Maisha Mchanganyiko ya Kijamii- Mhamiaji- Sehemu ya kwanza
Baada ya kuzungumzia Wakimbizi katika maisha mchanganyiko ya kijamii, leo na tutazame
kundi jingine la watu, nao ni Wahamiaji, kundi ambalo uwepo wake si rahisi kukwepeka
katika maisha ya kawaida ya kijamii, hasa katika ulimwengu wa leo wa utandawazi. Uhamiaji
wa binadamu ni harakati na watu kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa nia ya kutaka
kuwa na maisha tulivu zaidi katika eneo jipya. Kwa kawaida mtu anayeitwa mhamiaji
ni yule anayetoka umbali mrefu, au kutoka nchi moja hadi nyingine, au bara hadi bara,
lakini pia kuna uhamiaji wa ndani ya nchi. Uhamiaji unaweza kuwa , mtu binafsi, familia
au muungano wa familia na hata makundi makubwa, ilivyo historia nyingi za wakulima
na wafungaji , wanaohama kutoka eneo moja hadi jingine, kutoka wilaya hadi wilaya
au mkoa hadi mkoa, nchi hadi nchi. Aidha kulingana na mazingira ya kihistoria, hali
na mtazamo, pia kuna wahamiaji wanaoitwa kama walowezi, kama walivyo walowezi Wazungu
Afrika Kusini. Wote hao, huwa na sifa moja kuu, hamu ya kuhamia eneo jipya kwa lengo
la kutafuta maisha yaliyo bora zaidi. Katika utambuzi kwamba, moyo wa binadamu
umeumbwa na hamu ya kutaka kupata mengi zaidi, ufahamu, elimu, mali, maisha, miliki,
mamlaka na kadhalika, hupata msukumo mkali wa ndani, kwenda kutafuta hayo. Na ndivyo
ilivyokuwa tangu zama za kale, hata kwa wale wanaoitwa wavumbuzi, kama Christopher
Columbus, Marco Polo , Newton, n.k, walifunga safari za mbali kwenda kutafuta yanayofaa
zaidi katika maisha. Na pia ndivyo kwa wanasayansi, wanatafuta kuboresha maisha ,
kama ilivyo dhahiri leo hii kwamba, mtu hushinda Afrika na kupata kifungua kinywa
chake barani Ulaya. Hulala China na kuamka Marekani! Ulimwengu ambamo sasa watu wanashirikishana
soga kama vile wako chumba kimoja, na kumbe wanatenganishwa na umbali wa maelfu ya
kilomita. Kwa hakika haya ni maendeleo ya kasi. Ni katika hamu hiyo asili ya
binadamu, kuyatafuta maisha yaliyo bora zaidi, ambamo mna matokeo ya kutaka kuyahama
matatizo na kwenda mahali penye ahueni kimaisha. Hamu ya kuboresha maisha inayo usukuma
moyo wa mtu kuhama , iwe kwa wale wanaohama kutoka Ulaya kwenda Afrika au wanaotoka
Afrika kwenda Ulaya . Wote nia yao kuu ni kutafuta mahali wanapoweza kufanikisha maisha
bora zaidi, kuliko wakibaki katika maeneo yao asilia. Katika hali hiyo, mhamiaji
basi ni nani. Na kuna manufaa yoyote ya kuwa mhamiaji? Na tunazama katika mada hii
kwa kurejea ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisco alio utoa kwa ajili ya Wahamiaji na
Wakimbizi kwa mwaka 2014. Ujumbe aliouandika chini ya Jina : Wahamiaji na Wakimbizi:
Kuelekea Dunia iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu Francisco, katika ujumbe huo,
ameyatafakari mapito ya kijamii katika nyakati hizi akisema kwamba, katika njia zisizo
za kawaida, Jamii ya binadamu sasa inapita katika mchakato wa kutegemeana pamoja na
mwingiliano usiokuwa wa kawaida katika ngazi zote hata kimataifa. Na hivyo ni wakati
ambamo hakuwezi kukosa changamoto na matatizo, hasa katika taratibu zinazolenga kuboresha
hali ya maisha ya familia ya binadamu, si tu kiuchumi, lakini pia kisiasa na kiutamaduni
sawia. Ujumbe wa Papa unatahadharisha kwamba, cha msingi katika maisha haya mchanganyiko,
ni kukumbuka kwamba, kila mtu ni sehemu ya ubinadamu na ni mmoja wa familia nzima
ya watu na matumaini yote ya maisha bora ya baadaye. Kwa hisia hizo , Baba Mtakatifu
Francisco ameeleza , ndizo zilimsukuma kuchagua mada ya Wahamiaji na wakimbizi, kulekea
dunia iliyo bora zaidi, isindikize mwaka huu katika kuwapokea wahamiaji na wakimbizi.
