Chama cha Mtakatifu Anna Jimbo kuu la Mombasa kinaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 60
tangu kuanzishwa kwake!
Chama cha Wanawake cha Mtakatifu Anna, Jimbo kuu la Mombasa, Kenya, hivi karibuni
kimeadhimisha kumbu kumbu ya miaka sitini tangu kilipoanzishwa kama chombo makini
cha Uinjilishaji miongoni mwa Wanawake Wakatoliki, Jimbo kuu la Mombasa.
Ibada
ya Misa takatifu katika maadhimisho haya imeongozwa na Padre Boniface Malai aliyekazia
dhamana na nafasi ya wanawake wakatoliki katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaopania
kuwapatia waamini nyenzo za kuweza kushuhudia imani yao kwa njia ya matendo mema na
adili.
Padre Malai ambaye ni Dekano wa Dekania ya Taita, Taveta, Jimbo kuu
la Mombasa amewataka wanawake kujifunga kibwebwe ili kushirikiana na mihimili mingine
ya Uinjilishaji mpya katika utangazaji wa Injili ya Furaha miongoni mwa watu wa mataifa.
Wanawake wanakumbushwa kwamba, wao ni viungo muhimu sana katika kulea na kurithisha
imani kwa watoto wao. Wanawake Wakatoliki wakipania wanaweza kulitegemeza Kanisa mahalia
katika nyanja mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa.
Kumbu kumbu ya Miaka
sitini tangu kuanzishwa kwa Chama cha Mtakatifu Anna, zimekwenda sanjari na maadhimisho
ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria, iliyoadhimishwa
hapo tarehe 26 Julai 2014. Zaidi ya wanawake mia nane kutoka Dekania ya Taita, Taveta
walikusanyika pamoja ili kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa matendo
makuu aliyowakirimia katika maisha na utume wao ndani ya Jimbo kuu la Mombasa.
Katika
maadhimisho haya wanawake kumi waasisi wa Chama cha Mtakatifu Anna walikuwepo, jambo
la kutia faraja na matumaini kwamba, inawezekana watu kuwa waaminifu katika maisha
na utume wa Kanisa!
Wakati huo huo, Bibi Felista Kirigha, Mwenyekiti wa Dekania
ya Taveta, amewashukuru Mapadre na watawa kwa huduma zao makini kwa ajili ya ustawi
na maendeleo ya Wanawake Wakatoliki Jimbo kuu la Mombasa. Ameitaka Familia ya Mungu
Jimbo kuu la Mombasa, kushikamana na kushirikiana kwa pamoja ili kwa pamoja waweze
kulijenga Kanisa la Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.
Wanawake wamekumbushwa
kwamba, wanayo nafasi ya pekee kabisa katika kurithisha, kukuza na kulea misingi ya
imani, maadili na utu wema. Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika maisha na utume
wa Kanisa hasa kwa kushiriki katika Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo. Wanawake wanatakiwa
kusimama kidete kuwa ni watangazaji makini wa Imani kwa njia ya ushuhuda wa maisha
yao, kwa kuendelea kutangaza pia Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaozinyemelea
familia nyingi duniani.
Katika Ibada hii ya Misa Takatifu wanachama wapya thelathini
na wawili wamepokelewa katika Chama cha Wanawake wa Mtakatifu Anna, ili kuendeleza
dhamana ya chama hiki katika maisha na utume wa Kanisa. Ibada hii imehudhuriwa na
Mapadre, watawa na waamini walei kutoka Dekania ya Taita, Taveta, Jimbo kuu la Mombasa,
Kenya.