasi ya maji imepungua kwa kiasi
kikubwa. Huu ni wakati wa kufanya kazi kwa unyenyekevu, uvumilivu, amani na utulivu!