Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni, tarehe 20 Julai 2014 alipiga simu na kuzungumza
na Patriaki Ignatius Youssef Younan wa III wa Kanisa Katoliki la Siro, Antiokia, kuonesha
mshikamano wake wa kiroho na Wakristo pamoja na raia wasiokuwa na hatia wanaoendelea
kuteseka nchini Iraq, hasa mjini Mosul ambako vita inazidi kupamba moto!
Taarifa
zinaonesha kwamba, mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Ignatius
yamedumu kwa takribani dakika tisa na kwamba, Patriaki amemshukuru sana Baba Mtakatifu
kwa kuguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya wananchi wa Iraq. Baba Mtakatifu anawaomba
wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuongeza nguvu kusitisha vita hii ambayo inaonekana
kuwa na mlengo wa madhulumu ya kidini zaidi.
Baba Mtakatifu anasikitishwa
na ukimya unaoneshwa na Jumuiya ya Kimataifa kutokana na mauaji yanayoendelea huko.
Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea waamini na wananchi wote wa Iraq ambao kwa
sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha. Wakristo eneo la Mosul wanazidi kutoweka
baada ya kukaa katika eneo hili kwa kipindi cha zaidi ya miaka elfu mbili. Baadhi
yao wamekimbilia kutafuta hifadhi ya kisiasa huko Kurdstan.
Itakumbukwa kwamba,
Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano
wa kimataifa mjini Vatican, tarehe 19 Julai 2014 alikutana na kuzungumza na Patriaki
Younan mjini Vatican.