2014-07-28 09:11:15

Jengeni msingi wa familia katika utakatifu wa maisha!


Inapendeza na kufurahisha kuona Familia ambayo kimsingi ni Kanisa dogo la nyumbani imechangamka, wanafamilia wakijitahidi kuishi kwa amani, upendo na mshikamano unaojengeka kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee ambao ni tunu msingi ya maisha ya kijamii. Hali kama hii inajenga matumaini makubwa katika maisha ya ulimwenguni hapa na matumaini katika maisha ya uzima wa milele. Huu ndio ushuhuda uliotolewa na Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria, ambao Kanisa limefanya kumbu kumbu yao, hapo tarehe 26 Julai 2014.

Katika mahubiri yake kwenye Siku kuu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria, iliyofanyika kwenye Parokia ya Mtakatifu Anna iliyoko mjini Vatican, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amekumbushia kwamba, Watakatifu hawa ni mfano na kielelezo cha familia inayosimikwa katika maisha ya utakatifu na chombo thabiti kilichoshiriki kikamilifu katika Fumbo la Umwilisho wa Mwana mpendwa wa Mungu, yaani Yesu Kristo, kwa njia ya Bikira Maria.

Kanisa linawashukuru kwa namna ya pekee Watakatifu Joakim na Anna, kwani kwa njia yao, wamemzawadia Mwenyezi Mungu, Bikira Maria aliyebahatika kuteuliwa kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa. Familia hii ni kati ya Watu wa Mungu walioshiriki kurithisha imani na mapendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya upendo unaojikita ndani ya familia, kiasi kwamba, Bikira Maria akawa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili akakaa kati ya watu wake.

Kardinali Parolin anasema, Familia ni nguzo thabiti na urithi wa binadamu wote, iliyopewa dhamana ya kurithisha imani na kwamba, ni taasisi muhimu sana katika Jamii. Ikumbukwe kwamba, watoto na wazee ni viungo muhimu katika kuendeleza jamii, kwani watoto wanachukua ndani mwao amana na historia ya maisha ya jamii inayowazunguka na wazee kwa upande wao, wanarithisha uzoefu, mang’amuzi na hekima inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao.

Familia ya Watakatifu Joakim na Anna ni changamoto kwa familia za kikristo kuhakikisha kwamba, zinatekeleza dhamana na wajibu wake kwa kujikita katika utakatifu wa maisha kama inavyojidhihirisha pia kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema wanahimizwa kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea familia hasa wakati huu, Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia, itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014.

Wazazi ni vyombo muhimu sana katika kurithisha Injili ya uhai kama ilivyokuwa kwa Watakatifu Joakim na Anna, walioshiriki kwa namna ya pekee kumwandalia Mwana wa Mungu makazi hapa duniani. Kumbe, uaminifu katika maisha ya familia ni jambo ambalo linapaswa kudumishwa kama anavyokazia Mama Kanisa. Ibada ikwa Mtakatifu Anna imeenea sana ndani ya Kanisa.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.