2014-07-24 15:03:24

Mama Meriam kutoka Sudan akutana na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, siku ya Alhamisi mchana tarehe 24 Julai 2014 amekutana na kuzungumza na Mama Meriam Ibrahim Ishag, mwanamke Mkristo kutoka Sudan aliyehukumiwa adhabu ya kifo na hatimaye adhabu hii kubatilishwa na mahakama ya rufaa nchini Sudan hivi karibuni. Katika mazungumzo haya, Meriam alikuwa ameambatana na mme wake Daniel Wani pamoja na watoto wao wawili.

Mtoto wao mdogo anayeitwa Maya alizaliwa gerezani miezi miwili iliyopita. Familia hii imesindikizwa na Waziri mdogo wa mambo ya nchi za nje wa Italia Lapo Pistelli, ambaye alikuwa nchini Sudan, ili kukamilisha taratibu na mipango ya kuachiliwa huru kwa Mama Meriam kutoka Sudan ambaye pamoja na familia yake wanatarajiwa kwenda kuishi nchini Marekani.

Baba Mtakatifu na wageni wake wameweza kufanya mazungumzo yaliyodumu kwa takribani nusu saa kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha, iliyoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu amemshukuru Meriam na familia yake kwa ushuhuda wa imani ya Kikristo waliyoionesha. Kwa upande wake, Meriam amemshukuru Baba Mtakatifu na watu wote wenye mapenzi mema waliowasindikiza kwa sala na majitoleo yao hadi kuachiliwa huru.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amezungumza na viongozi wa Italia waliokuwa wamemshindikiza Mama Meriam na familia yake, ili kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Baba Mtakatifu ameonesha kuguswa na wote wanaoteseka kutokana na imani yao au ukosefu wa uhuru wa kidini, hasa zaidi kwa Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia.







All the contents on this site are copyrighted ©.