2014-07-28 09:03:06

Majivuno na kiburi vikiondoka, hapo unajenga urafiki na Mungu


Mpendwa msikilizaji wa Kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, tupo katika mfululizo wa vipindi vyetu juu ya Kanisa la nyumbani kama shule ya fadhila. Kwa wakati huu tunaitazama fadhila ya unyenyekevu kama fadhila mama ya fadhila nyinginezo kwani ndiyo ambayo huondoa kiburi na majivuno. Majivuno na kiburi vikiondoka, hapo tayari umeshakuwa rafiki wa Mungu, na fadhila nyingine zote zitapata uwanja. RealAudioMP3

Mara nyingi kiburi kinatufanya tupoteze urafiki wetu na binadamu wenzetu, na hatimaye na Mungu. Mtakatifu Augustino anasema, ‘kiburi kiliwafanya malaika wakawa mashetani’. Na sisi kwa njia ya kiburi, maringo na majivuno, tunajishetanisha. Namna bora zaidi ya kukwepa kujishetanisha ni kuiambata fadhila ya unyenyekevu.

Kila mmoja ajifunze kuwa mnyenyekevu. Ukiwa mnyenyekevu wewe ni fahari ya Mungu na ni heshima ya watu pia. Faida nyingine za kuwa mnyenyekevu ni hizi:- Utaijua haki na utakuwa mtetezi wa haki. Utaelekezwa vema na utatetewa siku ya dhiki na watu watasikitikia mateso yako (lakini ukiwa mwenye kiburi na maringo, siku ya dhiki watu watashangilia matatizo yako). Ukiwa mnyenyekevu, utafundishwa na kujifunza mema.

Ukiwa mnyenyekevu, utaonywa na utasahihishwa makosa yako, na hivyo utasaidiwa kuwa mtu mwema zaidi. Ukiwa mnyenyekevu utafikika na wengi na utakuwa msaada kwa watu/kimbilio la watu. Zaidi sana, ukiwa mnyenyekevu utapendwa na Mungu na mwisho utakufa kifo chema sana na kuungana na Mungu katika karamu ya wanyenyekevu huko mbinguni.

Kwetu sisi tunaomsadiki Kristo, kioo cha fadhila hii ni Kristo mwenyewe ambaye “daima alikuwa Mungu, lakini hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kung’ang’ania kwa nguvu...bali alijinyenyekesha akawa mtii mpaka mauti” (Fil.2:6-8)

Tukitaka tuone mkono wa Mungu katika miasha yetu, basi, na tuwe wanyenyekevu. Tunaambiwa “nyenyekeeni mbele za Bwana, naye atawainueni” (Yak. 4:10). Baraka ya Mungu huwaelekea walio wanyenyekevu. Kukosa fadhila ya unyenyekevu ni kufukuza baraka ya Mungu na ni kufukuza matashi mema ya watu pia.

Katika kipindi hiki tuone baadhi ya watakatifu wanasema nini kuhusu unyenyekevu. Bwana asema “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu”. (Mt 11:29). Yeye ndiye kioo cha unyenyekevu. Na watakatifu wote walimtazama Kristo aliye mfano wa unyenyekevu na wakamfuasa. Nasi huku tukivuviwa na mifano ya watakatifu, tunaalikuwa kumtazama Kristo na kumwomba daima tukisema “ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, fanya mioyo yetu ifanane na moyo wako”.

Mtakatifu Thoma wa Villanova anasema, “unyenyekevu ni mama wa fadhila nyingi, kwa sababu kutokana na unyenyekevu tunapata utii, heshima, uchaji, uvumilivu, kiasi, upole, amani. Aliye mnyenyekevu atakuwa mtii, ataogopa kuwaudhi watu, yuko katika amani na wote, anaishi kwa furaha, na yupo katika amani kubwa.”

Mt. Filip Neri anasema “Bila unyenyekevu mtu hawezi kuwa Mtakatifu.” Unyenyekevu ni ngazi imara ya kuupandia utakatifu. Mt. Augustino akiongelea unyenyekevu kama daraja anasema “Kimsingi ni katika unyenyekevu mtu anafanywa kuwa mfuasi wa Kristo, na kwa hilo roho inaandaliwa kuungana na Mungu.” Mambo yote ni lazima yapate msingi wake katika unyenyekevu. Naye akitambua thamani ya unyenyekevu daima alisali “Ee, Bwana unijalie hazina ya unyenyekevu.”

Mt. Joseph wa Calasanctus daima aliwaasa vijana wake kuwa “Kama unataka kuwa mtakatifu basi jifunze na ujivike unyenyekevu. Na kama wataka kuwa mtakatifu mkubwa zaidi ongeza juhudi ya fadhila ya unyenyekevu zaidi. Kama unataka kuwa mtakatifu usiruhusu siku ipite pasipo kutafakari juu ya madhaifu na mapungufu yako, uduni na hisia za kujidharau nafsi.”

Mtakatifu Antoni wakati alipokuwa akiitazama mitego mingi ya shetani ajiuliza, ni nani atakayevuka mitego yote hii!! kisha akajijibu akisema, ni wanyenyekevu tu ndio watapita katika mitego hii ya shetani, na watatoka katika fujo za ulimwengu huu wakiwa salama. Mtu mnyenyekevu hatanaswa na kuangamizwa na hila za ulimwengu.

Mt. Bernadi anasema “unyenyekevu” ni fadhila ambayo kwa kujitambua mwenyewe mtu anajifanya au kujiona duni na hivyo kutojikweza binafsi. Mt. Theresa wa Mtoto Yesu anasema unyenyekevu ni ukweli wa moyo, na hivyo Bwana anawapenda wanyenyekevu kwa sababu wanaupenda ukweli.

Naye Mtakatifu Benedikto katika Kanuni yake, anatupatia vipandio kumi na viwili vya unyenyekevu, akituonesha kuwa fadhila ya unyenyekevu ni muhimu sana kwa mtu anayepiga mbio kuutafuta utakatifu. Ni kwa njia ya unyenyekevu wa kweli tutapita salama katika mashindano ya duniani hapa, na mwisho wa uzima tutamwona Mungu.

Basi mpendwa msikilizaji, hadi hapo tunahitimisha tafakari yetu juu ya fadhila ya unyenyekevu. Ni fadhila ngumu lakini ni ya muhimu sana, na inawezekana kabisa kuwa mnyenyekevu. Daima tusali kama Mtakatifu Augustino tuseme, “Ee Bwana unijalie hazina ya unyenyekevu.”

Kutoka katika Studio za Radio Vaticani, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.