(Vatican Radio)Kila mwaka tarehe 27 Julai, Kanisa Katoliki nchini Uingrereza na
Ireland, husherekewa kama Siku ya Maisha, katika maana ya kuyapenda, kuyalinda na
kuyatetea tangu mwanzo wake hadi hatma yake ya kawaida. Ni siku hasa inayowahusisha
vijana, kuyajali na kuyatunza maisha kwa heshima kwenye kila hatua ya makuzi.
Kwa
ajili ya siku hii, Papa Francisco, amepeleka ujumbe wake , uliotiwa sahihi na Katibu
wa Vatican Kardinali Pietro Parolin, ambamo anatoa wito kwa watu wote wenye mapenzi
mema, kuyafurahia maisha, hasa kwa namna ya kipekee katika kuwajali wale walio katika
mazingira magumu na hatarishi.
Ujumbe huu uliotumwa kwa Kanisa Uingereza,
Ireland, Scotland na Wales, unawataka Wakatoliki kupeleka upendo na huruma ya Kristo,
kama majitoleo ya uzima, kwa wale wanao sumbuka na aina mpya ya umaskini na mazingira
magumu, yanayozidi kujitokeza dhahiri katika jamii ya kisasa kama ilivyoelezwa katika
Waraka wa Kitume wa Injili ya Furaha (cf. Evangelii Gaudium 210).
Mandhari
ya mwaka huu kwa ajili ya Maisha ni Kuishi , Kulinda na kufurahia Maisha tangu mwanzo
wake hadi mwisho wake wa asili. Kwao wote wanao husika na ufanikishaji wa Siku hii
ya Maisha, Baba Mtakatifu Francisco amewapa Baraka zake za kichungaji, akiwatakia
hekima, furaha na amani ya Bwana Mfufuka."