Papa ameendelea kutazama kukua kwa wimbi la binadamu kuhama, akirejea maneno
yaliyotolewa na mtangulizi wake, Papa Benedict XVI, kwamba hii ni “ishara ya nyakati"
( ujumbe kwa mwaka 2006 kwa Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani). Uhamiaji mara
nyingi huashiria au kutangaza kushindwa au uwepo wa mapungufu ndani ya eneo , Nchi
au jumuiya ya kimataifa katika kukomesha madhulumu dhidi ya ubinadamu . Lakini pia
kwa upande mwingine, huonyesha hamu ya binadamu kufurahia umoja na mshikamano uliosimikwa
katika mitazamo ya kuheshimu tofauti, kukubalika na ukarimu katika kushirikiana na
mgawanyo sawa wa mali za hapa duniani, na kwa ulinzi na maendeleo ya hadhi na umuhimu
wa kila binadamu. Papa alifafanua kwa upande Ukristo, hali halisi ya uhamiaji,
kama ilivyo katika hali halisi nyingine za haki za binadamu, huashiria mvutano kati
ya uzuri wa viumbe, unaojionyesha katika neema ya ukombozi na fumbo la dhambi. Mshikamano,
kukubalika, na ishara ya udugu na ufahamu wa uwepo huenda sambamba na kukataliwa,
ubaguzi, biashara haramu na unyonyaji, mateso na kifo. Na hasa kinachosumbua ni zile
hali ambamo uhamiaji unakuwa tena si jambo la hiari, lakini kama matokeo ya mashinikizo
yaliyo nje ya ubinadamu. Mtu kulazimika kukimbia madhulumu mbalimbali ya utendaji
haramu wa binadamu, kama kazi za sulubu, kutekwa nyara, na mateso ya mengine ya
mwili yakiwemo mauaji na utumwa. Leo hii kazi za kutumikishwa katika hali ya utumwa
limekuwa ni jambo la kusikika. Lakini pamoja na matatizo na hatari na hali ngumu zilizoko
mbele yao, bado watu wanahama maeneo yao kwa wingi, wakiwa wamejawa na imani na tumaini
thabiti, kwamba huko wanakokwenda wataweza kuwa na maisha bora ya baadaye, si tu
kwa ajili yao wenyewe lakini kwa familia zao na wale walio karibu nao. Ujumbe
wa Papa Francisco unaendelea kututaka tujiulize nini hasa kinacho hitajika katika
kujenga ulimwengu ulio bora zaidi kwa maisha? Je haipaswi kulenga katika maendeleo
halisi na muhimu yenye kuheshimu ya maisha ya kila mtu, katika kutafuta majibu yanayo
faa kukidhi mahitaji ya watu binafsi na familia, na kuhakikisha kwamba zawadi ya Mungu
ya maisha inaheshimiwa, kulindwa na kudumishwa ? Papa Francisco alihoji na kurejea
waraka wa Papa Paul VI, juu ya Maendeleo ya Watu, 6, ambamo ameeleza kuwa, matarajio
ya watu leo hii, ni uhakika wa kupata chakula, tiba kwa magonjwa na ajira ya kuridhisha
, kama utendaji zaidi katika uwajibikaji binafsi, kutenda zaidi, na kujifunza zaidi,
na kuwa na mali na maisha bora zaidi .
