2014-07-21 15:00:59

Upendo na Ukarimu kamwe havina likizo- Papa .


Mungu humpenda zaidi mtu mkarimu, anayetoa kwa moyo mkunjufu. Na hivyo twapaswa kujifunza kutoa kwa ukarimu, na kujitenga na kupenda mali. Ni ujumbe wa Papa uliochapishwa katika ukurasa wake wa Tweet @ Pontifex. Ujumbe ambamo Papa Francisco anarudia kukemea migawanyiko na utengano unaojitokeza hasa wakati huu wa mgogoro wa kiuchumi.
Mosinyori Henry Feroci, Mkuu wa kitengo cha Caritas Roma, ameufafanua zaidi kwa ujumbe wa Papa akisema, kuna mambo mawili. Kwanza: Papa Francisco anatukumbusha kwamba kimsingi kwa Wakristo, kama si watu wenye upendo , basi hawako katika moyo wa Mungu, kwa sababu Mungu ni upendo. Hii ina maana kwamba Mkristo, kama kweli anataka kuwa karibu na Bwana, ni lazima awe tayari kwakati wote, kuhudumia wengine, kwa kuwa, hiyo ndiyo maana ya kweli ya upendo.
Na wazo la pili, Papa Francisco anatukumbusha kuwa katika nyakati hizi ngumu, nia na malengo yetu hayapaswi kuweka kando heshima na mshikamano na watu walio katika matatizo makubwa ya kihali : watu wanaougua kilio cha vita, , watu wenye shida za maradhi, watu waliokosa ajira, wasio na makazi, wasio na chakula na mahitaji mengine msingi ya kila siku.
Lakini juu ya yote, Mons. Feroci ameonyesha imani yake kwamba, leo kuna haja ya kuwa makini katika utoaji wa huduma huo, kujua kweli wenye shida na wahitaji , ni kufungua macho yetu na kuona nini kinachomtokea ndugu yetu aliyebaki hoi njiani kama ilivyokuwa kwa mfano wa Msamaria mwema.
Katika maana hiyo, Papa anapenda kutuambia kwamba, upendo kamwe hauendi likizo ... Upendo upo katika mduara wote wa siku za mwaka 365, kwa Wakristo ni wajibu na haki kupenda. Na hivyo likizo la fadhila pengine linaweza kutokea tu kwa wale ambao hawawezi kumudu, ambao kila siku wanaishi katika mazingira magumu na shida, wana hamu ya kutoa mchango wao wa wema na pia kujisikia kama ni haki yao, kuwa karibu na Wakristo wengine, lakini hawawezi kufnaya hivyo kutokana na mazingira magumu wanayoyaishi.
Mons Feroci, anasema, Papa Francisco amekuwa mfano huo mzuri wa daima upendo hauna likizo,bali wakati wote ni wa huduma kwa ajili ya wengine. Na hivyo katika wakati wa mgogoro wa uchumi wa wakati huu, Papa anatoa mwaliko mpya katika dhana ya kushirikishana na kugawana tulicho nacho. Kugawana iwe kipengele muhimu katika maisha ya kijamii yenye upendo na huduma, kipengele muhimu katika elimu ya kuvunja mkate, na kuula wote, kama haki msingi kwa waamini, wanaokula na kunywa, mwili na Damu ya Kristo, mkate uliovunjwa kwa ajili ya wengine ...








All the contents on this site are copyrighted ©.