Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani limesema kwamba, litaendeleza ushirikiano na
mshikamano na nchi za AMECEA ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea
kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Ushirikiano kati ya Baraza
la Maaskofu Katoliki Marekani na Kanisa Barani Afrika umekuwa ni wa manufaa kwa pande
hizi mbili, tangu uhusiano huu ulipoanzishwa wakati wa utekelezaji wa Waraka wa kichungaji
wa Papa Yohane Paulo II, Kanisa Barani Afrika, Ecclesia in Africa.
Hayo yamesemwa
na Askofu Joseph W. Tobin, mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, mwishoni
mwa juma, kwenye maadhimisho ya mkutano wa kumi na nane wa AMECEA unaoendelea mjini
Lilongwe, Malawi. Anasema misaada ya kiutu na kimaendeleo imepokelewa kwa mikono miwili
na Kanisa Barani Afrika na kwamba, kwa sasa wanataka kujielekeza zaidi katika kuwezesha
majiundo makini ya mihimili ya Uinjilishaji mpya kwa Maaskofu Katoliki Kenya, Ethiopia
na Tanzania.
Askofu Charles Kasonde wa Jimbo Katoliki la Solwezi, Zambia akiwasilisha
mada yake kwenye mkutano wa AMECEA anabainisha kwamba, seminari na nyumba za malezi
ni vituo muhimu sana kwa ajili ya kufunda mihimi ya Uinjilishaji Mpya Barani Afrika
na kwamba, majiundo awali na endelevu yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika
maisha na utume wa Mapadre. Kanisa linaendeleza dhamana na utume wake wa utangazaji
wa Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia na kwamba, hili ni jukumu la Wakristo
wote, lakini Makleri wana mchango wa pekee!
Naye Askofu Paul Njiru Kariuki
wa Jimbo Katoliki la Embu, Kenya katika mahubiri yake kwenye Ibada ya misa takatifu,
iliyoadhimishwa hapo tarehe 19 Julai 2014 amewataka Mapadre kuiga mfano wa Bikira
Maria, Mama wa Mungu na Kanisa kwa kuonesha unyenyekevu na tayari kutekeleza mapenzi
ya Mungu katika maisha na utume wa Kanisa.
Anasema, maadui wakuu wa Uinjilishaji
mpya ni Makleri na waamini wanaoshindwa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha
yao, changamoto kwa Taifa la Mungu katika nchi za AMECEA kuiga mfano wa Bikira Maria
katika unyenyekevu na utayari wa kutekeleza mapenzi ya Mungu. Viongozi wa Kanisa wasaidie
juhudi za kumpeleka Yesu Kristo katika familia na jamii inayowazunguka; kwa kuwafariji
wale waliokata tamaa pamoja na kuwajengea uwezo maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii ili waweze kukabiliana kikamilifu na changamoto za maisha. Vijana wanapaswa
kusaidiwa ili kuwa na mwelekeo makini wa maisha, vinginevyo watachanganyikiwa na kukosa
dira ya maisha.
Askofu Kariuki anawakumbusha wajumbe wa mkutano mkuu wa kumi
na nane wa AMECEA kwamba, Bikira Maria alikuwa ni mwanamke aliyesheheni furaha, imani
na matumaini, kama inavyojidhihirisha katika utenzi wa Bikira Maria, "Magnificati".
Kumbe hata Kanisa katika nchi za AMECEA linapaswa kuwa ni kielelezo cha imani, matumaini
na furaha.
Professa Clement Majawa kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika
Mashariki na Kati, CUEA, anawahimiza Maaskofu wa AMECEA kuibua mbinu mkakati utakaopambana
fika na vikwazo vya imani kwa watu wa nyakati hizi. Umefika wakati wa kusoma alama
za nyakati, ili hatimaye, kuibua mbinu mkakati wa Uinjilishaji Mpya ili kuwajengea
waamini imani inayojielekeza katika ukweli, toba na wongofu wa ndani. Viongozi wa
Kanisa hawana budi kuwaendea waamini wao huko waliko kwa kuanzia kwenye Familia ili
kukabiliana na changamoto za Uinjilishaji.
Kuibuka na kuenea kwa madhehebu
ya Kikristo Barani Afrika, imani za kichawi na kishirikina, ibada za mashetani, ukabila,
udini, uchu wa mali na madaraka na umaskini ni mambo ambayo yanaonesha udhaifu mkubwa
katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya kibinadamu: kiroho
na kimwili. Imani kwa Kristo na Kanisa lake inapaswa kushuhudiwa katika matendo adili
na manyofu. Mikakati ya Uinjilishaji mpya ipanie kuziba mianya ya utupu wa maisha
ya kiroho inayowaandama waamini kwa kukazia toba, wongofu wa ndani na ushuhuda wa
maisha.
Professa Clement Majawa anasema kwamba, Uinjilishaji Mpya ni mchakato
unaokazia kwa namna ya pekee Katekesi ya kina kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa,
Maisha adili kadiri ya Amri za Mungu na Maisha ya Sala. Maisha ya kiroho hayana budi
kuwa na uwiano na maisha ya kila siku, vinginevyo, Kanisa litakuwa na watu ndumilakuwili,
wenye kubeba Biblia mikononi, lakini wanakesha usiku makaburini!