2014-07-28 16:10:30

Majadiliano ya kiekumene yaguse undani wa maisha ya watu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu asubuhi tarehe 28 Julai 2014 kwa mara nyingine tena amerejea mjini Caserta, kutekeleza adhima yake ya kumtembelea rafiki yake Mchungaji Giovanni Traettino wa Kanisa la Kipentekoste aliyempokea mbele ya Kanisa la Upatanisho ambalo bado linaendelea kujengwa na baadaye viongozi hawa wawili wakafanya mazungumzo ya faragha.

Waamini wa Kanisa la Kipentekoste wameonesha furaha na upendo mkubwa kwa Baba Mtakatifu Francisko na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii kubwa kwa ajili ya Kanisa kwa nyakati hizi. Viongozi hawa wawili wamezungumzia kuhusu upatanisho pamoja na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kikekumene yanayojikita kwa Kristo mwenyewe pamoja na kutambua kwamba, kuna tofauti msingi kati ya Makanisa haya, lakini kwa pamoja yanaungama imani moja kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anasema, amependa kwenda kuwatembelea ndugu zake katika Kristo kwani wao tayari wamekwishafika kumtembelea mara nyingi mjini Vatican. Ni hija ya kuomba msamaha na huruma ya Mungu kwa Wakatoliki ambao wamewatesa na kuwadhulumu Waamini wa Makanisa ya Kipentekoste. Wakristo wote watambue kwamba ni wao ni ndugu na wamoja katika Kristo na kwamba, anayepeswa kupewa sifa na utukufu ni Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Baba Mtakatifu amewataka Wakristo kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene bila ya kusimama wala kukata tamaa. Jambo la msingi ni kwa waamini kujibidisha kukutana na Yesu kwa njia ya Maandiko Matakatifu, Sakramenti na huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kwa kukutana na Yesu Kristo, waamini wanachangamotishwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kweli.

Mchungaji Traettino katika mazungumzo yake anasema kwamba, ametafakari kwa kina na mapana kuhusu Fumbo la Umwilisho, lakini badala ya kuamua kuandika barua kwa rafiki yake, Papa Francisko ameamua kuja na kusali pamoja nao, ili kuonja uwepo wa Kristo katika maisha ya wafuasi wake, ili kujengana na kuimarishana katika imani kwa Kristo na Kanisa lake. Hapa Kanisa linaonesha umoja katika utofauti wake.

Ziara hii ambayo Baba Mtakatifu alipenda iwe ni faragha kati ya marafiki wawili, lakini limegeuka kuwa ni tukio la kimataifa kwa kuwakutanisha waamini Kanisa la Kipentekoste kutoka ndani na nje ya Italia. Kwa mara ya kwanza viongozi hawa wawili walikutana kwenye Uwanja wa Michezo wa Olympic mjini Roma wakati Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kusali na Chama cha Uamsho wa Kikristo.

Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa kichungaji, Injili ya Furaha anawaalika wakristo kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayogusa undani wa mtu: kiroho na kimwili. Majadiliano ya kiekumene ni njia muafaka ya Uinjilishaji mpya, inayowataka Wakristo kushuhudia imani yao kwa njia ya matendo. Wakristo wa Makanisa mbali mbali anasema Baba Mtakatifu wanaweza kutajirishana kwa kushirikishana karama walizokirimiwa na Roho Mtakatifu.







All the contents on this site are copyrighted ©.