2014-07-25 09:40:58

Watakatifu waliosimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Familia!


Wakatatifu Yohane Paulo II na Gianna Beretta Molla, ndio wasimamizi wauu wa Maadhimisho ya Nane ya Siku ya Familia Kimataifa itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 27 Septemba 2015. Ni ujumbe uliotolewa na Kamati kuu ya Maandalizi ya Siku ya Familia Kimataifa huko Philadelphia inayoshirikiana kwa karibu sana na Baraza la Kipapa la Familia.

Askofu mkuu Charles Chaput wa Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani, hivi karibuni katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima ya Mtakatifu Yohane Paulo II, katika Kanisa kuu la Watakatifu Pietro na Paulo Jimbo kuu la Philadelphia alitangaza kwamba, Watakatifu Yohane Paulo II na Gianna Beretta Molla ndio wasimamizi wakuu wa maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa. Itakumbukwa kwamba, Yohane Paulo II ndiye Papa pekee aliyetembelea Jimbo kuu la Philadelphia kunako mwaka 1979 na tangu wakati huo, akapendwa na waamini wengi, ambao hadi leo hii wanamkumbuka sana.

Watakatifu walioteuliwa wanajipambanua sana katika kupenda, kulinda, kutetea na kudumisha misingi bora ya maisha ya ndoa na familia. Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa ni "Upendo ni utume wetu: familia ni hai". Hadi sasa maandalizi ya maadhimisho haya yanakwenda vyema na kwamba, waamini wanaalikwa katika sala zao, kuomba maombezi ya watakatifu Yohane Paulo II na Gianna Beretta Molla, ili waweze kuwasaidia kutolea ushuhuda wa Injili ya Familia kati ya watu wanaowazunguka.

Watakatifu hawa kwa njia ya nyaraka lakini zaidi kwa ushuhuda wa maisha yao wameonesha kwamba, familia ni msingi wa maisha ya kijamii. Mtakatifu Yohane Paulo II kwa ujasiri mkubwa kunako mwaka 1994 alianzisha maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa na kwa mara ya kwanza ikaadhimishwa mjini Roma na baadaye, mwaka 1997 maadhimisho haya yakafanyika huko Rio de Janeiro.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akaadhimisha tukio hili Jimbo kuu la Valencia, Hispania na mwaka 2009, Kardinali Tarcisio Bertone, akamwakilisha Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika maadhimisho haya nchini Mexico. Jimbo kuu la Milano, Kaskazini mwa Italia likawa mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya Saba ya Familia Kimataifa na kuadhimishwa mwaka 2012.

Mtakatifu Gianna Beretta Molla ambaye kitaaluma alikuwa ni daktari wa binadamu aliyeishi kati ya mwaka 1922 hadi mwaka 1962, huko Milano, Kaskazini mwa Italia, aligundulika kuwa na Saratani ya kizazi wakati ambapo alikuwa na ujauzito, akakataa kutumia tiba ambayo ingekuwa na madhara kwa mtoto wake aliyekuwa tumboni, akafariki dunia akiwa na umri wa miaka arobaini, lakini akaacha ushuhuda wa ujasiri wa Injili ya Uhai unaojionesha kwa Gianna Beretta Molla. Akatangazwa kuwa Mwenyeheri kunako mwaka 1994 na hatimaye kuandikwa kwenye orodha ya watakatifu na Yohane Paulo II, miaka kumi baadaye.







All the contents on this site are copyrighted ©.