2014-07-22 09:47:58

Ongezeni kasi ya kupambana na umaskini miongoni mwa watanzania!


Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania amezitaka taasisi za Serikali nchini humo kuongeza kasi ya kupunguza umasikini miongoni mwa wananchi, akisisitiza kuwa wananchi wamekaa katika umasikini kwa muda mrefu mno kupita kiasi. Rais Kikwete amesema kuwa wanachotarajia wananchi kutoka kwa taasisi za Serikali ni kusaidiwa kutoka kwenye umasikini kwa kasi kubwa zaidi kwa sababu wamekaa katika hali ya umasikini kwa muda wa kupita kiasi.

Rais Kikwete ametoa maelekezo hayo Jumapili, Julai 20, 2014, wakati alipokagua shamba la kisasa la zao la buni kwenye kijiji cha Lipokela, Wilaya ya Songea, ikiwa ni moja ya shughuli zake katika siku ya nne ya ziara yake ya siku sita katika Mkoa wa Ruvuma.

Rais Kikwete amesimama kwenye shamba hilo akiwa njiani kutoka Wilaya ya Mbinga kuelekea Wilaya ya Songea ambako leo amefungua soko la kimataifa katika kijiji cha Mkenda, kilicho mpakani kabisa mwa Tanzania na Msumbiji. Baadaye, Rais amekagua daraja kwenye Mto wa Ruvuma ambalo linaunganisha Tanzania na Msumbiji.

Rais Kikwete ametoa maelekezo hayo baada ya kuambiwa kuwa pamoja na kwamba shamba hilo, pengine ni kubwa kuliko jingine lolote la buni nchini, limefanikiwa kupata miche 3,000,000 ya buni za kisasa ambayo lilihitaji lakini wakulima wa kawaida wa zao hilo la kahawa wanashindwa kupatiwa kiasi hicho hicho cha miche ya buni.

“Kwanini tunashindwa kupata miche milioni tatu kwa ajili ya wananchi ambayo wenyewe mmesema kuwa gharama yake yak uizalisha ni shilingi milioni 900? Kwanini tunashindwa kupata miche ya kutosha ili wakulima wetu wapande na kuongeza kipatoc hao?” Rais Kikwete amemwuuliza Profesa James Teri, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Kahawa Tanzania (TACRI).

Ameongeza Rais Kikwete: “Hatuwezi kuwabakiza wananchi wetu katika umasikini kwa miaka mingine 30 kwa sababu tu hatuna uwezo wa kuzalisha miche ya kutosha. Hatuwezi kufanya hivyo, wameishi kiasi cha kutosha katika umasikini.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “Kazi yetu ni kuwatoa watu wengi zaidi katika umasikini kwa haraka kubwa zaidi kwa sababu wamechelewa mno. TACRI inaweza kufanya hivyo kwa kuwapa wananchi mbegu bora zaidi ya buni, ili waondokane na mibuni ya zamani ambayo uzalishaji wake ukochini. Hivyo, nataka kujua tunaweza kufanya nini kufanikisha hili siyo kuniambia habari ya changamoto ambazo TACRI inakumbana nazo katika kutimiza majukumu yake.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Siridhiki na kasi ya kujaribu kuwatoa watu wetu katika umasikini. Nahitaji kupata miche milioni tatu kwa ajili ya wananchi wetu. Kama iliwezekana kulipatia shamba hilo miche milioni tatu kwa nini isiwezekane kwa wananchi?”
Shamba hilo kubwa la mibuni (inayozalisha kahawa) ni mali ya Kampuni ya AVIV, ambayo ni kampuni tanzu ya Kampuni ya Olam International, ambayo inaendesha shughuli za biashara katika nchi 65 duniani. Olam iliingia Tanzania miaka 20 iliyopita na shughuli zake kubwa ni katika mazao ya korosho na kiwanda cha kuchambua pamba kilicho Bunda, Mara.

Duniani, Olam ina mashamba ya mibuni katika nchi tano ambazo ni Tanzania, Zambia, Ethiopia, Laos na Brazil. AVIV ambayo inapanda mibuni ya kuzalisha kahawa yaa ina ya Arabica ilipanda miche ya kwanza miaka mitatu iliyopita na inakaribia kuvuna kwa mara ya kwanza. Katika kijiji hicho cha Lipokela, AVIV ina ardhi yenye ukubwa wa hekta 2,000.


Wakati huo huo habari kutoka Dar es Salaam zinasema kwamba, Viongozi wa Wakuu wa Mikoa nchini Tanzania wameaswa kufahamiana kama viongozi ili kubadilishana uzoefu wa kujenga mtandao wa mawasiliano na mahusiano kwa ajili ya kupashana habari na kushauriana. Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Idd wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Wakuu wa Mikoa (RC) na Makatibu Tawala Mikoa (RAS) nchini Tanzania, Jumatatu tarehe 21 Julai 2014, Jijini Dar es salaam.

“Jengeni mshikamano wa mahusiano katika utendaji kazi wenu mkiimarisha maelewano miongoni mwenu mtarahisisha utendaji na kuepuka migogoro isiyo ya lazima” alisema Balozi Seif. Balozi Seif aliendelea kusema, “Tumieni nafasi hii kufahamiana muweze kujenga mtandao wa mahusiano, mawasiliano mkiimarisha mashirikiano ili kuleta maendeleo katika maeneo yenu ya kazi kwa manufaa ya wananchi”.

Balozi Seif alisema kuwa kila kazi inachangamoto zake, katika kutekeleza majukumu yao vizuri na kubainisha kuwa viongozi hawa baadhi yao wamekuwa na misuguano ya hapa na pale ambayo husababishwa na mawasiliano yasiyoridhisha. Balozi Seif alisisitiza kuwa dawa ya misuguano hiyo itapatikana kupitia mafunzo hayo ya siku tatu ambapo viongozi hao watakumbushwa mengi waliyoyasahau, watapata mengi ya kujifunza, kujikumbusha na kujinoa ili kuhuisha uhai wa utekelezaji wa majukumu yao ambao utaleta mshikamano na umoja miogoni mwa watendaji hao.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Hawa Ghasia alipokuwa akimkaribisha Mgeni Rasmi alisema kuwa mafunzo hayo yataimarisha mahusiano na mawasiliano ya viongozi hao katika kutekeleza majukumu yao ili yapate tija iliyokusudiwa.
Waziri Ghasia amewaasa viongozi hao kuwa wasipofanya kazi kama timu hawawezi kupata tija katika maeneo yao ya kazi hasa katika kuwaletea maendeleo wananchi wanaowaongoza na nchi kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akimshukuru na kumhakikishia Mgeni Rasmi Balozi Seif kuwa wanamatumaini makubwa kuimarisha mahusiano kati yao vilevile na wanasiasa wote na kuahidi kuwa watatoa huduma bora zaidi.








All the contents on this site are copyrighted ©.