Moyo wa binadamu una hamu ya kutenda
zaidi na zaidi, kupata maarifa na zaidi au mali zaidi na zaidi n.k. Lakini maendeleo
hayawezi kuwa ya ukuaji wa uchumi peke yake , bali pia ni muhimu kuzingatia hoja
zingine katika ubinadamu na mwelekeo wa mtu, ikiwa ni pamoja mambo ya kiroho. Mapapa
wote wanasisitiza , asiwepo mtu wa kupuuzwa, licha ya hali yake ya umaskini, ugonjwa,
kufungwa, au kuwa mgeni, au mhamiaji au mkimbizi (cf. Mt 25:31-46). Na hili linaweza
kufanikishwa kwa kuachana na utamaduni wa ulafi na ubinafsi wa kujilimbikizia , bali
kwa kujenga utamaduni wa umoja na mshikamano katika kugawana na kushirikishana utajiri
wa dunia na kuwakubali wengine. Baba Mtakatifu Francisko anaonya , kwa mtazamo
huo, Mhamiaji hapaswi kuchezewa kama kete katika bao. Wahamiaji ni watu wa kawaida
ambao, kwa msukumo asilia wa ndani ya moyo na kwa sababu mbalimbali , huamua kuondoka
katika maeneo yao na kwenda sehemu nyingine kujaribu kuboresha maisha si kwa ajili
yao tu lakini pia kwa familia zao na jamii zao. Leo hii takwimu za Idadi ya watu,
wanaohama kutoka nchi hadi nchi au bara hadi bara jingine, au kuhama maeneo ndani
ya nchi zao na maeneo ya kijiografia, ni kubwa pengine kuliko hata ilivyowahi kutokea
kihistoria. Kanisa tangu mwanzo wake , daima huambatana na wahamiaji katika
safari yao, na hasa hupenda kuelewa chanzo cha uhamiaji, ili liweze kutenda vyema
zaidi na kuondokana na madhara yake hasi, ila kuongeza ushawishi wake chanya kwa jamii
asilia, walio katika kuhama na hatima ya safari yao.
Na hivyo, wakati maendeleo
ya ulimwengu bora yanapohimizwa , Mama Kanisa, hawezi kukalia kimya kashfa ya umaskini
katika hali zake zote, na hasa ikikuzwa na vurugu, unyonyaji, ubaguzi, vikwazo mbinu
kwa uhuru wa kimsingi, iwe kwa mtu binafsi au kwa vikundi. Mara nyingi haya yameonekana
kuwa sababu msingi zinazofanya uwepo wa wimbi la watu kuingia katika harakati za
kuhamahama, ikionyesha uwepo wa uhusiano kati ya uhamiaji na umaskini. Waliokimbia
kutoka hali ya umaskini uliokithiri au mateso kwa matumaini ya maisha bora ya baadaye,
au tu ili kuokoa maisha yao wenyewe, kwa sababu hizo, mamilioni ya watu huchagua kuhamia
maeneo mengine. Bahati mbaya pamoja na matumaini na matarajio yao, wao mara nyingi
hupambana na kutoaminiwa, kukataliwa na kutengwa, na hata kunyimwa uhuru wa dhamiri
na kupokonywa heshima ya ubinadamu wao. Katika ukweli wake, Papa Francisco alisisitiza
, uhamiaji leo hii, katika mtazamo mpana wa utandawazi, unahitaji mtazamo na mbinu
mpya katika kusimamia, kulinda usawa kwa ufanisi zaidi , na hili linahitaji ushirikiano
wa kimataifa, huruma kubwa. Imeandaliwa nami T.J.Mhella.