Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kuanzia tarehe 9 Julai hadi tarehe 16 Agosti 2015 itaadhimisha
kilele cha Jubilee ya miaka 75 tangu kuzaliwa kwa Muasisi wake Fra Roger na miaka
10 tangu alipofariki dunia. Ni tukio linalotarajiwa kuwakutanisha vijana wa kiekumene
kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wawakilishi wa dini na serikali pamoja na maskini
na wale wanaohudumiwa na Jumuiya hii.
Mwezi Julai
2015, vijana wanaoishi katika Monasteri au katika nyumba za kitawa watashirikishwa
ili kukutana na kuzungumza na wakuu wa mashirika ya kimonasteri na kitawa kutoka Makanisa
ya Kiorthodox, Kikatoliki na Kiluteri. Kati ya viongozi mashuhuri wanaotarajiwa kuwepo
ni pamoja na Padre Adolfo Nicolas, Mkuu wa Shirika la Wayesuit, Padre Bruno Cadorè,
Mkuu wa Shirika la Wadomenikani pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa kwa upande
wa wanawake.
Mwezi Septemba 2015 kutafanyika Kongamano la Kimataifa kuhusu
mchango wa Frà Roger katika masuala ya kitaalimungu, tema itakayochambuliwa na Kardinali
Walter Kasper, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa umoja wa Wakristo.
Hapa vijana waliobobea katika taalimungu watashiriki kikamilifu, ili kutoa mchango
wao wa jinsi wanavyomfahamu Frà Roger.
Taarifa zinazonesha kwamba, kuanzia
Mwezi Julai kuna mikutano muhimu inayoendelea kufanyika kwenye Jumuiya ya Kiekumene
ya Taizè. Kila Jumapili, vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanafika kwenye
Makao makuu kwa muda wa juma zima, ili kusali na kutafakari kuhusu Neno la Mungu.
Vijana wengi kutoka Italia wanatarajiwa kuhudhuria huko mwishoni mwa mwezi Julai hadi
mwezi Agosti. Fra Alois ndiye anayewaongoza vijana hawa katika tafakari ya kina inayohimiza
upendo na mshikamano wa kidugu kati ya watu.