2014-07-22 11:41:28

Uinjilishaji Mpya unajikita katika ushuhuda wa maisha!


Askofu Michael Didi wa Jimbo Katoliki la El Obeid lililoko nchini Sudan amewataka Makleri na Watawa kuishi kile wanachohubiri, ili kuwa kweli ni mfano wa kuigwa kwa vijana na wasichana wanaotamani kujisadaka kwa jili ya Kristo na Kanisa lake. Kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu, watu wengi wanaweza kuvutwa na kuguswa ili kujiunga na Kanisa Katoliki, vinginevyo, Kanisa litakimbiwa na waamini na hapo ndipo kutakapokuwepo kilio na kusaga meno!

Viongozi wa kidini wanapaswa kutambua kwamba, vijana wa kizazi kipya ni kundi lenye udadisi mkubwa, linalojitaabisha kutafuta habari, ujuzi na maarifa; ni kundi ambalo kimsingi linahitaji kuona na kushuhudia imani ikimwilishwa katika matendo adili na kwa njia hii linaweza kuvutwa kushiriki katika utume na maisha ya Kanisa, vinginevyo, vijana watalikimbia Kanisa kwani halina mashiko wala mvuto!

Askofu Michael Didi ameyasema hayo, Jumatatu, tarehe 21 Julai 2014 wakati wa kuhamasisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wajumbe wa Shirikisho la Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA wanaoendelea na maadhimisho ya mkutano wao wa kumi na nane huko Lilongwe, Malawi. Hata waamini wanapaswa pia kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya utakatifu wa maisha unaojionesha katika maisha yao ya kila siku. Uinjilishaji Mpya unajikita katika ushuhuda wa maisha, toba na wongofu wa ndani.

Kwa upande wake, Askofu Martin Mtumbuka wa Jimbo Katoliki la Karonga, Malawi, amegusia umuhimu wa huduma za maisha ya kiroho na taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vya Kikatoliki katika Nchi za AMECEA kama fursa makini katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Taasisi za elimu ya juu, ziwe ni vituo vya urithishaji wa imani, maadili na utu wema. Wahudumu wa maisha ya kiroho katika taasisi hizi wawasaidie wanafunzi kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Yesu katika maisha yao.

Taasisi hizi zitambue kwamba, ni vyombo vya Uinjilishaji, kumbe, Jumuiya za taasisi ya elimu ya juu ziwezeshwe kwa Katekesi makini, Maadhimisho ya Ibada na Sakramenti mbali mbali za Kanisa pamoja na kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika matendo, ili kuleta mvuto na mashiko katika maisha ya watu!







All the contents on this site are copyrighted ©.