Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki,
Jumapili tarehe 27 Julai 2014 ameadhimisha Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu kwenye
Kanisa kuu la Mtakatifu Diego, Calfornia, ili kusali kwa ajili ya kuwaombea Wakristo
wanaoteseka huko Iraq, Syria, Palestina na Misri.
Wamewakumbuka pia wananchi
wanaoteseka kutokana na vita huko Ukrain. Waamini wa Makanisa ya Mashariki wanamshukuru
sana Baba Mtakatifu Francisko kwa kuonesha moyo wa upendo na mshikamano kwa Wakristo
na wote wanaoteseka sehemu mbali mbali kutokana na dhuluma za kidini pamoja na vita.
Kardinali Sandri amewapongeza Wakristo kwa kuendelea kuwa mashahidi wa imani na waaminifu
kwa Injili ya Kristo hasa katika kipindi hiki kigumu cha maisha yao.
Waamini
wanaendelea kuhamasishwa kushikamana kwa dhati na wote wanaoteseka kutokana na kulazimika
kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao. Waamini wasikate
tamaa, bali waendelee pia kusali kwa ajili ya kuombea haki, amani na upatanisho wa
kitaifa.
Ibada hii imehudhuriwa na viongozi na wakristo kutoka katika Makanisa
ya Mashariki wanaoishi mjini Calfornia. Kardinali Sandri amekutana na kuzungumza pia
na waamini wa Makanisa ya Mashariki kutoka Jijini Los Angeles na San Diago. Akiwa
nchini Marekani anatarajia pia kuwatembelea na kuzungumza na Wakristo wa Makanisa
ya Mashariki ili kwa pamoja kuweza kuangalia changamoto zinazojitokeza katika mikakati
ya shughuli za kichungaji.