2014-07-26 10:07:48

Jengeni utamaduni wa kusikiliza kwa makini!


Fra Alois mkuu wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè katika tafakari zake kwa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaokwenda kwenye Jumuiya hii ili kujichotea hekima, ufahamu na maarifa ya maisha ya kiroho anawakumbusha kwamba, pale ambapo mwanadamu anateseka anakuwa na matumaini ya kupata faraja na nafuu katika maisha yake; anatamani kukutana na mtu ambaye yuko tayari kujisadaka kwa ajili ya kumsikiliza kwa makini, kumbe hapa kuna umuhimu wa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini ili kuwasaidia watu wanaoteseka: kiroho na kimwili!

Fra Alois anasema, utamaduni wa kusikiliza kwa makini ni tiba muafaka kwa magonjwa mengi yanayomsibu mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Kuna haja ya kufanya matendo ya huruma kwa kuwatembelea: wagonjwa, maskini, wafungwa, wakimbizi na wahamiaji, haya ni makundi ya watu wanaoteseka, watu wanaohitaji kuonja huruma na upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya jirani zao.

Vijana wanachangamotishwa kujijengea utamaduni wa kuwatembelea watu wenye shida na mahangaiko ya ndani, ili kujenga mshikamano wa upendo na udugu kati ya watu badala ya kuwageuzia kisogo kama inavyojionesha na wengi kutokana na ubinafsi pamoja na uchoyo mambo yanayoendelea kumwanadama mwanadamu wa leo! Vijana wanapewa mwaliko wa kuondoa moyo wa jiwe na kujiwekea moyo wa nyama, unaoguswa na shida na mahangaiko ya jirani zao. Wanakumbushwa kwamba, Yesu mwenyewe katika maisha na utume wake, alijitambulisha kwa njia ya watu maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Kuna watu ambao wanateseka, watu ambao wanaishi katika hali na mazingira magumu, matokeo yake, watu kama hawa wamekata na kujikatia tamaa ya maisha na matokeo yake wanajikuta wakitumbukia katika ulevi wa kupindukia pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Watu hawa wakionjeshwa moyo wa upendo na ukarimu, wanaweza kubadilika na kuwa watu wema zaidi, hakuna mtu aliyezaliwa barabarani pasi na familia!

Kumbe, kuna haja ya kuwaonjesha matumaini mapya katika mchakato wa maisha, kwa kuwasaidia kutambua hali yao sanjari na kuwapatia mbinu za kuweza kujikomboa kutokana na hali kama hii, ili waweze kuwa ni watu wapya zaidi, tayari kutoka kifua mbele, kushuhudia upendo wa Mungu katika maisha yao! Si rahisi kuweza kuleta mabadiliko ya ghafla kwa maskini anasema Fra Alois, lakini jambo la msingi ni kuona kuwa wanaonjesha moto wa matumaini mapya, unaowasaidia wasikate tamaa. Hapa kinachotakiwa ni ushuhuda wa mshikamano wa upendo kati ya watu, hapa kila mtu anaguswa kutoka katika undani wake!

Tafakari itakayoongoza Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kwa mwaka 2015 inaongozwa na kauli mbiu "Yesu anatualika kuvuka mipaka iliyo karibu na ile ya mbali". Lengo ni kuguswa na mahangaiko ya watu: kiroho na kimwili, changamoto inayotolewa na Maandiko Matakatifu. Kwa njia hii watu wanaweza kugundua maana ya maisha na kuendelea kuonja upendo wa Mungu kwa ajili ya watu wake.

Fra Alois anasema, Mwaka 2015 ni muhimu sana kwa maisha na utume wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè, kwani wataadhimisha kumbu kumbu ya miaka 75 tangu Jumuiya hii ilipoanzishwa na miaka 100 tangu alipozaliwa Fra Roger na miaka 10 tangu alipouwawa kikatili. Kilele cha maadhimisho haya ni kuanzia tarehe 9 hadi 16 Agosti 2015, kwa kuwashirikisha waamini kutoka madhehebu na dini mbali mbali duniani. Kwa kusoma alama za nyakati, Fra Alois alipanga hija ya miaka mitatu, ili kujipyaisha tena katika mwanga wa Injili sanjari na ujenzi wa mshikamano kati ya binadamu!







All the contents on this site are copyrighted ©.