Balozi wa Vatican nchini Angola asikitishwa na Serikali kuchelewa kutoa kibali cha
kurusha matangazo kwa Radio Ecclesia!
Askofu mkuu Novatus Rugambwa, Balozi wa Vatican nchini Angola ameonesha masikitiko
yake makubwa kutokana na Serikali ya Angola kuchelewesha kutoa ruhusa kwa Radio Ecclesia
kuongeza nguvu ya matangazo yake ili yaweze kusikika nchi nzima. Hadi wakati huu,
matangazo ya Radio Ecclesia yasikika mjini Luanda, Angola peke yake, ingawa ni Radio
ya siku nyingi iliyoanzishwa kunako mwaka 1954.
Radio hii katika uhai wake
imekumbana na misukosuko mingi kiasi hata cha kufungiwa kurusha matangazo yake na
Serikali ya MPLA, baada ya Angola kujitwalia uhuru wake. Radio Ecclesia ni kati ya
njia muhimu sana za mawasiliano nchini Angola na kwa kipindi cha miaka mingi imeomba
ruhusa ya kupata kibali cha kurusha matangazo yake nchi nzima lakini hadi sasa hakuna
mafanikio yoyote.
Askofu mkuu Novatus Rugambwa anasema, watu wana kiu ya kusikiliza
matangazo yanayorushwa na Radio Ecclesia, kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji
mpya, unaokwenda sanjari na matumizi ya njia za kisasa za mawasiliano ya jamii. Askofu
mkuu Rugambwa ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa anahojiwa na Radio Saut ya Ujerumani
alipokuwa anatembelea Jimbo Katoliki la Benguela.
Kwa mara ya kwanza Askofu
mkuu Rugambwa tangu aanze utume wake nchini Angola kunako mwaka 2010 ameonesha masikitiko
haya makubwa. Itakumbukwa kwamba, kwa sasa kuna mkutano unaoendelea mjini Luanda kwa
nchi zile zinazozungumza Kireno na kwa mara ya kwanza mkutano huu unafanyika nchini
Angola.