2014-07-28 09:57:24

Kumbu kumbu ya miaka 100 tangu Vita kuu ya Kwanza ya Dunia ilipotokea!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 27 Julai 2014 katika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alikumbusha kwamba, tarehe 28 Julai 2014, Jumuiya ya Kimataifa inafanya kumbu kumbu ya miaka mia moja tangu Vita kuu ya Kwanza ya Dunia ilipoanza na kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao.

Papa Benedikto wa kumi na tano wakati huo alisema kwamba, vita hii ni majanga yasiyokuwa na mafao wala mashiko, hali ambayo ilipelekea mateso ya watu kutoka sehemu mbali mbali kwa kipindi cha miaka minne, amani ikawekwa rehani! Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 28 Julai 2014 iwe ni siku ya maombolezo. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, makosa yaliyofanyika huko nyuma hayatajirudia tena na kwamba, watu watajifunza kutokana na historia kwa kutoa nafasi kwa amani kutawala kwa njia ya majadiliano yanayojikita katika uvumilivu na ujasiri.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu ameyaelekeza mawazo yake katika maeneo makuu matatu ambako mtutu wa bunduki unaoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Maeneo haya ni: Mashariki ya Kati, Iraq na Ukrain. Baba Mtakatifu anaendelea kuwaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja naye kwa njia ya sala ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia watu na viongozi katika mataifa haya hekima na nguvu wanazohitaji katika kuimarisha mchakato wa amani kwa kukabiliana na changamoto zote kwa njia ya majadiliano na upatanisho. Kini cha yote ni mafao ya wengi na heshima kwa kila mtu.

Kwa njia ya vita kila kitu kinaweza kutoweka na kuharibika, lakini kwa njia ya amani, kila kitu kinadumishwa. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba: vita inawapokonya watoto matumaini na maisha bora kwa siku za usoni; vita inasababisha vifo, majeraha na vilema; vita inasababisha watoto kubaki yatima na kwamba, watoto hawana vitu vya kuchezea bali mabaki ya silaha; vita inasababisha watoto kukosa tabasamu katika maisha yao. Baba Mtakatifu anawataka wahusika kusitisha vita kwani inaendelea kusababisha madhara makubwa kwa watu!







All the contents on this site are copyrighted ©.