2014-07-22 09:20:28

Jifunzeni kutoka kwa Yesu!


Kardinali Zenon Grocholewski, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la elimu Katoliki amewataka walezi, walimu na wanafunzi kurudi kwenye shule ya Yesu ili kuweza kujifunza mambo msingi katika maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili, kwani Yesu Kristo ndiye kiongozi mkuu na rejea katika malezi kamilifu ya mwanadamu. RealAudioMP3

Kardinali Grokolewski ameyasema hayo katika barua aliyowaandikia washiriki wa Kongamano la Elimu Katoliki lililoandaliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya na kusomwa na Katibu mkuu msaidizi wa Baraza Padre Michael Remery. Kardinali Grocholewski amewakumbusha wajumbe kwamba, sekta ya elimu kwa sasa inakumbana na changamoto kubwa inayowataka walimu kubadilika na kujisadaka zaidi kwa kuonesha ukarimu, majitoleo binafsi pamoja na kufanya tathmini ya kina kuhusu utume wao kama walimu.

Amewataka walimu kutambua kwamba, majiundo makini ya Kikristo kwa ajili ya walimu na maisha yao ya kiroho ni muhimu sana na ni kati ya changamoto endelevu zinazopaswa kufanyiwa kazi. Utambulisho wa Mwalimu Mkatoliki hauna budi kujionesha katika utume wake kwani hii ni sehemu ya vinasaba vya maisha yake kama sehemu ya mchakato unaomshirikisha katika kazi ya Mungu. Mwalimu anayo dhamana ya kusaidia majiundo ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, kuna uhusiano wa karibu sana kati majiudno ya Kikristo yanayofanywa kwa ajili ya walimu na uinjilishaji ambao ni sehemu ya utume wao.

Uinjilishaji Mpya ni mchakato unaokwenda sanjari na historia ya mtu mzima; maendeleo yake na maisha yake ya kiroho. Jambo msingi linalotiliwa mkazo na Mama Kanisa katika mchakato wa majiundo ya mwanadamu: kiroho na kimwili ni ushuhuda makini unaotolewa na wahusika. Haitoshi kuwa wataalam kwa mambo wanayofundisha, kupata mafanikio makubwa kutokana na weledi wa mbinu za kufundishia pamoja na teknolojia.

Hapa jambo la maana zaidi ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaokumbatia ukweli, uzuri na wema unaobubujika kutoka katika undani wa maisha ya mwalimu mwenyewe.

Kwa upande wake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika ujumbe wake anabainisha kwamba, dhamana ya Walimu Wakatoliki ni muhimu sana si tu katika maendeleo na ustawi wa Kanisa, bali kwa ajili ya mafao ya wengi ndani ya Jamii kwa sasa na kwa siku za usoni.








All the contents on this site are copyrighted ©.